
Dar es Salaam. Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye amefanya mabadiliko makubwa ya kisiasa kwa kutengua uteuzi wa Waziri Mkuu wake, Ousmane Sonko na kuvunja baraza lote la mawaziri, hatua inayotamatisha rasmi ushirikiano wa karibu wa viongozi hao wawili walioingia madarakani kama washirika wa kisiasa.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, uamuzi huo ulitolewa kupitia hotuba fupi iliyorushwa nchini humo usiku wa Ijumaa Mei 22, 2026 kupitia Shirika la Utangazaji la Senegal (RTS) kutoka Ikulu ya mjini Dakar, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Oumar Samba Ba, alitangaza taarifa ya Ikulu ya kuondolewa rasmi kwa Sonko serikalini.
“Kwa amri nambari 2026-1128 ya Mei 22, 2026, Rais wa Jamhuri, Bassirou Diomaye Diakhar Faye, amesitisha majukumu ya Ousmane Sonko, Waziri Mkuu, hivyo amewaondoa pia mawaziri na makatibu wakuu. Wajumbe wa Serikali inayoondoka wanawajibika kushughulikia mambo ya sasa,” alisema Oumar Samba Ba.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la RFI, hatua hiyo ya kuvunjwa kwa Serikali imekuja saa chache baada ya Sonko kuonekana mbele ya Bunge la taifa akijibu maswali ya wabunge, ambapo alisisitiza msimamo wake kuhusu uongozi na kutofautiana kimtazamo na Rais Faye.
“Mimi si Waziri Mkuu ambaye hutii na kukubaliana na kila kitu bila kujua,” alisema Sonko bungeni, akiongeza kuwa kulikuwa na kutokubaliana ndani ya Serikali, lakini hakukuwa na kizuizi cha moja kwa moja katika utendaji wa kazi za serikali.
Ujumbe wa Sonko uliozua gumzo
Baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo, Sonko aliacha maswali mengi baada ya kuandika ujumbe mfupi kwenye mitandao ya kijamii akisema: ‘Usiku wa leo nitalala na moyo mwepesi’.
Hatua hii inaashiria uwepo wa mvutano mkali kati ya viongozi hawa kiasi kwamba kuenguliwa kwake serikalini amepona kama ni muda wa kupumzika, huku duru za habari kutoka nchini humo zikionesha kuwa mvutano kati ya viongozi hao wawili ulianza kujitokeza wazi miezi kadhaa iliyopita licha ya kuingia madarakani kwa pamoja mwaka 2024.
Faye alishinda urais Machi 2024 baada ya Sonko kuzuiwa kugombea, hatua iliyomfanya amuunge mkono kama mgombea mbadala aliyemkubali kwenye uchaguzi uliopita.
Baada ya ushindi huo, Faye alimteua Sonko kuwa Waziri Mkuu Aprili 2024, hatua iliyoonekana kuimarisha umoja wa kisiasa kwa chama chao kilichokuwa kikiongoza mageuzi ya kisiasa nchini Senegal.
Chanzo cha mgogoro kati yao
Hata hivyo, tofauti za kimtazamo zilianza kujitokeza ndani ya Serikali kuhusu mwelekeo wa kiuchumi na usimamizi wa nchi.
Sonko alisisitiza mageuzi makubwa ya kiuchumi na msimamo mkali dhidi ya masharti ya taasisi za kifedha za kimataifa kama IMF, wakati Rais Faye alionekana kuelekea zaidi katika sera za ushirikiano na taasisi hizo pamoja na kulinda uthabiti wa uchumi wa taifa.
Pia, mvutano uliongezeka kuhusu usimamizi wa madeni ya nchi na mikataba ya mafuta na gesi, ambapo kila upande ulikuwa na mtazamo tofauti kuhusu kasi na namna ya utekelezaji wa sera hizo.
Hatua hizi zilisababisha mgawanyiko wa kimyakimya ndani ya serikali na baadaye kuanza kujitokeza hadharani kupitia kauli za viongozi wote wawili.
Inaripotiwa kuwa, kwa kipindi cha karibu wiki tatu kabla ya hatua ya kumfukuza, Rais Faye alinukuliwa akisema anaweza kumwondoa Waziri Mkuu huyo iwapo angepoteza imani naye, kauli iliyochukuliwa kama ishara ya mwelekeo mbaya zaidi wa mzozo huo.
Wachambuzi wa siasa wanasema hatua hiyo inaonyesha uwezekano wa mgawanyiko mpya wa kisiasa ndani ya kambi iliyoshinda uchaguzi, unaoweza kubadili sura ya kisiasa za taifa hilo.
Wachambuzi wataja athari kisiasa
Profesa Maurice Soudieck Dione kutoka nchini humo, amenukuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa akieleza kuwa pande zote sasa zitahitaji mikakati mipya ya kisiasa.
“Sasa, pande zote mbili zitalazimika kutafuta mikakati inayofaa ili kuwepo na kubadilika ndani ya uwanja wa kisiasa, ingawa Rais ana uwezo mkubwa, kuna mifumo ndani ya mfumo wa bunge ambayo inaweza kufanya kazi kwa faida ya Waziri Mkuu Sonko,” amesema Profesa Dione.
Ameongeza kuwa kutokana na mvutano huo kufikia kilele hicho, mwelekeo wa uchaguzi ujao unaweza kuongeza ushindani wa kisiasa zaidi ndani ya nchi hiyo.
“Uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2027 na uchaguzi wa urais mwaka 2029, hatari ni kwamba tutashuhudia vita kati ya walio wengi kutoka kambi ya Rais na walio wengi bungeni, hali ambayo inaweza kuwa na matokeo mabaya kwa utendaji mzuri wa masuala ya umma,” ameonya Profesa Dione.
Akizungumzia hatua hiyo na mwelekeo wa siasa za Afrika Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azaveli Lwaitama amesema ni hatua ya kawaida katika Serikali za kidemokrasia akitaja kuwa mvutano wa mawazo kati ya marafiki hao wa zamani ni hatua ya kawaida katika siasa.
“Tumezoea kuona chama kikiingia madarakani kinakaa milele, kwa Senegal kuna Rais na Waziri Mkuu, Rais kumtimua waziri ni jambo la kawaida, hii inaonesha namna kuwajibishana ndani ya serikali na vyama vya siasa kunavyoweza kufanyika.
Hawa kina Faye na Sonko ni wapinzani walioshinda uchaguzi, kutumbuana kwao kunaonesha kuwa upinzani kuongoza nchi haimaanishi kuwa ni serikali ya malaika, msuguano wa mawazo ndiyo maendeleo ikiwa hatua zinazochukuliwa ni za kikatiba na halali. Hiyo ndiyo demokrasia,” amesema.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa kiini cha mvutano baina ya viongozi kinaweza kuwa muhimu zaidi kuliko mvutano wenyewe.
Amesema ni kawaida kutofautiana lakini ni muhimu kujua chanzo na athari za jambo linaloibua mvutano huo.
“Afrika tusiogope mabadiliko kwani siyo kosa. Hiki kinatufundisha kuwa kuingia wapinzani madarakani haimaanishi msuguano wa hoja utaisha. Senegal ni mfano mzuri wa kuigwa, mabadiliko ni hatua muhimu ya maendeleo,” amesema.
