Arusha. Tanzania inatarajia kukuza zaidi uchumi wake baada ya kugundulika kwa utajiri wa madini maarufu kama Rare Earth Elements (REEs) katika kijiji cha Mkiu, Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Madini hayo ya aina ya Neodymium (Nd) na Praseodymium (Pr), yana mahitaji makubwa duniani kutokana na matumizi yake katika utengenezaji wa magari ya umeme, mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo, simu za kisasa, vifaa vya kielektroniki pamoja na teknolojia nyingine zinazotegemea nishati ya kijani.
Akizungumzia ugunduzi huo Mei 20, 2026 na waandishi wa habari, Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Lucas Mlekwa amesema madini hayo yamegundulika katika mwendelezo wa tafiti mbalimbali za madini zinazoendelea mkoani humo.
Amesema utafiti huo unaofanywa kwa ushirikiano kati ya Serikali na kampuni ya Hongji Mining Co. Ltd unaendelea kubaini kiwango cha madini yaliyopo ardhini kabla ya kuanza uwekezaji mkubwa wa uzalishaji.
Amesema, pia, ugunduzi huo unaipa Tanzania nafasi ya kuwa miongoni mwa nchi muhimu katika mapinduzi ya teknolojia duniani kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya vifaa vinavyotumia nishati safi.
Mlekwa amesema kampuni ya Hongji Mining tayari imekamilisha awamu ya kwanza ya utafiti na sasa ipo katika hatua ya pili ya uchunguzi wa kina kabla ya uzalishaji rasmi kuanza, katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 280.
Amesema zaidi ya Sh1 bilioni moja tayari zimelipwa kama fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo huku tathmini ya athari kwa mazingira ikiwa katika hatua za mwisho kabla ya uzalishaji kuanza rasmi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hongji Mining Co. Ltd, Yahya Mohamed amesema kampuni hiyo itatumia teknolojia ya kisasa ya In Situ Leaching, ambayo inapunguza athari kwa mazingira kwa kutohusisha uchimbaji mkubwa wa mashimo ya wazi wala migodi ya chini ya ardhi.
Mbali na mradi huo wa Njombe, Tanzania pia ina mradi wa Ngualla uliopo Songwe ambao unatambulika kimataifa kuwa miongoni mwa maeneo yenye kiwango kikubwa cha madini ya hayo ambayo bado hayajaanza uzalishaji rasmi.
Muonekano wa madini ya Rare earth.
Mtaalamu wa uchumi, Ediko Mosha amesema uwekezaji katika madini hayo unaweza kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na mauzo ya nje, huku ukichochea ukuaji wa sekta nyingine kama usafirishaji, biashara, huduma na viwanda vya teknolojia.
