
Shinyanga. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amewatembelea baadhi ya majeruhi wa ajali ya gari waliolazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga (Mwawaza), amesema hali zao zinaendelea vizuri tofauti na walivyopokelewa jana.
Ajali hiyo ilitokea Mei 19, 2026 saa 12 jioni na kusababisha kifo cha Boaz Martine, aliyekuwa mpiga picha wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza leo Mei 20, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Toyota Harrier anayedaiwa kupita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari, hali iliyosababisha kugongana na gari aina ya aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop lililokuwa limebeba waandishi, askari na watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
“Mtu mmoja anayejulikana kama Boaz Martine amefariki dunia katika ajali hiyo. Dereva wa Toyota Harrier anasakwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zaidi,” amesema Magomi.
Kamanda Magomi amewataja majeruhi wa ajali hiyo ni Koplo Swahiba Msangi wa Kituo cha Polisi Shinyanga, Neema Madono (36), Rehema Edson (45), Shadia Omari (32), Laurent Peter (34), Johnson James pamoja na Frank Mshana ambaye ni mwandishi wa habari wa ITV/Radio One.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, leo Mboni Mhita, amewatembelea baadhi ya majeruhi hao walifikishwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya na kulazwa katika chumba cha uangalizi wa karibu, lakini kwa sasa wamehamishiwa katika wodi za kawaida baada ya afya zao kuimarika na kuendelea kupata matibabu.
Akizungumza leo Mei 20, 2026 baada ya kuwajulia hali majeruhi wa ajali hiyo, Mhita amemuelezea marehemu Boaz Martine kama mchapakazi na hakuwa kama mpiga picha tu bali alikuwa kama mdogo wake kwani kila kazi aliyoenda aliambatana nae,
“Nimezoea sana ninapokuwa na waandishi namuona Boaz pamoja na Johnson pembeni, lakini kwa leo inakuwa ngumu kwangu hata kuzungumza, kwani alikuwa kama mdogo wangu, hakuwa tu kama mpiga picha na hii ni kwa sababu kila nilipokuwa kwenye kazi nilikuwa naye,” amesema Mhita.
Kwa upande wao baadhi ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga wamemuelezea marehemu Boaz kama mtu aliyekuwa mpole, mwenye heshima, asiyekuwa na shida na mtu yeyote pia alikuwa tayari kusaidia kwa kadri ya uwezo wake,
Mwandishi wa Jambo FM Eunice Kanumbamesema kuwa, “hakuwa na shida na mtu yeyote alikuwa mpole sana, ameenda bado mdogo sana nahisi ni kama niko ndotoni yaani siamini.”
Kwa upande wake Frola Masalu ambaye ni mwandishi wa Global TV amesema: “Kinachoniuma zaidi ni ile siku ya Ijumaa Mei 15, 2026 nilimwambia kaa hapo nikupige picha, hiyo siku tulikuwa Itwangi baada ya chakula kwenye hoteli fulani kisha tukaelekea kwenye uzinduzi wa shule.”
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga (Mwawaza), Daktari John Luzila, amesema hospitali hiyo ilipokea majeruhi saba pamoja na mwili mmoja.
Amesema kati ya majeruhi hao, wawili walikuwa katika hali mbaya na walipelekwa moja kwa moja katika Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU) kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya dharura, huku wengine wakiendelea kupatiwa huduma katika wodi za kawaida.
“Nilipokea majeruhi saba na mwili mmoja, wawili walipelekwa chumba cha dharura (ICU) mmoja hakuwa ameumia sana alipewa tu matibabu na kuruhusiwa, lakini mmoja aliyekuwa ICU amerudishwa kwenye wodi ya kawaida na mwingine ilibidi tumpeleke Bugando maana aliumia sana, kwa sasa hapa tuna majeruhi watano ambao wanaendelea na matibabu na hali zao zinaendelea vizuri,” amesema Dk Luzila.
