
Wadau wa sekta ya usafirishaji nchini Kenya, wametangaza kumaliza mgomo waliopanga kuufanya tena wiki ijayo baada ya majadilino na Rais William Ruto.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kupitia hotuba kwa taifa, Rais Ruto, amesema tatizo la mafuta ni la dunia nzima, na kwamba serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kupunguza makali ya gharama za maisha.
Kuhusu maazimio waliyoafikia na wadau wa sekta hiyo, Rais Ruto amesema Serikali yake itapunguza shilingi 10 zaidi kwenye bidhaa ya mafuta ya dizeli kuanzia mwezi Juni na Julai.
Aidha ameiagiza wizara ya usafirishaji kukaa na wadau wa sekta ya usafirishaji kutatua changamoto za kikodi pamoja na kuzungumza na taasisi za kifedha kuona namna zinaweza kutoa ahueni Katia riba za mikopo iliyochukuliwa na wafanyabiashara wa sekta hiyo.
Katika hatua nyingine Rais Ruto ameruhusu wamiliki wa matatu kutoondoa michoro maarufu kama Graffiti akisisitiza iwe imezingatia maadili na usalama.
Rais Ruto amekiri kuwa hali ya uchumi wa wananchi imeendelea kuwa ngumu, lakini akawatoa hofu akisema serikali itaendelea kujadiliana na wadau muhimu kuhakikisha mwananchi anapunguziwa mzigo.
Ruto pia aliwataka wanasiasa kuacha kupotosha uma kuhusu suala la upatikanaji wa mafuta nchini, akisema baadhi wametumia shida hii kuwahadaa wananchi kufanya vurugu, akionya dhidi ya wale wanaotaka kuleta mgawanyiko kwenye taifa.
Kwa upande wao, muungano wa wamili wa matatu kupitia mwenyekiti wake Albert Karakacha, wametangaza kufuta kabisa mgomo wao, wakisema wataendelea kushirikiana na Serikali kutatua changamoto zao pamoja na zile za wananchi wa kawaida.
Albert amesema wanasiasa hawapaswi kutumia madai yao kisiasa akisema muda wa kufanya siasa haujafika.
Hata hivyo kauli yao imechukuliwa kwa hisia mseto na raia wa Kenya ambao wanahoji ni kwanini wamebadili sehemu ya takwa kuu la madai yao ya wali kushinikiza serikali kupunguza bei ya mafuta, baadhi wakituhumiwa kupkea rushwa na shinikizo.
