Dar kujenga maegesho ya magari vituo vya mwendokasiDar kujenga maegesho ya magari vituo vya mwendokasi

Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam uko katika mchakato wa kujenga maegesho ya magari katika vituo vikubwa vya mwendokasi ili kuwapa wananchi nafasi ya kuegesha magari na kutumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT).

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema hayo leo Mei 25, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari namna walivyojipanga kukabiliana na foleni wakati wa michuano ya AFCON 2027.

Chalamila amesema ili kukamilisha hilo, tayari mazungumzo yameanza na halmashauri mbalimbali za jiji ili zitenge maeneo ya maegesho karibu na vituo vikubwa vya mwendokasi.

Amesema wananchi wengi sasa wanaingia katikati ya jiji wakiwa na magari binafsi kutokana na kukosekana kwa maeneo rasmi ya kuyaacha kabla ya kuendelea na safari kwa kutumia mwendokasi.

“Tunataka mtu anayetoka Kinyerezi au maeneo mengine akiwa na gari lake, afike sehemu maalumu apaki gari lake kisha apande mwendokasi kwenda katikati ya jiji. Hii itasaidia kupunguza magari mengi yanayoingia mjini,” amesema Chalamila.

Kauli hiyo imekuja wakati Mkoa wa Dar es Salaam ukiendelea kukabiliwa na msongamano wa magari katika barabara kuu, hali inayochangiwa na ongezeko la watu, shughuli za kiuchumi pamoja na maboresho ya miundombinu yanayoendelea.

Katika hatua nyingine, Chalamila amesema matumizi ya aina zote za vyombo vya usafiri katika barabara kuu nayo yanachangia msongamano.

Amesema katika baadhi ya barabara kuu kuna magari makubwa, bajaji, pikipiki, baiskeli pamoja na mikokoteni ambavyo vyote hutumia njia moja jambo linaloleta msongamano wa magari.

“Ukifika kwenye baadhi ya barabara utakuta kuna lori, bajaji, pikipiki, mikokoteni na hata mifugo inapita humo humo. Hii nayo ni changamoto. Sisi kama mkoa tunapitia uwezekano wa kuweka utaratibu wa kudhibiti baadhi ya vyombo vya usafiri kuingia katika barabara kuu za jiji,” amesema.

Pia, Chalamila amesema mkoa unafikiria kuweka mfumo wa tozo kwa baadhi ya magari yanayoingia katikati ya jiji kama inavyofanyika katika baadhi ya mataifa duniani ili kupunguza msongamano usio wa lazima.

“Katika miji mingi duniani ukiingia katikati ya jiji kuna utaratibu wa kulipia au muda maalumu wa maegesho. Hii inaleta nidhamu ya matumizi ya magari mjini,” amesema.

Amesema hatua zote hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza foleni katika Jiji la Dar es Salaam na kuboresha usafiri kwa wananchi.

Chalamila amesema hayo ikiwa ni siku chache tangu Mwanafunzi wa Shahada ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar wa Salaam (UDSM), Tukay Thomas kuibuka mshindi wa shindano lililofanywa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega la kuibua mawazo ya kutatua kero ya foleni nchini.

Waziri Ulega alisema wizara iliamua kuwashirikisha vijana katika kutafuta suluhisho za changamoto za usafiri mijini ili kuhamasisha matumizi ya maarifa ya darasani katika vitendo na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa.

Idadi ya watu, biashara

Katika hatua nyingine, Chalamila amesema uwepo wa foleni ndani ya jiji unachangiwa na ongezeko la idadi ya watu na kiwango cha maisha.

“Ukija Dar es Salaam utakuta kaya moja ina magari mawili, matatu au manne. Hiyo inaonesha hali ya maisha imepanda lakini pia inachangia magari kuwa mengi barabarani,” amesema.

Mbali na hilo, amesema matengenezo makubwa ya barabara yanayoendelea katika maeneo mbalimbali ya jiji nayo yamekuwa chanzo kikubwa cha foleni.

Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni barabara za mwendokasi, madaraja pamoja na miradi inayotekelezwa chini ya Mpango wa Maendeleo wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

“Barabara nyingi sasa hivi zimefunguliwa kwa sababu ya ujenzi unaoendelea. Kuna zinazojengwa kwa fedha za Serikali, nyingine kwa fedha za Benki ya Dunia (WB) na nyingine kwa fedha za Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB),” amesema.

Amesema Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kurudisha hali ya kawaida ya matumizi ya barabara.

“Pia, maboresho makubwa yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam nayo yamechangia kuongezeka kwa msongamano wa magari ya mizigo. Ongezeko la mizigo inayopitia bandari hii, limekuwa kubwa kuliko ilivyotarajiwa, hali inayosababisha malori mengi kuingia na kutoka bandarini kila siku,” amesema.

“Bandari ilikisiwa ifikapo mwaka 2030 iwe inapokea tani milioni 30 za mizigo, lakini mwaka jana tayari tulifikia tani milioni 27. Hii inaonesha biashara imeongezeka sana, hivyo ni ishara kuwa lazima kitu kifanyike ili kuufungua mji,” amesema.

Amesema pamoja na maboresho yaliyofanyika bandarini, bado uwezo wa reli ya kusafirisha makontena kwenda Kwala haujaendana na kasi ya upakuaji wa mizigo bandarini, hivyo kulazimika kutumia malori mengi kusafirisha mizigo hiyo.

“Leo makontena zaidi ya 2,000 yanashushwa kwa siku lakini reli haiwezi kubeba yote kwa wakati mmoja, hivyo malori yanabeba sehemu kubwa ya mizigo hiyo,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali inaendelea kuboresha reli pamoja na Bandari Kavu (ICD) na Kwala ili kupunguza utegemezi wa malori katika kutoa mizigo katikati ya jiji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *