
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) limeripoti visa zaidi ya 125,000 vya maambukizi yanayohusiana na panya na vimelea katika Ukanda wa Gaza ulioathiriwa na vita katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu.
“Mgogoro mwingine katika Ukanda wa Gaza. Panya na vimelea vinaongezeka. Maambukizi ya ngozi yanasambaa. Hatari ya magonjwa inaongezeka,” ilisema taarifa ya UNRWA katika mtandao wa kijamii wa X jana Alkhamisi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina limeongeza kuwa mamia ya wafanyakazi wa huduma za matibabu wa UNRWA wanatibu takriban visa 400 kwa siku, lakini wanaweza kutibu zaidi ikiwa watapata vifaa vya kutosha vya dawa. Shirika hilo limesisitiza kwamba vifaa vya matibabu lazima viruhusiwe kuingia Gaza kwa kiwango kikubwa.
Matokeo hayo ya kusikitisha yanakuja huku kukiwa na ukiukwaji wa kila siku wa makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel tangu Oktoba 10, 2025.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, ukiukaji huo umewaua Wapalestina 887 na kujeruhi wengine 2,602 hadi sasa.
Usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza ulifuatia miaka miwili ya mauaji ya kimbari ya Israel yaliyoanza Oktoba 2023, na baada ya kuuawa shahidi zaidi ya Wapalestina 72,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Raia wengine zaidi ya 172,000 wa Kipalestina wamejeruhiwa na takriban asilimia 90 ya miundombinu ya Gaza imeharibiwa kikamilifu.
