
Wanaume, wanawake, na watoto 243 kutoka Côte d’Ivoire ambao walikuwa wameishi nchini Tunisia kwa miezi kadhaa katika mazingira ngumu sana, wameamua kurudi nyumbani na wamerejeshwa Abidjan mwishoni mwa wiki hii iliyopita, Mei 23 na 24. Wakimbizi hao wanasema kurudi nyumbani kwa hiari mara nyingi kumeonekana kama unafuu, ingawa hawakuweza kufika bara la Ulaya kama walivyotarajia awali.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Abidjan, Benoît Almeras
Walichagua kurudi nchini mwao Côte d’Ivoire. Mwishoni mwa wiki hii iliyopita, wahamiaji 243 kutoka Côte d’Ivoire- wengi wao wakiwa wanaume, lakini pia baadhi ya wanawake na watoto wachache – walifika Abidjan kwa ndege maalum kutoka Tunisia. Zoezi hili la kurejeshwa nyumbani ambalo liliandaliwa na nchi hizo mbili, kulingana na mamlaka inayoshughulikia masuala ya raia wa Côte d’Ivoire walio ugenini (DGIE), kurudi huku kwa hiari kunawakilisha unafuu kwao, licha ya kushindwa kwa lengo lao la awali, ambalo lilikuwa kufika bara la Ulaya.
Katika kituo cha mapokezi katika wilaya ya Abobo, ambapo wamefikia wakati wakisubiri kurudi kwa familia zao, wengi wanashuhudia hali ngumu sana ya maisha waliyopitia nchini Tunisia. Kwa mfano, hii ndiyo hali iliyomkuta Fanta, ambaye amerudi baada ya kuishi Sfax kwa miaka miwili. “Hali ilikuwa ngumu kwa kweli… Kuna mahali huko Sfax, kando ya bahari, ambapo polisi wanapokuja, wanaharibu kila kitu, wanachoma kila kitu, na kukufukuza kama wanyama,” anasimulia, kabla ya kusema kwamba alijaribu kuvuka Bahari ya Mediterania mara sita. “Lakini hakufaulu,” anasema.
“Wengi wanarudi wakiwa na masikitiko makubwa”
Aliposikia jina lake likitajwa, Fanta—ambaye alikuwa akisubiri chini ya eneo lililofunikwa ambapo mtumishi wa umma alikuwa akihudhuria “kuwaachilia” wahamiaji hawa kutoka Côte d’Ivoire waliochagua kurudi nyumbani—alichukua sanduku lake la nguo na aingia ndani ya teksi ili kujiunga na wazazi wake huko Yopougon. Wengine walikuwa wakisubiri mabasi kwenda Daloa na Bouaké, miongoni mwa maeneo mengine. Baadhi walipendelea kuficha nyuso zao, kwa kukataa kutambuliwa. Watu wengi wanasita kurejea kwa hiari katika nchi yao, anaelezea Mamadou Sako, mmoja wa maafisa wa DGIE: “Wengi wanarudi wakiwa na masikitiko makubwa kwa sababu wazazi wao walikuwa wameweka matumaini yao kwao… Lakini wanaporudi nyumbani, matumaini hayo hutoweka, na wanarudi mikono mitupu.”
Kwa mujibu wa DGIE, changamoto ni kuwashawishi watu hawa wanaokimbilia uhaibuni kwamba fursa pia zipo nchini Côte d’Ivoire, iwe ni katika suala la mafunzo au ajira. “Hatutaki kuwakatisha tamaa,” anaongeza Mamadou Sako. “Tunajaribu tu kuwashawishi kwamba wanaweza kubaki nchini Côte d’Ivoire au kwamba kuna njia bora za kuondoka kuliko uhamiaji haramu.”
Akiwa amerudi nchini mwake baada ya kukaa miaka miwili nchini Tunisia, Cissé ni miongoni mwa wale ambao hawajasikitika. “Nimerudi nyumbani nikiwa mzima. Ninaweza kufanya kazi na kuwa na maisha bora. Bado nina matumaini!” anasema dereva huyu mwenye umri wa miaka arobaini, ambaye anaona kurudi kwake Côte ‘Ivoire kama nafasi ya pili baada ya kukaa miezi minane gerezani kwa kukosa kibali cha kuishi wakati alipokimbilia nchini Tunisia.
Kati ya mwaka 2022 na 2025, karibu wahamiaji 8,700 kutoka Côte d’Ivoire walichagua kurudi nyumbani kwa msaada wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji. Theluthi moja yao walirudi kutoka Tunisia.
