Ajenda muhimu za kitaifa zinavyofichwa nyuma ya kivuli cha uchaguziAjenda muhimu za kitaifa zinavyofichwa nyuma ya kivuli cha uchaguzi

Matamanio ya kupata Katiba mpya, Tume huru ya uchaguzi na kujenga maridhiano ya kitaifa, ni nguvu muhimu ambazo zimekuwa zikizungumzwa mwaka hadi mwaka kwa lengo la kulikwamua taifa katika mkwamo wa kisiasa.

Hata hivyo, jitihada hizo za wadau zimekuwa zikikwama chini ya kivuli cha uchaguzi mkuu kila msimu unapofika, hivyo kufanya mzunguko wa kujadili masuala hayo kabla ya kuyazika unapofika wakati wa uchaguzi.

Hiyo ni kutokana na dhana iliyozoeleka nchini ya kufungamanisha mchakato wa mambo haya na kalenda ya uchaguzi, hali ambayo kila awamu mjadala huo unaishia kupisha uchaguzi na kuibuka tena baada ya uchaguzi kwisha.

Ajenda hizi zimekuwa zikiishi chini ya kivuli cha uchaguzi mkuu tangu mjadala wa kukusanya maoni ya wananchi ulioongozwa na Jaji mstaafu, Joseph Warioba, mwaka 2013.

Mchakato huo uliokwama mwaka 2014 kupisha uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ulizika ndoto ya kuhitimisha jambo hilo kwa sababu ya uchaguzi.

 Ajenda hizo zilizofifia baada ya uongozi wa awamu ya tano mwaka 2015/2020 kutoonyesha kipaumbele kwa ukamilishaji wake, zilirudi tena katika awamu ya sita.

Katika awamu hii, Rais Samia Suluhu alionyesha nia kwa vitendo na kuanzisha mchakato wa maridhiano baina ya makundi ya wadau, yakihusisha vyama vya siasa vya Chadema na CCM, hatua iliyoibua matumaini ya kufikiwa mwafaka wa mambo hayo kwa Taifa. Hata hivyom juhudi hizo ziliishia njiani.

Itakumbukwa kwamba katika bajeti ya mwaka 2024/25, Serikali ilitenga Sh9 bilioni kwa ajili ya kuelimisha wananchi kuhusu Katiba, ikiwa ni hatua ya awali ya kuanza mchakato wa kuandika Katiba mpya.

Hata hivyo, kutokana na chaguzi zilizofuata mbele, mchakato huo ulifunikwa na akili zote kuelekezwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025 ambao ulisusiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilichotaka uchaguzi huo uahirishwe ili kuandika Katiba mpya.

Wachambuzi wa siasa wanasema katika historia ya Tanzania, uchaguzi huo ulithibitisha madhara ya kuendelea kupuuzwa kwa ajenda hizi baada ya machafuko yaliyotokana na ghasia za uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 29, 2025.

Ikiwa imepita miezi sita tangu kumalizika kwa uchaguzi huo, kilio cha Katiba mpya, Tume huru na maridhiano ya kitaifa vimeendelea kubeba mijadala ya wadau huku zikielekea zikikabiliwa na kivuli cha uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2029 na uchaguzi mkuu wa 2030.

Uwajibikaji na utashi

Mwanazuoni mkongwe, Prodesa Issa Shivji anasisitiza juu ya uwajibikaji katika ajenda za kitaifa kwani ndiyo kiungo cha amani na haki, akionya kuwa amani bila haki ni ya muda mfupi na huzaa migogoro ya baadaye.

Ametoa mifano ya historia ya Tanzania inayoonyesha kuwa pale uwajibikaji ulipozingatiwa, imani ya wananchi iliongezeka.

Kwa mtazamo wake, changamoto ya sasa si kukosekana kwa hoja, bali ni utekelezaji wake unaosubiri mazingira ya kisiasa.

Mhadhiri mwandamizi mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Azaveli Lwaitama anasema maridhiano hayawezi kusubiri kalenda ya uchaguzi, akihoji kama ni sahihi kwa Taifa kusubiri hadi mwaka 2030 kupata Katiba mpya.

“Maridhiano hayawezi kujengwa bila ukweli wa matukio ya kisiasa, bila mchakato wa wazi na huru, taifa linaweza kuingia kwenye mkanganyiko unaojirudia kila uchaguzi unapofika,” anasema Dk Lwaitama.

Nafasi ya vyama

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman anasema msimamo wa kisiasa wa vyama huathiri mazingira ya uamuzi wa wakati husika.

Anasema vyama vya siasa hubeba ajenda na kupitia wafuasi wake huchora ramani ya utekelezaji au kukwamisha utekelezaji wa ajenda husika akisisitiza utashi wa kisiasa katika kufikia mwafaka wa kitaifa katika mambo yanayoibua mjadala mpana.

Kwa upande wake, mbunge wa zamani, Saed Kubenea anahoji kuhusu msimamo wa vyama kushiriki au kususia mifumo ya kisiasa, akionya kuwa mzunguko wa migogoro ya kisiasa hauwezi kuisha bila majibu ya moja kwa moja ya viongozi.

Mbali na hao, Kiongozi Mstaafu wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe analia na namna vyombo vya ulinzi na usalama vinavyoshiriki katika masuala ya vyama vya siasa, akiona kuwa ni tatizo katika kufikiwa mwafaka wa pamoja katika ajenda za kitaifa.

“Bila uwajibikaji wa vyombo vya usalama na kutenganishwa kwao na siasa, Tanzania itaendelea kubaki kwenye mkwamo wa kisiasa unaojirudia,” anasema.

Kada wa Chama cha Mapinduzi Ezekiel Wenje anasema ili kufikia utekelezaji wa ajenda za kitaifa, mazungumzo ndiyo njia itakayowezesha mchakato huo.

“Hakuna njia ya kutoka kwenye mkwamo wa kisiasa bila mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande zinazokinzana,” anasema Wenje.

Hatua zichukuliwe

Mhadhiri kutoka Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Denis Konga anasema yaliyotokea Oktoba 29, 2025 yametukumbusha kwamba kupuuzia ajenda hizi tatu muhimu ni hatari kwa Taifa, akisisitiza kuwa yanapaswa kushughulikiwa bila kutazama kalenda za kisiasa ikiwemo ratiba ya uchaguzi au awamu ya kiongozi kukaa madarakani.

“Ni wazi kuwa ajenda hizi zimekuwa zikihusishwa sana na kalenda za uchaguzi mkuu na ule wa mitaa, na hivyo utekelezaji wake umekwama mara kwa mara. Lakini sasa tunahitaji kuchukua hatua bila kungoja ratiba za uchaguzi ili kuepuka sintofahamu kama zilizoshatokea,” anasema.

Konga anasisitiza kuwa bila kukamilishwa ajenda hizo, Taifa hakitaweza kuwa na misingi imara ya mamlaka na uhuru halisi wa vyombo vya dola na mamlaka za nchi.

Anatoa mfano kwamba viongozi wengi barani Afrika wamekuwa wazito kuchukua hatua za kushughulikia madai ya jamii katika kuweka mifumo huru ya taasisi kwa sababu wengi wao wanatawala kwa maslahi yao binafsi na makundi yao, hali ambayo imeishia kuvuruga amani kwa mataifa yao.

“Ili kunusuru Taifa letu, ni muhimu kuharakisha mchakato wa Katiba mpya, ambayo itawezesha kupatikana Tume huru na hayo mengine yote na mchakato unapaswa kuanza sasa bila kusubiri,” anasema.

Anaongeza kuwa: “Tunapaswa kutumia majukwaa ya wazi na yanayokubalika na wananchi walio wengi, na kuzingatia rasimu ambayo inatokana na maoni ya Watanzania wenyewe badala ya ile iliyoandaliwa na Bunge maalumu ambayo inalalamikiwa na wengi kuwa ilipuuza maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Rasimu ya Warioba,” anaongeza.

Wanasiasa kutoaminiana

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Kenani Kihongosi, katika katika moja ya mikutano yake na wanahabari, alieleza kuwa Katiba mpya ni sehemu ya ilani ya 2025–2030, lakini utekelezaji wake unategemea mchakato wa maridhiano na ushirikishwaji wa wananchi.

Kauli hiyo inaendana na ahadi ya chama hicho katika ilani yake na msimamo wa Rais Samia ambaye amekuwa akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha Taifa linapata Katiba mpya ifikapo 2030 huku akisisitiza umuhimu wa maridhiano kabla ya kufika huko.

Chadema ambacho kimeendelea kupigia kelele ajenda hizo kwa tahadhari na masharti, nacho msisitizo wake umekuwa ukijielekeza kwenye mazingira yanayokwamishwa na kisingizio cha uchaguzi zinazotolewa na Serikali.

Kauli za viongozi wake, wanasisitiza utekelezaji wa ajenda hizi ukamilike kabla ya uchaguzi huo, hali inayoendeleza ajenda hizi kuchochewa na kukwamishwa na kalenda za uchaguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *