Ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa umepuuzilia mbali mkutano wa Baraza la Usalama la umoja huo ulioitishwa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran ukiutaja kuwa ni “onyesho lingine la unafiki,” na kusisitiza kwamba hakuna msingi wa kisheria wa kutumia azimio lililopitwa na wakati kuiwekea vikwazo Tehran.

Baraza la Usalama la UN lilikutana jana Jumanne chini ya ajenda kuhusu Kamati ya 1737, chombo cha vikwazo kilichoanzishwa mwaka wa 2006, baada ya kura ya kiutaratibu iliyopitishwa kwa 11-2 huku wanachama wawili wakijizuia kupiga kura. Russia na China zilipiga kura ya kupinga kuitishwa mkutano huo, huku Pakistan na Somalia zikijizuia kupiga kura.

Taarifa iliyotolewa na ujumbe wa Iran UN imesema: Baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama, kwa amri ya Marekani, wamekariri madai yasiyo na msingi dhidi ya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran na kurudia kampeni ya kutoa taarifa potofu ya Marekani na utawala wa Israel kama “kasuku,”.

“Hili ni onyesho lingine la unafiki na unduumakuwili katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,” ujumbe huo umesema.

Mkutano huo ulimalizika bila matokeo yoyote, na hakuna mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyewasilisha ripoti.

Ujumbe wa Tehran umesisitiza kwamba hakuna msingi wa kisheria kwa kile kinachoitwa Kamati ya 1737, hakuna azimio lililobaki la vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Iran, na hakuna uhalali wa kufanya mikutano chini ya ajenda ya NPT.

Tehran imesema Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo liliidhinisha makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 yanayojulikana kama JCPOA, liliisha muda wake tarehe 18 Oktoba, 2025, na kukomesha athari za maazimio yaliyowekwa awali dhidi ya Iran.

Kwa msingi huo taarifa ya Ofisi ya Mwakilioshi wa Iran Un imesema: “Haya ni matumizi mabaya ya wazi ya mamlaka ya Baraza la Usalama na jaribio la makusudi la kupotosha jamiii ya kimataifa.”

Taarifa hiyo imesisitiza tena azma ya Iran ya kuendelea kuheshimu Mkataba wa Kutosambaza Silaha za Nyuklia (NPT), ikisema kwamba kwa zaidi ya miongo mitano, iIran imeendelea kuwa taifa linalowajibika na haijawahi kufanya jitihada zxa kutengeneza silaha za nyuklia.

“Tishio halisi kwa utawala wa kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia ni kutokujali kwa wale wanaoshambulia vituo vya nyuklia vya amani vilivyo chini ya uangalizi huku wakidai kuheshimu sheria za kimataifa” imesema taarifa hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *