Rais Mwinyi ataka taasisi za umma kujiendesha kibiasharaRais Mwinyi ataka taasisi za umma kujiendesha kibiashara

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesema umefika wakati kuondokana na taasisi za umma ambazo zinapewa mishahara na ruzuku kutoka Serikali kuu.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Mei 23, 2026 wakati akifungua Jukwaa la Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi Zanzibar ambapo amesema utaratibu wa hazina kutoa fedha kuendesha taasisi hizo umepitwa na wakati.

“Bado zipo taasisi nyingi ambazo zinapewa mishahara kutoka serikali kuu na nyingine kupewa ruzuku hivyo umefika wakati sasa kuondokana na taasisi za aina hiyo.”

Katika kulitilia mkazo jambo hilo, Dk Mwinyi ametolea mfano nchini China ambapo   taasisi za serikali hazina tofauti na za sekta binafsi.

“Ipo mifano ya nchi ya China taasisi zao za serikali zinavyoendeshwa, huwezi kutofautisha na taasisi binafsi kwani za serikali zinafanya vizuri hivyo ni lazima kujifunza,” amesema.

Dk Mwinyi amesema hivi sasa taasisi ni lazima zitengeneze fedha ziingizwe Hazina na hayo yanawezekana kwani zipo benki Zanzibar ambazo zinafanya vizuri katika hilo, hivyo ni lazima taasisi zote za umma ziende kwa mwendo huo.

Amesema hali hiyo hufanya mashirika mengi kushindwa kutoa gawio na michango serikalini ipasavyo.

Hata hivyo, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora yatakayorahisisha kuwa na uchumi jumuishi kwa taasisi za umma na binafsi.

“Tutaendelea kuwa nanyi bega kwa bega katika kuleta mabadiliko na kufikia dhamira ya Serikali ya kufanikisha mageuzi ya kiuchumi na kijamii, tutahakikisha tunalifikia lengo hili kwa usimamizi makini kwa mashirika haya,” ameahidi.

Akizungumzia kauli mbiu ya jukwaa hilo isemayo “Uharikishaji wa Ukuaji Endelevu katika Mabadiliko ya Uongozi na Ushirikiano wa Kimkakati’ amesema   inasisitiza na kuhimiza jitihada katika kuongeza kasi ya maendeleo endelevu.

Ametumia fursa hiyo kuiagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina kuendelea kuzisimamia taasisi za umma zenye bodi na mabaraza kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi kwa taasisi hizo na kuongeza juhudi kwa mashirika ili kuwa na mashirika yenye uwezo wa kuisaidia Serikali kukuza uchumi wa nchi.

Naye, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Hamad Omar amesema jukwaa hilo limeandaliwa lengo ni kuhama katika utendaji wa kawaida na kufanya kazi na kupata matokeo ya utendaji makubwa kwa muda mfupi kwani hivi sasa dunia haimsubiri mtu.

Hata hivyo, alisisitiza kusimamia mikataba ya utendaji itakayopima ufanisi wa viongozi na taasisi kila mwaka na kutoa matokeo yatakayoleta mabadiliko ya utekelezaji wa haraka na kuhimiza mabadiliko ya kuhama kutoka kwenye maandishi kwenda kwenye utekelezaji wa haraka wa miradi ya kimkakati.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Muhammad Sanya, amesema jukwaa hilo ni muhimu katika kurahisisha utendaji wao wa kazi na kufanikisha majukumu mbalimbali hasa kufikia maono ya viongozi wakuu wa Serikali kwa mafanikio na ubunifu.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Equity, Dk James Mwangi, amesema uchumi wa Zanzibar sasa unakua kwa kasi ya kuvutia wa asilimia 8.7, na unaorodheshwa miongoni mwa chumi tano zinazokuwa kwa kasi zaidi duniani.

“Ni wazi kuwa licha ya fahari mliyonayo kwa yaliyopatikana, bado mnalenga zaidi kuendelea kukuza uchumi wenu na ndio maana neno kuongeza kasi ni sahihi, naungana na ndoto hiyo, kwa sababu tuko katika wakati wa pekee katika historia,” amesema Mwangi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *