Urusi yafanya shambulio kubwa Kyiv, Ukraine, manusura asema “natumai rafiki zangu wako hai”Urusi yafanya shambulio kubwa Kyiv, Ukraine, manusura asema “natumai rafiki zangu wako hai”

Afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa nchini humo ametoa wito wa kusitishwa kwa madhara dhidi ya raia.

Inakadiriwa kuwa takribani watu wanne wameuawa, na wengine takribani 80 wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa mamlaka za Ukraine, makumi ya majengo ya makazi, shule kadhaa na kituo cha usambazaji maji vilipigwa, na soko liliungua.

Vanya mwenye umri wa miaka 13, ambaye nyumba yake mjini Kyiv ilipigwa katika shambulio hilo, amenusurika  bila kujeruhiwa. “Natumaini tu majirani na marafiki zangu wako hai,” amewaeleza wafanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) waliokuwa eneo la tukio.

UNICEF imeeleza kuwa shambulio hilo kubwa na la muda mrefu ni kama “usiku wa kutisha kwa watoto na familia”.

Kuamshwa na ‘sauti za kutisha za vita’

Matthias Schmale, afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, amesema kwamba yeye na wenzake, kama wakazi wote wa Kyiv, waliamshwa tena usiku wa manane na “sauti kubwa na za kutisha za vita”. 

Schmale amebainisha kuwa shambulio hilo lilidumu takribani saa saba, na mabaki ya makombora yalianguka na kusababisha moto katika maeneo mbalimbali ya jiji. “Raia wanaishi katika hatari kubwa kutokana na vurugu hizi zisizokoma,” amesema Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu. “Kiwango hiki kikubwa cha madhara kwa raia lazima kikome.”

Ofisi za WHO zashambuliwa

Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) mjini Kyiv zilikuwa miongoni mwa majengo yaliyoharibiwa katika shambulio hilo la usiku.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kupitia mtandao wa X kuwa mabaki ya kombora yaliharibu madirisha ya ghorofa ya tatu ya jengo linalotumiwa na mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa. Hata hivyo hakuna mfanyakazi aliyejeruhiwa.

Dkt. Tedros ametoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya vituo vya afya na raia, na akarudia wito wa WHO wa kusitisha mapigano na kwamba, “amani ndiyo dawa bora.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *