MONUSCO yasafirisha tani 30 za vifaa vya Ebola Bunia DRCMONUSCO yasafirisha tani 30 za vifaa vya Ebola Bunia DRC

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MONUSCO, umeongeza juhudi za kukabiliana na mlipuko wa Ebola katika jimbo la Ituri kwa kusafirisha karibu tani 30 za vifaa vya dharura kwenda mji wa Bunia ndani ya siku nne.

Katika taarifa yake, MONUSCO imesema kuwa Mei 17, tani tano za vifaa vya matibabu ziliwasili Bunia kutoka Nairobi nchini Kenya kupitia ndege iliyokodiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO. Vifaa hivyo vilijumuisha mavazi ya kujikinga (PPE), dawa, vifaa vya maabara na mahema ya kuwahudumia wagonjwa wa Ebola.

Aidha, magari manne na pikipiki mbili zilisafirishwa kutoka Goma nchini DRC na Entebbe nchini Uganda ili kusaidia shughuli za usafirishaji na huduma za dharura katika maeneo yaliyoathirika.

Mnamo Mei 20, tani nyingine 11 za vifaa vya kukabiliana na Ebola ziliwasili Bunia kupitia safari za ndege za MONUSCO kutoka Kinshasa na Nairobi.

MONUSCO pia imeendesha kampeni za uelimishaji kwa wananchi katika maeneo ya Tchabi na Fataki mkoani Ituri kuhusu hatua za kujikinga dhidi ya Ebola. Kupitia vipaza sauti, vikosi vya walinda amani vimehamasisha wananchi kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kula nyama za porini, kuepuka mikusanyiko na kutoa taarifa mapema kwa visa vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi hadi Mei 18, jumla ya visa 457 vya washukiwa wa Ebola vilikuwa vimeripotiwa Ituri huku watu 131 wakifariki tangu mlipuko huo kuanza, wakiwemo watu 33 waliofariki karibuni.

Maafisa wa afya wameonya kuwa hadi sasa hakuna tiba maalumu wala chanjo ya aina mpya ya Ebola iliyogunduliwa, hivyo jamii zinatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga ili kuzuia maambukizi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *