Je wajua kwa nini ugonjwa unaitwa EbolaJe wajua kwa nini ugonjwa unaitwa Ebola

Dalili za Ebola

Afisa huyo Dkt Marie Roseline Belizaire ambaye ni Mkurugenzi wa masuala ya dharura WHO Kanda ya Afrika amesema dalili za Ebola huanza ghafla zikiwemo homa kali, uchovu mkubwa, maumivu ya misuli, kichwa na koo. Ugonjwa huo unaweza kuendelea na kusababisha kutapika, kuhara, maumivu ya tumbo na hata kutokwa damu katika hatua kali. Hata hivyo, WHO inaeleza kuwa utambuzi wa mapema na matibabu ya haraka vinaweza kusaidia kuokoa maisha.

Chanjo ya Bundibugyo bado haijapatikana

WHO imethibitisha kuwa mlipuko wa sasa unasababishwa na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo. Dkt. Vasee Moorthy, Afisa wa WHO anayehusika na tafiti na maendeleo amesema kwa sasa hakuna chanjo iliyoidhinishwa kwa aina hiyo, ingawa chanjo ya majaribio ipo lakini bado haijapatikana kwa matumizi ya haraka.

WHO: Bado si janga la dharura la kimataifa

Kamati ya WHO inayohusika na dharura za afya imesema hali ya sasa bado haijafikia kiwango cha kutangazwa kuwa janga la kimataifa. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Lucille Bloomberg, amesema hatua za haraka zinahitajika ili kulinda wananchi na wahudumu wa afya katika maeneo yaliyoathirika.

WHO yajibu madai ya kuchelewa kuripoti

Afisa wa WHO, Dkt. Anais Legand, amesema shirika hilo lilichukua hatua mara moja baada ya kupata taarifa kutoka mamlaka za afya nchini Congo. “Ningependa kuwakumbusha wote kwamba ufuatiliaji huanzia ndani ya jamii na huanza na mamlaka za afya katika kila nchi. Mara tu WHO ilipopata taarifa ya dalili hiyo, msaada ulitolewa kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kufanya uchunguzi haraka iwezekanavyo. Na hatimaye hili lilithibitishwa mwishoni mwa wiki iliyopita. Uchunguzi bado unaendelea ili kubaini ni lini na wapi hasa mlipuko huu ulianza. Kwa kuzingatia ukubwa wake, tunadhani kwamba huenda ulianza miezi kadhaa iliyopita.”

Uganda yapongezwa kwa hatua za kinga

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus ameipongeza serikali ya Uganda kwa kuahirisha maadhimisho ya Siku ya Mashahidi yaliyotarajiwa kuhudhuriwa na mamilioni ya watu, hatua iliyolenga kudhibiti maambukizi ya Ebola nchini humo. Tayari taifa hilo la Afrika Mashariki pia limetangaza mkakati wa kitaifa wa kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *