
Dar es Salaam. Baada ya kutangaza nia ya kurejea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, amepokewa rasmi ndani ya chama hicho kwa kukabidhiwa kadi ya uanachama.
Mbunge huyo wa zamani wa Iringa Mjini kupitia Chadema, alikihama chama chake hicho, Juni 30, mwaka juzi kwenda Chama cha Mapinduzi (CCM), alikokaa kwa mwaka mooja na miezi 11.
Baada ya kuihama Chadema, Mchungaji Msigwa alitumika katika majukwaa ya siasa na kampeni ya CCM kukikosoa chama hicho cha upinzani. Mara nyingi aliambatana katika ziara za aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi, ambaye sasa ni Makamu wa Rais.
Mchungaji Msigwa alitangaza nia ya kurejea Chadema kupitia kurasa za mitandao yake ya kijamii, usiku wa jana Jumamosi, Mei 23, 2026 na asubuhi ya leo Jumapili, Mei 24, 2026 amechapisha picha ya kadi ya uanachama aliopewa.
Katika taarifa yake ya awali ya kutangaza kurudi Chadema, Msigwa aliandika yaliyotokea Oktoba 29, mwaka jana yaliyohusisha mauaji ya watu yalimuumiza na ni miongoni mwa sababu za uamuzi huo.
“Matukio hayo yaliniumiza na kunifanya nishindwe kuendelea kuishi katika huzuni kubwa na ukimya,” ameandika na kuwaomba radhi wanachama wa chama hicho.
Hata hivyo, Mwananchi Mei 23, 2026 ilimtafuta kutaka kuthibitisha ujumbe huo kama wa kwake, naye alithibitisha umeandikwa naye.
Taarifa ya kupokewa kwa Msigwa, ameichapisha katika ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani twitter), akiambatanisha na kadi ya uanachama yenye namba za usajili CDME403082.
Katika chapisho lake hilo ameandika, “asante viongozi wa tawi langu kwa kunikubalia kuwa mwanachama tena. Heshima kwenu.”
Mbali na hilo, kurasa za mitandao ya kijamii za Chadema, zilichapisha ujumbe wa Msigwa wa nia ya kurudi katika chama hicho na kuandika, “karibu tena Chadema Mchungaji Msigwa.”
