Dar es Salaam. Mratibu mkuu wa uzinduzi wa albamu mpya ya 16 ya Iwanga Pepeta, Steve Nyerere amesema mashabiki wa muziki wa dansi watarajie mambo makubwa kutoka katika bendi hiyo yatakayosindikizwa na uzinduzi vifaa vipya vya muziki.
Akizungumza na Mwananchi baada ya uzinduzi wa studio mpya ya muziki ya Twanga Pepeta Entertainment, uliofanyika Mei 17, Steve Nyerere anasema bendi hiyo baada ya miaka mingi ya kuendelea kutamba kwenye muziki wa dansi nchini, imejipanga kuandika historia mpya.
Baada ya uzinduzi huo, Steve Nyerere, Asha Baraka pamoja na viongozi wa bendi hiyo wameahidi maandalizi ya aina yake na kuifanya shoo hiyo, itakayofanyika Agosti 7 kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, kurejesha hadhi ya muziki wa dansi kwa kutoa burudani ya kiwango cha juu kwa mashabiki.
Steve Nyerere Afunguka
Katika kuhakikisha inazikonga mioyo ya mashabiki, anasema bendi hiyo imeanza maandalizi rasmi ya uzinduzi huo ambao pia unatarajiwa kusindikizwa na burudani mbalimbali tofauti.
Lengo la kufanya maandalizi mapema ni kuwawezesha kufanya onyesho la kihistoria na kuwa bendi ya kwanza nchini kufanya onyesho kwenye ukumbi wenye hadhi kubwa kama wa Mlimani City.
Steve Nyerere anasema kuanza kwa maandalizi ya onyesho hilo ni dalili kubwa tukio hilo litakuwa la kihistoria nchini na mpango wa kuwaweka kambini wanamuziki wa bendi hiyo una lengo la kuongeza umoja, nidhamu ya kazi pamoja na kuandaa mfumo mzuri wa burudani utakaotolewa siku ya uzinduzi.
Anasema kambi haitakuwa na mwingiliano wa masuala mengine ya kila siku na kuwezesha wanamuziki kufikiria zaidi shoo hiyo inayotarajia kuwa ya aina yake.
Anaongeza hatua hiyo ni sehemu ya mandalizi makubwa ambayo hayajawahi kufanywa kwa muda mrefu katika muziki wa dansi nchini, huku wadau wakiamini inaweza kuleta ushindani mpya katika tasnia hiyo.
“Ule sio uzinduzi wa kawaida kabisa, sisi tunakwenda kuweka historia mpya kutokana na bendi ya Twanga Pepeta. Tunataka mashabiki wakifika Mlimani City waone kitu tofauti kabisa na walichowahi kuona kwenye muziki wa dansi,” anasema na kuongeza;
“Tunataka wanamuziki wa bendi hii wafanye ‘rehearsals’ za kutosha, wajipange vizuri na kuhakikisha kila kitu kinakuwa katika ubora mkubwa kabla ya Agosti 7.”
Vyombo Vipya Kuanikwa, Wahi Tiketi
Mbali na uzinduzi wa albam mpya, Steve Nyerere anasema pia kutakuwa na uzinduzi wa vyombo vipya vya bendi hiyo na matukio mengine mbalimbali yatakayowapa burudani mashabiki watakaofika Mlimani City.
Aidha aliweka wazi safari hii hakutakuwa na tiketi za bure ‘complimentary’ kwa watu watakaohudhuria tamasha hilo, huku akisisitiza kila mtu atalazimika kununua yake. “Safari hii hakuna complimentary.
Tunataka watu waone thamani ya muziki wa dansi na mchango wa wasanii. Kila mtu atanunua tiketi yake kwa sababu tunataka kufanya kitu kikubwa na cha tofauti,” alisema.
Asha Baraka Atoa Msimamo
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bendi hiyo Asha Baraka anasema wamejipanga kuhakikisha uzinduzi huo unakuwa wa mafanikio makubwa na kuleta sura mpya katika muziki wa dansi.
Anasema wameunda kamati maalum ya wadau wa muziki ambayo itafanya kazi kwa karibu na Steve Nyerere kuhakikisha maandalizi yote yanakamilika kwa wakati.
“Tumeamua kushirikiana na wadau mbalimbali kwa sababu tunataka kufanya jambo kubwa ambalo litabaki kwenye historia ya muziki wa dansi Tanzania. Mashabiki wa Twanga Pepeta wakae tayari kuona mambo makubwa,” anasema Baraka.
Uzinduzi huo wa albam mpya ya Twanga Pepeta unatarajiwa kuvuta mashabiki wengi wa muziki wa dansi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kutokana na ukubwa wa bendi hiyo na historia yake katika muziki wa Tanzania.
Chalz Baba azungumzia Album
Kwa upande wake, Kiongozi wa bendi hiyo, Chalz Baba anasema wanamuziki wa Twanga Pepeta wamepokea kwa furaha maandalizi hayo na tayari morali ya kazi imeongezeka.
Anasema uzinduzi huo ni nafasi muhimu ya kuonyesha muziki wa dansi bado una nguvu kubwa na unaweza kuendelea kufanya vizuri mbele ya mashabiki wa kizazi cha sasa.
“Kuna watu wengi wamekuwa wakisema muziki wa dansi umeshuka, lakini sisi tunaamini bado una nafasi kubwa sana.
Kupitia uzinduzi huu tunataka kuonyesha dansi bado inaweza kufanya makubwa na kuwapa mashabiki burudani nzuri,” anasema Chalz Baba na kuongeza albam mpya ya Twanga Pepeta imebeba nyimbo mbalimbali zenye ladha tofauti kwa ajili ya mashabiki wa rika zote.
“Tumefanya kazi kubwa sana studio kuhakikisha mashabiki wanapata nyimbo nzuri zenye ujumbe na burudani. Tunataka kila shabiki wa Twanga Pepeta ajione sehemu ya mafanikio haya,” anasema.
Luizer Mbutu Kuhusu Studio
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Luizer Mbutu anasema sambamba na uzinduzi wa albam hiyo, Iwanga Pepeta pia imezindua studio mpya ambayo itatumika kurekodi kazi mbalimbali za muziki.
Studio hiyo inajulikana kwa jina la Twanga Pepeta Entertainment, ina vifaa vya kisasa kwa ajili ya kurekodi kazi za wasanii mbalimbali.
“Hii ni studio ya kisasa zaidi hapa nchini, ina kila kifaa ambacho kinatumika kurekodi kazi za wanamuziki, hii ni fursa kwa wanamuziki kuja kufanya kazi na studio hii,” anasema Luizer.
Anasema studio hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa kuifanya Twanga Pepeta iendelee kuwa taasisi kubwa ya muziki wa dansi nchini.
“Tumekuwa tukifanya kazi kubwa kuhakikisha Twanga Pepeta inakwenda na wakati. Studio hii mpya itatusaidia kuongeza ubora wa kazi zetu, pia kutoa nafasi kwa wasanii wengine kufanya kazi zao katika mazingira mazuri,” anasema Luiza.
