
Togo imetangaza ruhusa kwa raia wa nchi zote za Afrika kuingia nchini humo bila visa na kukaa huko kwa hadi siku 30, mradi tu wawasilishe maombi kielektroniki kupitia jukwaa la serikali, saa 24 kabla ya kuwasili nchini Togo.
Kwa hatua hii, Togo inajiunga na kundi dogo la mataifa sita pekee ya Afrika ambayo yamefungua mipaka yao kikamilifu kwa raia wa bara hilo, ikiwa ni pamoja na Rwanda, Ushelisheli, Gambia, Benin na Ghana. Kenya pia inakaribia orodha hiyo, ikiwa imeondoa nchi mbili (Somalia na Libya) katika msamaha wa visa.
Hata hivyo, ruhusa hii inabaki kuwa katika duara finyu katika bara la Afrika lenye nchi 54, ambapo nchi 48 bado zinashikilia mfumo wa visa wa jadi unaozuia harakati za watu na mitaji. Athari za kikwazo hiki cha ulazima wa kuwa na visa zinaonekana katika kiwango cha biashara ya ndani ya Afrika, ambacho hakizidi 16%, ikilinganishwa na zaidi ya 60% ndani ya nchi za Umoja wa Ulaya.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Mwendo Huru wa Watu, iliyopitishwa mwaka wa 2018, imeidhinishwa na nchi nne pekee hadi sasa, huku ikihitaji uidhinishaji wa nchi 15 ili kuanza kutumika.
Ama pasipoti ya umoja wa Afrika, iliyozinduliwa mwaka wa 2016, inabaki kuwa kwa wanadiplomasia na maafisa wa ngazi za juu wa serikali.
Kielezo cha ruhusa ya visa baina ya nchi za Afrika cha 2024 kinaonyesha maendeleo madogo, kwani Waafrika sasa wanaweza kusafiri bila visa katika 28% ya matukio ya uhamaji ndani ya bara, ikilinganishwa na 27% mwaka wa 2022 na 20% pekee mwaka wa 2016. Nchi 33 kati ya 54 hutoa msamaha wa visa kwa nchi 10 au zaidi, huku karibu robo ya wasafiri wakipata visa wanapowasili mpakani au kwenye viwanja vya ndege.
Nchi zinazopinga ruhusa ya visa zinatetea msimamo wao kwa wasiwasi wa masuala ya kiusalama, hasa katika eneo la Sahel, ambalo linakabiliwa na mojawapo ya migogoro mikubwa zaidi ya silaha duniani, pamoja na biashara haramu ya silaha na binadamu na uhalifu wa kimataifa. Katika upande wa kiuchumi na kisiasa pia baadhi ya nchi zinazopinga sera ya Afrika bila mipaka ya visa zinategemea mapato ya visa kama chanzo cha mapato thabiti, hofu ya uhamiaji wa nguvu kazi kwenda kwenye chumi zinazovutia zaidi na kadhalika.
Pamoja na hayo, wafuatiliaji wanaamini kwamba hatua ya Togo inawakilisha maendeleo chanya ambayo yanaongeza kasi katika mchakato wa kufungua milango ya nchi za bara la Afrika, lakini haionyeshi mabadiliko makubwa ya kitaasisi.
