Pemba. Abasi Massoud Athumani (30), amefariki dunia baada ya kuzama katika bwawa la maji lililopo Skuli ya Alkhamis Camp, Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba.
Mashuhuda wa tukio hilo, Khalid Bilali na Sheha wa Shehia ya Wawi, Khamis Moh’d Khamis, wamesema Abasi alikwenda katika bwawa hilo kwa ajili ya kufua nguo na kabla ya kumaliza aliingia bwawani kuoga ndipo maji yalipomzidia na kuzama.
Tukio hilo limetokea leo Mei 20, 2026, Kikosi Cha Zimamoto na Uokozi Wilaya ya Chakechake lilipokea taarifa na kufika eneo la tukio kwa ajili ya juhudi za uokoaji.
Khalid amesema kijana huyo walikuwa wanafua pamoja na muda mfupi alidai kutaka kuoga kwenye bwawa hilo na kumwambia bora achukue ndoo asioge katika bwawa hilo lakini aliamua kufanya hivyo.
Amesema baada ya kuzama alishindwa kumsaidia kwa vile hajui kuogelea na kuchukua hatua za kuwasiliana na watu wa karibu kutoa taarifa za kijana huyo kuzama.
‘’Tulikuwa tunafua pamoja hapa lakini baada ya muda mfupi alitaka kuoga kwenye bwawa hilo, lakini nikamshauri bora uchukue ndoo akoge nje ya bwawa kwa vile hawajui kuogelea ndio muda umeshafika akajiingiza kwenye maji na kuzama,‘’ amesema Khalad.
Khamis Mohamed Khamis ambaye ni Sheha wa Shehia ya Wawi amesema amepata taarifa kutoka vijana hao na kufika kwenye tukio na kuwasiliana Ofisi za Wilaya na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kuja kusaidia kuopoa mwili wa marehemu huyo.
‘’Mimi kuna vijana walinifuata nilikuwa nipo karibu na nilipofika nikawasiliana na Ofisi za Wilaya na Kikosi Cha Zimamoto na Uokozi kuja kutusaidia kuopoa mwili wa kijana huyo,’’ amesema.
Mlezi wa kijana huyo, Mzee Said Othman amesema akiwa katika shughuli zake za kilimo alifuatwa na kijana mmoja kumwambia Abasi amezama na ndipo alipokuja kushuhudia harakati za kumuokoa bila matumaini kabla ya kutokea zimamoto kuuopoa mwili huo.
Mkuu wa Operesheni wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Mrakibu Mwandamizi Kanda ya Pemba, Mbarouk Ali Juma amesema walipata taarifa ya kuzama kwa kijana huyo majira ya saa tano asubuhi na walikwenda kutoa huduma ya uokozi, lakini walipompata alikuwa tayari ameshafariki dunia.
Akizungumza mara baada ya kukamilika uokoaji, Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Zuhura Mgeni Othman, amewataka wamiliki wa Skuli ya Alkhamis Camp kuchukua hatua za haraka kuhakikisha bwawa hilo linawekewa ulinzi na tahadhari maalumu ili kuzuia wanafunzi pamoja na vijana wengine kulifikia kiholela.
Pia, amewasisitiza wazazi na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani kuongeza uangalizi kwa watoto na vijana, akieleza kuwa bwawa hilo lina kina kirefu cha maji kinachoweza kuhatarisha maisha ya watu endapo halitasimamiwa kwa umakini na tahadhari stahiki.
