BALAA linaloonyeshwa na winga wa Simba raia wa Senegal, Libasse Gueye, limewaibua Waarabu wa MC Alger wanaodaiwa tayari wameanza kumfuatilia nyota huyo, licha ya uongozi wa kikosi hicho kuonyesha matumaini makubwa ya ujenzi wa timu hiyo.
Nyota huyo aliyejiunga na Simba Januari 17, 2026, akitokea Teungueth FC ya kwao Senegal, amekuwa mhimili mkubwa wa timu hiyo kwenye kikosi cha Kocha, Steve Barker kinachopigania ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilioukosa kwa misimu minne mfululizo.
Taarifa kutoka Algeria, zinaeleza mabosi wa MC Alger wanafuatilia mwenendo wa nyota huyo kwa ajili ya kuipata saini yake msimu ujao, licha ya ugumu itakaokutana nao, kutokana na umuhimu wake katika kikosi hicho cha Msimbazi.
Vyanzo mbalimbali kutoka Algeria vinaeleza Gueye ni miongoni mwa wachezaji wanaoangaliwa ili kuongezea nguvu timu hiyo, ambayo ndio mabingwa wa Ligi Kuu ya Algeria msimu wa 2025-2026, baada ya kufikisha pointi 62, ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani.
Katika mechi 29 ilizocheza MC Alger za Ligi Kuu ya Algeria hadi sasa, imeshinda 19, sare tano sawa na ilizopoteza, ikifunga mabao 39 na kuruhusu 18, ikiwa kileleni mwa msimamo na pointi 62, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.
Licha ya MC Alger kuonyesha nia ya kumhitaji, Simba inaamini nyota huyo ni hazina ya kuiwezesha kutetea mataji yake iliyokosa kwa misimu minne mfululizo, ikiwemo ya Ligi Kuu na CRDB, ambayo mara ya mwisho kuchukua ni msimu wa 2020-2021.
Gueye anayecheza nafasi winga na wakati mwingine kiungo mshambuliaji akitokea kati, alisajiliwa na Simba kutokana na kiwango bora alichokionyesha katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024, akiwa na Senegal.
Nyota huyo alisajiliwa Simba ili kuziba nafasi iliyoachwa na Jean Charles Ahoua ambaye alienda CR Belouizdad ya Algeria, baada ya kuonyesha kiwango kizuri na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025 alipofunga mabao 16.
Gueye aliyecheza pia Demba Diop FC (U-20), Diambars de Saly FC zote za kwao Senegal kisha Pontevedra CF na Valencia (U-19) za Hispania, tangu ajiunge na Simba akitokea Teungueth FC, amefunga mabao matano ya Ligi Kuu Bara na kuasisti moja.
Mchezaji huyo aliyezaliwa Julai 5, 2003, baada ya msimu wa 2025-2026, kuisha atabakisha mkataba wa miaka miwili na Simba utakaofikia tamati rasmi Juni 30, 2028, jambo litakaloisababishia MC Alger kutenga kitita kikubwa cha fedha ili kumpata.
