
Timu za upelelezi za Iran zimefanikiwa kusambaratisha seli nne za wanamgambo wa Kitakfri wenye mfungamano na utawala wa Israel katika mkoa wa Sistan na Baluchistan, kusini mashariki mwa Iran mkoa unaopakana na Pakistan.
Wizara ya Intelijensia ya Iran ilitangaza katika taarifa yake siku ya Jumanne kwamba wanachama 19 wa seli zenye uhusiano na Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) wamegunduliwa na kukamatwa katika mkoa wa Sistan na Baluchistan kufuatia operesheni kadhaa kubwa zilizofanywa na Idara ya Intelijinsia ya Iran.
Mamluki hao wa Israel walikuwa wakipanga kufanya hujuma za ugaidi lakini walikamatwa kabla ya kufanya lolote.
Taarifa ya Wizara ya Intelijensia ya Iran imeeleza kuwa, katika opareshehi hizo kubwa, timu za ujasusi vimekamata kiasi kikubwa cha silaha nyepesi na nzito, ikiwa ni pamoja na bunduki aina ya DShK M1938, maguruneti kadhaa, bunduki tano aina ya Kalashnikov, bastola sita na idadi kubwa ya risasi n.k.
Wizara ya Intelijensia ya Iran imeeleza kuwa magaidi waliokamatwa si Wairani. Watu hao walisajiliwa na makundi ya kigaidi ya Takfiri yenye makao yake katika nchi jirani za mashariki mwa Iran na walipewa mafunzo ya jinsi ya kufanya mashambulizi ya mabomu.
