
Canada. Wengi wetu tumeshasikia mengi kuhusiana na wanawake wa Kitanga. Tunaposema “wanawake wa Kitanga,” ni lazima tukiri kwanza kuwa Mkoa wa Tanga una makabila mengi na tofauti. Hivyo, hatuwezi kusema kwa kujiamini kuwa wanawake wote wa mkoa huo wana sifa au tabia zinazofanana.
Hata hivyo, tutatumia dhana hii ya jumla ili kujibu swali linalotokana na mtazamo huo wa jamii.
Leo tutawaangazia wanawake wa Kitanga, japo si wote. Wale wasiowajua vizuri na wanaoshangazwa na ufundi wao katika mapenzi, mara nyingi hudhani kuwa wanawake hawa wanatumia limbwata au dawa za kiasili. Ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho.
Wanawake wa Kitanga wanasifika kwa uchangamfu, ukarimu, na ustadi mkubwa katika masuala ya mapenzi na ndoa.
Kwa mfano, mara nyingi utasikia watu wakisema: “Kuingia Tanga ni rahisi, lakini kutoka ni mtihani.” Je, ni kwa nini? Hatuwezi kutoa jibu moja la mkato, na huenda tusijue chimbuko hasa la usemi huu.
Hata hivyo, hebu tudurusu na kudadavua kidogo sifa za wanawake hawa. Hawa ni wanawake wanaosifika kwa kuweza kumuandalia mume maji ya kuoga yaliyochanganywa na marashi au manukato, ili akitoka bafuni anukie vizuri. Je, hili si jambo la kuvutia? Ni wapi pengine utaratibu huu unafanyika kwa kiwango hiki hapa nchini?
Hebu jifikirie; mume ni mvuvi, anarejea nyumbani akiwa na shombo la samaki. Wewe kama mke unamfanyia nini ili arudi kwenye hali ya usafi na harufu nzuri?
Au mume ni mkulima labda anarudi nyumbani jioni baada ya kushika jembe kwa saa saba, akiwa ameloa jasho. Utamsaidiaje kupumzika?
Wapo wanaokwenda mbali zaidi na kudai japo hatuna ushahidi wa kisayans kuwa mwanamke wa Kitanga anaweza hata kumbeba mumewe mgongoni kama mtoto kumpetipeti! Lahaula! Nani asiyevutiwa na ukarimu na mahaba ya namna hii?
Je, mambo haya ni limbwata kweli au ni usafi na malezi? Hamjawahi kusikia msemo kuwa “mwanamke ni usafi”? Kama tabia hizi ndizo zinazoitwa limbwata, basi kwenye ndoa linaswihi na kuruhusiwa kabisa.
Japo usafi unapaswa kuwa jambo la faragha na la hiari kwa wanandoa wote, bado kuna wengi wanaoteseka kwenye ndoa zao hasa kinamama, kwa kutozingatia usafi wa miili na wa ndimi zao (maneno wanayotamka).
Kwa wanaotaka kuepuka dhoruba za ndoa, usafi si hiari tena, bali ni wajibu.
Huwezi, kwa mfano, kuingia kitandani ukiwa mchafu au unanuka jasho halafu utegemee mambo yaende vizuri.
Japo linaweza kuonekana jambo la kawaida, je, matatizo haya hayapo? Ni wangapi wanaoweza kuwaambia wenzao ukweli kuwa ni wachafu na wanapaswa kujisafisha? Msioneane aibu; ambianeni ukweli.
Wapo wasiopenda kukosoana kwa maneno bali hutumia vitendo. Ni heri kulaumiana kwa kuambiana ukweli iwe kwa maneno au kwa vitendp, kuliko kukwazana, kuogopana, na hatimaye kufarakana kwa jambo dogo lakini la msingi kama usafi.
Je, ni bora kunyamaza na kuumizana moyoni, au kuambiana na kutatua tatizo pamoja?
Kuna baadhi ya jamii ambazo watu wake hawana utaratibu wa kupiga mswaki kabla ya kulala. Mtu anashinda anakula mchana kutwa, kisha anaingia kitandani hivyo hivyo. Wengine hawaogi wala hawanawi kabla ya kulala.
Jamani, binadamu si mnyama wa kulala na kuamka mchafu. Hata kuku akikaribia kuingia ‘mtandoni hujisafisha kwa michanga ili alale akiwa safi!
Tukizingatia hayo na kuyahusisha na sifa za wanawake wa Kitanga, tunaweza kupata jibu la fumbo hili hata bila kuwahoji. Mbali na usafi, kuna methali isemayo: “Njia ya kufika kwenye moyo wa mwanaume inapita tumboni kwake.”
Hapa ndipo umuhimu na ustadi wa mapishi unapoingia. Jiulize, ni wanawake wangapi leo hii wanaojua mapishi ya kiwango cha kumfanya mume achukie kabisa vyakula vya hotelini?
Anayebisha hili ajiulize: Kwa nini biashara ya hoteli na migahawa ni moja ya biashara kubwa na zenye faida kubwa duniani? Ni kwa sababu binadamu wote wanapenda chakula kizuri.
Huwezi kupika michemsho isiyo na ubunifu kila siku ukategemea kushindana na mke anayejua kuandaa kuku wa kupaka au mnofu uliokolea viungo.
Wapo watu matajiri wasiokula vyakula vizuri majumbani mwao, si kwa sababu hawana uwezo wa kifedha, bali ni kwa sababu wenza wao hawajui kukaangiza. Na wapo masikini wanaokula vizuri sana kwa sababu tu ya ufundi wa mke jikoni. Kimsingi, hakuna chakula kibaya; kinachokifanya chakula kiwe kitamu au la, ni ustadi wa mapishi.
Mambo ya chumba cha kulala hayo hatuyagusi kwa leo. Hata hivyo, kama ilivyo kwenye usafi na mapishi, huko nako kunahitaji juhudi, maandalizi, na ufundi si haba. Leo tunaishia hapa.
