Miaka 22, ni umri wa mtu mzima. Mwenye uwezo wa kumiliki totoz kadhaa kama siyo ‘waifu’ kabisa. Katika umri huo tayari Dk Salim Ahmed Salim, alikuwa Balozi wa Bongo kule Misri. Sijui simbilisi, njegere na tumblli za ‘jenzii’ kama zinamjua huyu mwamba.
Sipo kuzipatia historia hizi kware na mbilimbi za kizazi kipya. Nipo hapa kishangwe zaidi, kimizuka zaidi. Mchizi wangu kabisa hata ‘eji’ zetu zipo sawa, Mikeli Ateta kanipa furaha niliyoikosa miaka 22 sasa. Umri wa Anko Reagan, mtoto wa dada yetu wa kwanza.
Anko Reagan kishaua masomo yake Mlimani pale. Hii ina maana kazaliwa, kasoma hadi eñimu ya digrii. Bila kuona furaha ya Anko wake, nikishangilia timu yangu ya Asenali ikibebea ndoo. Ni safari ndefu sana, lakini ncha yake imeletwa na Ateta.
Huu ndo wakati wa pisi zenye malengo na mimi kuninasa. Tena kirahisi sana, maana waswahili husema usifanye maamuzi ukiwa na hasira au furaha sana. Mimi nina furaha sana, na nipo tayari kufanya maamuzi yoyote. Kazi kwenu ninyi.
Huu ndo wakati ambao naweza kuoa bila kujali kabila, rangi, sura, shepu, tabia gharama za harusi wala dini. Nina furaha mpaka na furaha yenyewe ina furaha. Oyaa niko ‘hepi’ bila ‘krismasi’ na ‘nyu yia’. Hizi ni nyakati ambazo bila naweza kugawa hata figo.
Wakati ‘Aseno’ inabeba ndoo bila kufungwa. Ikulu ya Magogoni aliishi Mkapa, Ilala Boma alichili Mzee Makamba. Ni wakati Juma Nature yupo na Sinta, Miss Tizedi ni Sylvia Bahame, Amina Chifupa ni mtangazaji, kocha wa Simba ni James Siang’a.
Uwanja mkubwa nchini ni Uhuru ‘Shamba la Bibi’. TID anatamba na Zeze, Pro. Jay anakimbiza na Promota Anabeep. Ukumbi wa burudani mkubwa na wa maana ni Diamond Jubilee. Ngwea hana albamu wala Mikasi, ana singo moja tu ya Geto Langu tu.
Binti ukitaka mume mvumilivu wa matukio, jibebee shabiki wa Aseno. Usione tunatamba sana wakati huu, ni baada ya miaka 22 ya uvumilivu. Aseno kama wale Wayahudi waliotembea miaka 40 Jangwani wakiisaka Kaanan na Mussa wao.
Mzee Wenga alituacha kibwege sana. Siyo kwamba tunampuuza mzee wa watu, ‘noo’ kuna mengi mazuri katuachia. Yule dingirai alipotua ‘Landani Tauni’ kuinoa Aseno 1996. Alibadilisha mambo mengi, kama staili ya kucheza na menyu kwa mafutibola wetu.
Asenali kutoka mpata mpatae, weka kigingi niweke chuma. Hadi soka la usiniguse, nipe mbovu na mimi nikupe nzuri. Ufundi kibao na pasi nyingi nyingi, huyu Pep Gadiola akasoma. Mzee Wenga soka lake lilikuwa linavutia kwa kiwango cha mahaba ya Zuchu kwa Mondi.
Ukiondoa bia na nyama choma kwa wakati ule. Soka la Aseno ilikuwa ni starehe kubwa kinoma. Hata mashabiki wa ‘Manchesta Unaitedi’ walitamani kama siyo kupendelea kutazama soka la Aseno. Kuliko kombolera za soka la Fagasoni na wavuta bange wake.
Kwa mabwege mliozaliwa juzi juzi tu, soka la Aseno ilikuwa ni zaidi ya lile la Gadiola na Messi wake. Aseno waligonga mapasi kuliko udwanzi wa ‘Iniesta na Xaiv ageini.’ Kama hutaki kenge wewe katazame mechi ya Aseno na ‘Basa’ pale Emiretisi.
Yule mvuta fegi wa kuitwa ‘Jaki Wilishea’, alikuwa anawakusanya wale viungo wa ‘Basa’ atakavyo. Zama sana uvunguni, beba mali tuondoke. Kimbiza pale kiduarani na ‘Basa’ akafa mbili moja. Ni ule ubongo wa Wenga uliorutubisha vipaji vya watoto pale ‘Landani Kolnei’.
Aseno ndo timu pekee ambayo, wachezaji wake waliingia graundi na kuaamkia wachezaji wa timu pinzani. Walcoti, Wlishea, Gibbs, Ramsey, Denlisoni, Samir Nasri, Hleb, Diabi, Song. Hawa wote walikuwa wavulana wanaotesa mazee ya Oldi Trafodi.
‘Ene wei’ baadaye Mzee Wenga, akaanza kuishi maisha ya Mangi wa Marangu. Ubahili uliopitiliza, alinunua wachezaji wa buku jero na kuwauza kwa laki mbili. Kulipa mkopo wa kausha damu, chama liwe na uwanja wake. Sasa hivi tunajidai na liuwanja pana.
Mishe za kulipa madeni zilifanya tushindwe kununua majitu. Kama Tieri Henri, Kanu, Sol Campbel, Vieira, Bergkamp, Overmas, Edu, Emmanuel Petit, Tonny Adams, Martin Keown, Le Dxon, Winter Burn na Ashley Cole. Ndo ikawa wasindikizaji.
Ateta ndo Nabii Joshua alipokea jukumu la Wenga a.k.a Mussa. Na sasa tupo Kaanani, kwenye nchi ya ahadi tunakula mema. Ni mabingwa rasmi wa ‘Epielo’, sisi ndo wenye nyumba kwa sasa pale Uingereza. Ateta katufanya tuwe katili mpaka YUROPA.
Usilete stori za Rio Fedinandi na goli la Chama. Huu ni msimu wa bata la ubingwa wa Aseno. Sitaki kusikia tatizo na shida za mtu, nipo katika dunia yangu hii sasa. Jambo nililosubiri miaka 22 lipo mezani. Kombe la ubingwa wa ligi kuu Uingereza.
Bastola cash and… toa code someka… wapi ilipo bata wapi leo kinaeleweka… na pesa mingi mpaka natamani jiteka…. then watu wapo King, Stone kama Jamaica…. ni mamodel, madodo wa kuroll na magangasta… Divas and Hustlers, Paper Chasers!
