
Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema licha ya majengo mazuri ya hospitali yaliyojengwa, huduma zinazotolewa haziridhishi.
Hata hivyo, wameitaka Serikali kupitia upya sera yake ya utoaji wa huduma kwa kushirikiana na sekta binafsi kwenye hospitali za umma.
Wakizungumza katika michango yao wakati wa kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo barazani leo Mei 20, 2026, wamesema mfumo huo unahatarisha ajira za wazawa kwa kuwa, wataalamu wa ndani wanalipwa mshahara kidogo ikilinganishwa na wanaoletwa na kampuni zilizopewa fursa hiyo.
Baadhi ya wawakilishi wamesema kampuni zilizopewa fursa hiyo zinatoa huduma kwa kujisikia.
Mwakilishi wa Chambani, Mahmoud Shineni Ali amesema kuna kuzorota kwa huduma licha ya miundombinu kuboreshwa kwa kiasi kikubwa.
“Licha ya kubinafsisha utoaji wa huduma katika hospitali hizi, lakini kasi ya utoaji huduma inakuwa ndogo, mgonjwa anaweza kukaa zaidi ya saa nne bila kupata huduma,” amesema.
Moza Mohamed Khamis, mwakilishi wa wanawake akitolea mfano wa baadhi ya nchi zinazotumia sera hiyo kama Ghana, amesema Serikali ndio inasimamia huduma zote na ukaguzi wa dawa na kuwauliza wagonjwa na iwapo mgonjwa akikutwa na tatizo analipwa hivyo kampuni inayopewa inakuwa makini.
“Serikali iamue, ikifanya ukaguzi au uchunguzi wake yenyewe itabaini kasoro nyingi kwenye hizi hospitali na madakatari wengi wanaondoka kwasababu hawaheshimiwi,” amesema.
Amesema hakuna uwazi katika utaratibu huo kwamba, amepewa mtu fulani na akifanya manyanga aondoshwe.
Amesema hata mishahara ni tofauti, wakati wataalamu wazawa wakilipwa mshahara kwa Sh1.7 milioni kwa mwezi, lakini wataalamu wanaoajiriwa na kampuni hizo wanalipwa Sh7 milioni, hivyo inawakatisha moyo wataalamu wa ndani.
“Kuna daktari hata kuandika ripoti hajui, lakini ndio hao unakuta wanalipwa mishahara mikubwa na wataalamu wetu wa ndani kunyanyaswa,” amesema.
Pia, amezungumzia kuhusu bima akisema inakatwa mishahara lakini mtu akienda hospitali wanazungushwasho kwani haipo sawa kwa wananchi.
Mwakilishi wa Ole, Seif Hamad Suleiman (ACT- Wazalendo) amesema Serikali imeingia kwenye mtindo huo wa ‘Outsourcing’ na pengine dhamira ilikuwa mzuri na bora, lakini akasema kuna matatizo mengi yanayokosa majawabu.
“Hawa waliokabidhiwa hizi hospitali za wilaya badala ya kutoa huduma imekwenda kuwa kero, hakika kuna matatizo mengi kwenye ‘Outsourcing’, lazima tuwe na mkakati wa kuwalinda wataalamu wetu wa ndani vingevyo watakuwa wanakimbia, kila siku,” amesema Seif.
Amesema wamepewa mamlaka ya kuajiri na kinachoshangaza masilahi ya wataalamu wazawa ni kidogo karibu mara saba ya wageni.
Mwakilishi wa Chumbuni, Makame Mohamed Sufiani (CCM) amesema hospitali nzuri lakini madaktari ni wajeuri, kwa hiyo hata huduma hazifikiwi waliomo wanatumia jeuri.
“Hospitali nzuri lakini wanaotoa huduma sio wazuri wanazungusha watu na hawana kauli nzuri kwa wagonjwa,” amesema.
Dk Nasra Nassor Omar, nafasi za wanawake (ACT- Wazalendo) amesema kampuni hizo zinakuja na madaktari wao lakini hata wale wataalamu wa ndani wanaopata nafasi hizo, wanapewa mshahara ambao haustahili kulipwa.
“Hii haileti manufaa kwa Serikali unamsomesha mtu kisha analipwa kidogo anaondoka, kwahiyo tunawatumia vibaya hususani kwa hawa waliokuwa outsource na Serikali,” amesema Dk Nassra
Pia, Dk Nassra amesema wizara inadaiwa madeni mengi, akitaka kujua mpango uliopo wa kulipa madeni hayo ambayo wakati mwingine yanadaiwa na taasisi za Serikali, hivyo kuzifanya zishindwe kufanya kazi kwa ufanisi kutokna na madeni hayo.
Kwa mujibu wa mwakilishi huyo, wizara inadaiwa Sh20 bilioni na Bohari Dawa na Sh1.8 bilioni inadaiwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Kwa hiyo inahitaji mambo mengi ila kumekuwapo na madeni ambayo hayalipwi na tunaambiwa Bohari ya Dawa inahitaji kujitegemea lakini kwa malimbikizo haya haiwezi kujitegemea,” amesema.
Mwakilishi wa Ziwani Mohamed Ali Salim (ACT) amesema wanajenga majengo lakini hawawajali wanaowajengea majengo hayo kwani wagonjwa wanapofika kwenye hospitali hizo hawapewi thamani kama inavyotakiwa.
Zainabu Khamis Shomari nafasi za wanawake (CCM) amesema ipo haja ya kuangalia masilahi ya madaktari kwani ni madogo ikilinganishwa na kazi wanayoifanya.
“Tuangalie masilahi ya madaktari, unakuta daktari hata gari hana anapanda daladala, hii haiwezekani katika nchi ambayo tunakwenda na ulimwengu wa kisasa na tumejenga majengo yetu mazuri,” amesema Shomari.
Hata hivyo, amesema nia ya Serikali ya kujenga majengo mazuri isifananishwe na utoaji wa huduma mbovu kwa kile alichoeleza kuwa hilo ni suala la utendaji.
