Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva kufanyika Mlimani CityTamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva kufanyika Mlimani City

Dar es Salaam. Wasanii wa muziki wa Bongo Fleva nchini wameandaa tamasha maalumu la kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa muziki huo nchini.

Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Julai 10, 2026 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, likiwakutanisha pamoja wasanii wakongwe waliotikisa katika miaka ya mwanzo ya Bongo Fleva.

Lengo la tamasha hilo ni kuwakumbusha mashabiki historia ya muziki huo pamoja na mchango wa wasanii walioweka msingi wa Bongo Fleva inayofurahiwa na kizazi cha sasa.

Akizungumza leo Mei 21, 2026 wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo uliofanyika katika ukumbi wa Hayat Hotel jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Muziki Tanzania ambaye ni msanii wa Bongo Fleva, Fid Q, amesema moja ya changamoto zinazoukabili muziki wa Tanzania kushinda tuzo kubwa za kimataifa kama Grammy ni kukosekana kwa utambulisho wa kipekee wa muziki huo.

“Bongo Fleva ya zamani ilikuwa na utambulisho wa kipekee uliobeba lugha, tamaduni na simulizi za maisha ya Mtanzania. Muziki huo ulizungumza maisha halisi ya mtaani, ndoto, changamoto, mapenzi na matumaini ya jamii,” amesema Fid Q.

Hata hivyo, amesema baadhi ya wasanii wa kizazi cha sasa wamejikita zaidi katika kuiga mitindo ya kimataifa kama Amapiano na Afrobeat badala ya kujenga sauti yao ya kipekee.

“Hatupo hapa kuwaponda wanaofanya Amapiano, lakini ni lazima tujiulize kama muziki wa sasa bado unawakilisha sauti halisi ya Tanzania,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mratibu wa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva, Madee Ali, amewataka wasanii wa zamani kuacha kuitwa wakongwe akieleza kuwa wao ni msingi na historia ya muziki wa Bongo Fleva nchini.

Aidha, tamasha hilo linatarajiwa kutoa fursa kwa wasanii wa kizazi kipya kuungana na waanzilishi wa muziki huo kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu za ubunifu zilizosaidia Bongo Fleva kushika nafasi kubwa katika anga la muziki nchini na Afrika kwa ujumla.

Kwa upande wake msanii Chid Benzi amesema amefurahishwa na umoja huo ambao kwake anaona kama moja njia ya kuwaweka pamoja wao kama wasanii wa aina mbalimbali.

Ameendelea kwa kusema hio miaka ya 30 Bongo Flava inawahusu zaidi wasanii wakongwe lakini hata wa kizazi kipya watakuwepo kama sehemu ya wao waweze kujifunza kutoka kwa wakubwa wao kimziki

Mastaa ambao wamejitokeza katika uzinduzi huo ni pamoja na Afande Sele, Mr Blue, Chid Benz, Dully Sykes, Fid q, Madee Ali, Feruzi, Loud Eyz na wengineo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *