Waziri Mkuu aonya wanaotumika kuhujumu utulivu wa nchiWaziri Mkuu aonya wanaotumika kuhujumu utulivu wa nchi

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba ameonya kuhusu uwepo wa watu wanaodaiwa kuwa vibaraka wa kuhamasisha uvunjifu wa amani nchini, akisema baadhi yao hujificha kwenye mitandao ya kijamii ili kuchochea migawanyiko ya kisiasa na kijamii.

Akizungumza leo Mei 23,2026 kwenye mkutano wa hadhara mkoani Iringa, Dk Mwigulu amesema Tanzania inaendelea kuwa na utaratibu wake wa kidemokrasia wa kupata viongozi kupitia vyama vya siasa vilivyosajiliwa Kikatiba, akisisitiza kuwa hakuna utaratibu mwingine nje ya mfumo huo.

Amesema kauli zinazojaribu kuingiza masuala ya mgawanyiko wa kidini au kuhoji misingi ya mfumo wa kisiasa wa nchi, zinapaswa kupuuzwa, akidai kuwa baadhi zinatokana na watu wanaotumika kwa masilahi binafsi.

Dk Mwigulu amesema Serikali imebaini kuwepo kwa watu wanaoendesha shughuli za makusudi za kuchochea taharuki katika jamii, huku akiwataka wananchi kuwa makini na taarifa wanazopokea hasa mitandaoni.

Amesema baadhi ya watu wanaohamasisha vurugu hawaguswi na madhara yanayoweza kutokea, bali huendelea na maisha yao ya kawaida huku wakiacha wengine wakihatarisha amani na usalama wao.

“Tusisikilize na wala tusiwe na ushirika na mtu anayekutuma kuvunja amani wakati yeye hayupo hapo. Yeye yuko kwenye starehe zake, anakunywa soda baridi na anakula mshikaki wakati wewe unahatarisha maisha yako,” amesema.

Ameongeza kuwa, hali hiyo ni ishara ya namna baadhi ya watu wanavyoweza kutumika bila kujali madhara ya matendo yao kwa jamii na Taifa kwa jumla.

“Wanaotumika kama vibaraka na wanaohangaika na vyeo tusipotezeane nao muda, mimi kazi yangu ni kushughulika na kero za wananchi hicho ndicho ambacho Rais amenituma. Watu wanahangaika na madaraka.

“Nani amewaambia madaraka niliyonayo ni madogo, hebu wasome Katiba, nimepewa majukumu; na Katiba imebainisha kuwa Waziri Mkuu atakuwa na madaraka ya juu ya udhibiti, usimamizi wa shughuli za Serikali za kila siku na usimamizi wa shughuli za Serikali bungeni. Hivi kweli mtu mwenye akili timamu utawaza hivyo vyeo wanavyosema vibaraka,” amehoji Mwigulu na kuongeza:

“Niwaambieni Watanzania, kuna michezo mingi tunachezewa na hawa vibaraka, wakitafuta kutugombanisha kila leo, nimeona niyaseme haya kwa sababu jambo la kijinga likirudiwa rudiwa na lisipopata ufafanuzi huanza kuonekana la maana.”

Dk Mwigulu amesema amekuwa akifuatilia kwa karibu mienendo ya kimataifa na kujifunza kutokana na migogoro iliyowahi kutokea na mara nyingi migogoro hiyo huendeshwa na watu wenye masilahi maalumu, ambao hupewa majukumu ya kuchochea vurugu kwa njia mbalimbali, zikiwamo za kisiasa na kiuchumi.

“Wapo vibaraka na wako kazini. Wakati ninyi mnapata kipato halali kwa jasho, wao wanatumika kuvuruga amani,” amesema.

Dk Mwigulu amesema hata katika nchi nyingine baadhi ya watu wamekuwa wakitumiwa kwa njia fiche kuleta misuguano ya kijamii, huku malengo ya msingi yakiwa tofauti na yale yanayoelezwa hadharani.

Amesema Serikali itaendelea kuwa macho dhidi ya watu wanaotaka kuhatarisha amani ya nchi, akisisitiza kuwa, amani ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ustawi wa wananchi, hivyo kila Mtanzania ana jukumu la kulinda tunu hiyo.

Kuhusu matukio ya utekaji

Akizungumzia mfululizo wa matukio ya utekaji amesema mashambulizi na vurugu zilizowahi kujitokeza nchini si matukio ya kawaida, bali ni sehemu ya michezo ya vibaraka inayolenga kuigawa Tanzania na kuondoa amani iliyopo.

Kutokana na hilo, amewataka Watanzania kuwa macho na kuanza kutafakari kwa kina matukio yanayotokea badala ya kuyachukulia kawaida bila kujiuliza malengo yaliyopo nyuma yake.

 “Unakaa hivi unasikia sister katekwa, mara padri katekwa, mara mwingine katekwa ameumizwa na amekutwa na pingu. Hii ni michezo na haijaanza jana,” amesema.

Dk Mwigulu amesema matukio hayo yanahitaji kutazamwa kwa jicho la tahadhari, kwa kuwa mara nyingi huambatana na ajenda zinazolenga kuvuruga mshikamano wa Taifa.

“Watanzania tuamke, hizi ni ajenda za watu wenye akili wanaolitafuta Taifa letu. Sio mambo ya kipuuzi puuzi tu,” amesema.

Akitolea mfano wa matukio yaliyopita, Waziri Mkuu amesema kuna kipindi viongozi wa vijiji katika eneo la Kibiti walikuwa wanauawa mashambani bila wahalifu kuchukua chochote, hali iliyozua hofu kubwa.

Amesema pamoja na matukio hayo kutokea kwa wingi, wananchi wengi hawakuwahi kujiuliza lengo la mashambulizi hayo lilikuwa ni nini.

“Kila siku mwenyekiti wa kijiji anauawa shambani, hawachukui hata jembe. Tumewahi kujiuliza walikuwa wanaua ili iweje?” amehoji.

Amesema baada ya matukio ya Kibiti, kukafuata matukio ya mabomu kurushwa maeneo mbalimbali yakiwamo makanisa na mikutano ya kisiasa, jambo lililokuwa na lengo la kuchochea migogoro ya kidini na kisiasa.

“Bomu limerushwa kanisani, hatujiulizi walikuwa wanatafuta nini? Wanajua kabisa ikitokea pale itaonekana kuna mgogoro wa kidini,” amesema.

Amesema hata mashambulizi yaliyowahi kutokea kwenye mikutano ya kisiasa yalikuwa na lengo la kuibua taharuki na kuifanya jamii ionekane imegawanyika kisiasa.

“Walikuwa wanapima waone wakifanya hivi, itaonekana moja kwa moja kuna mgogoro wa kisiasa,” amesema.

Waziri Mkuu pia amegusia tukio la kukamatwa kwa mtu aliyeingia nchini akiwa na mabomu, akisema hatua hiyo ilionesha namna baadhi ya watu wanavyoweza kutumika kuleta taharuki.

“Anasema eti kuna insecurity ndiyo maana akaingia na mabomu kujilinda. Ni nchi gani watu wanaenda na silaha kujilinda?” amehoji.

Amesema baadhi ya watu wanaotekeleza vitendo hivyo huacha alama zinazolenga kuwafanya wananchi wachukiane na kuipoteza imani kwa taasisi za nchi.

Kutokana na hali hiyo, Dk Mwigulu amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuwa macho dhidi ya watu wanaotaka kuhujumu amani ya Taifa.

“Nielekeze vyombo vya ulinzi na usalama, kueni macho na njama za aina hii. Shughulikeni na waovu wa aina hiyo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *