
Milio ya risasi imesikika karibu na Ikulu ya White House jioni ya Jumamosi, Mei 23. Kulingana na ripoti za awali, mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka ishirini alivamia kituo cha usalama kabla ya kupigwa risasi na maafisa wa Secret Service.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Hili linaweza kuwa jaribio lingine la mauaji dhidi ya Rais wa Marekani Donald Trump. Na kama ni kweli litakuwa shambulio la nne. Siku ya Jumamosi, Mei 23, muda mfupi baada ya saa 12 jioni, mwanamume mmoja alifyatua risasi katika kituo cha usalama karibu na Ikulu ya White House. “Alitoa bunduki kwenye begi lake na kuanza kufyatua risasi,” alielezea Anthony Guglielmi, msemaji wa Secret Service, Shirika la Ulinzi wa Viongozi wa Marekani, ambalo maafisa wake walimuua mshambuliaji.
“Maafisa wa Secret Service walirudisha risasi na kumpiga mshukiwa, ambaye alisafirishwa hadi hospitali ya eneo hilo ambapo alitangazwa kuwa amefariki.” Wakati wa tukio la kurushiana risasi, mpita njia pia alipigwa risasi,” afisa huyo aliongeza katika taarifa, bila kutoa maelezo kuhusu hali ya mpita njia huyo.
Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa Ikulu ya White House wakati wa tukio hilo, baada ya kufuta safari zake zote za wikendi kutokana na mgogoro na Iran. Polisi walizingira jengo hilo, na wanajeshi kutoka kikosi cha ulinzi wa taifa walimzuia mwandishi wa habari wa AFP kuingia katika eneo hilo.
Waandishi wa habari waliokuwa kwenye bustani ya Kaskazini wakati huo waliripoti kwene mtandao wa kijamii wa X kwamba waliamriwa kukimbia kujificha kwenye chumba cha waandishi wa habari cha Ikulu ya White House. “Tulisikia milio kati ya milio 20 na 25 ambayo ilisikika kama fataki, lakini ilikuwa milio ya risasi, na kila mtu akaanza kukimbia,” mtalii kutoka Canada aliyekuwa katika eneo hilo ameliambia shirika la habari la AFP.
Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vilimtambua mshukiwa huyo kama Nasire Best mwenye umri wa miaka 21. Kulingana na vyombo hivyo vya habari, mtu huyu kutoka Maryland, karibu na Washington, alikuwa na historia ya matatizo ya afya ya akili na tayari alikuwa anajulikana na Secret Service kwa kuzunguka-zunguka Ikulu ya White House mara kadhaa. “Alikuwa na historia ya vurugu na alionekana kupendezwa sana” na jengo hilo, alisema Rais wa Marekani Donald Trump.
