
Dar es Salaam. Mshtakiwa Un Hyok Ra (37) ambaye ni raia wa Korea Kaskazini anayekabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kumiliki vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh6.4 bilioni, ataendelea kusalia rumande hadi Juni 9, 2026 kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Hatua hiyo inatokana na upande wa Jamhuri kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa bado wanaendelea na uchunguzi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Florida Wencelaus ameieleza Mahakama hiyo leo Mei 21, 2026 wakati kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha.
“Mheshimiwa hakimu, mshtakiwa leo hajaletwa Mahakamani na kesi hii imeitwa kwa ajili ya kutajwa na bado shauri hili lipo katika hatua za kiupelelezi, hivyo tunaomba Mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amesema Wancelaus.
Hakimu Mshasha alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hadi Juni 9, 2026 kwa kutajwa na ambapo pia itatolewa hati ya wito wa kumuita mahakamani mshtakiwa huyo kutoka rumande.
Kwa mara ya kwanza mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo, Mei 8, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 10054 ya mwaka 2026
Katika kesi ya msingi, Ra ambaye ni mkazi wa Mikocheni, anadaiwa Aprili 19, 2026 katika eneo la Hoteli ya Golden Tulip–Masaki, Wilaya ya Kinondoni, alikutwa akimiliki nyara za Serikali ambazo ni vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh6.4 bilioni, mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa wanyamapori nchini.
Shtaka la pili, siku na eneo hilo, mshtakiwa alijihusisha na biashara ya nyara za Serikali kwa kuuza vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh6.476 bilioni mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa wanyamapori.
