DRC: WHO yapanua hatua za mazishi salama wakati huu hatua dhidi ya Ebola zikikabiliwa na upinzaniDRC: WHO yapanua hatua za mazishi salama wakati huu hatua dhidi ya Ebola zikikabiliwa na upinzani

Wakati idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Ebola ya virusi vya Bundibugyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikifikia 101 na 10 kati yao wakiwa wamefariki dunia, juhudi za kukabili kuenea kwa ugonjwa huo zinakabiliwa na upinzani kutoka kwa jamii hususan wakati wa mazishi.

Dkt. Marie Roselyne Belizaire, ambaye ni Mkurugenzi wa Mwitikio wa Dharura wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, (WHO) Kanda ya Afrika amesema mazishi salama ya watu waliofariki dunia kwa Ebola ni muhimu kwa sababu Ebola huenea kupitia kugusana na majimaji ya mwili—ikiwemo kutoka kwa watu waliokufa.

Ikumbukwe kuwa hadi sasa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo havina tiba wala chanjo.

Kanuni za mazishi ili kudhibiti kuenea kwa Ebola

Akihojiwa na Idhaa ya Kifaransa ya Umoja wa Mataifa kutoka Kinshasa, mji mkuu wa DRC, Afisa huyo amesema, “hata hivyo, mila nyingi za mazishi huhusisha kuosha au kuugusa mwili, jambo linaloongeza hatari kubwa ya maambukizi.”

“Ili kukabiliana na hali hiyo, WHO imetekeleza utaratibu wa mazishi yenye heshima unaolinganisha heshima ya kitamaduni na kinga dhidi ya maambukizi,” amesema Dkt. Belizaire akitaja taratibu hizo kuwa ni:

  • Familia haziruhusiwi kuugusa mwili, lakini zinaweza kuhudhuria mchakato wa mazishi.
  • Jamaa hupewa vifaa vya kujikinga ili waweze kushuhudia mazishi kwa usalama.
  • Familia zinaweza kufanya sala na taratibu za kidini, mradi zisihusishe kugusana kimwili.
  • Timu za mazishi hueleza kila hatua ili kuhakikisha uwazi na kupunguza hofu.

Dkt. Belizaire amesisitiza kuwa familia “zina nafasi ya kuwaomboleza wapendwa wao,” ingawa mwili hauwezi kurejeshwa kwao.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa upinzani wa hivi karibuni ulisababisha vurugu kubwa.

Changamoto katika kusimamia mazishi salama

Licha ya hatua hizo, bado kuna vikwazo kadhaa:

  • Taarifa potofu zinazochochea uvumi kuwa miili inashughulikiwa vibaya
  • Vitisho vya kiusalama dhidi ya timu zinazohusika na mazishi
  • Kuchelewa kwa usafirishaji wa vifaa kwenda vituo vya afya vilivyo mbali
  • Mila na desturi zilizokita mizizi ambazo ni vigumu kubadilishwa haraka

Mambo haya yamefanya iwe vigumu zaidi kwa timu kutekeleza mazishi kwa wakati—hatua muhimu katika kukatiza mnyororo wa maambukizi.

Upinzani wa jamii unapunguza juhudi muhimu za mwitikio

Dkt. Belizaire amesisitiza kuwa matukio kadhaa ya hivi karibuni ya kiusalama—ikiwemo mashambulizi dhidi ya vituo vya afya na kuvurugwa kwa timu za mazishi—yanatokana na kutokuaminiana kwa jamii na taarifa potofu zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii. Matukio hayo yamekwamisha:

  • Uchunguzi wa Ebola — Kuchelewesha kuwafikia watu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi
  • Ufuatiliaji wa waliokutana na wagonjwa — Kupunguza uwezo wa kufuatilia watu walio katika hatari kubwa
  • Upatikanaji wa huduma za afya — Timu kushindwa kuingia kwa usalama katika baadhi ya jamii

Dkt. Belizaire ameonya kuwa upinzani huo “unaongeza kwa kiasi kikubwa hatari ya maambukizi ya ugonjwa” na kudhoofisha imani kwa wahudumu wa afya.

Licha ya changamoto hizo za kiusalama  timu za afya za shirika hilo zimeendelea kufanya kazi kwa karibu na wahudumu wa afya wa kijamii.

Mwitikio mpana wa WHO: Kupeleka huduma karibu na jamii

Ili kuimarisha imani na kupunguza upinzani, WHO inapeleka maabara tembezi kwa ajili ya uchunguzi wa haraka na kusaidia vitengo vya kutenga wagonjwa na vituo vya matibabu katika maeneo yaliyoathirika.

Halikadhalika amesema, WHO inaimarisha ufuatiliaji wa mipaka ya DRC na Uganda pamoja na Sudan Kusini.

Hatua nyingine ni kushirikiana na viongozi wa jadi na waganga wa kienyeji ili kuboresha kukubalika kwa hatua za afya sambamba na kuwafundisha wahudumu wa afya wa jamii ili wakazi waone sura wanazoziamini na kuzifahamu

Dkt. Belizaire amebainisha kuwa kugundua ugonjwa mapema huongeza sana nafasi ya kupona—hadi asilimia 95 ikiwa wagonjwa watatafuta huduma siku ya kwanza ya dalili, kulingana na milipuko ya awali.

Wito wa ushirikiano wa jamii

Akitamatisha mahojiano, Dkt. Belizaire ametoa ujumbe kwa wananchi wa DRC akisema, “mlipuko huu ni mkubwa, lakini si wa kukata tamaa. Tunahitaji ushirikiano wa jamii… ili kulinda maisha yao. Mafanikio ya mwitikio sasa hayategemei tu uwezo wa kitabibu bali pia imani ya jamii, mawasiliano ya wazi, na uwajibikaji wa pamoja.”

Idadi ya wanaoshukiwa kuwa na virusi vya Ebola

Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema idadi ya wanaoshukiwa kuwa na Ebola ya virusi vya Bundibugyo ni zaidi ya 900 na kati yao hao watu 200 wamepoteza maisha.

Akizungumza leo Jumatatu kwenye mkutano wa Mawaziri uliofanyika kwa njia ya mtandao  kuhusu Mlipuko wa Ebola ya virusi vya Bundibugyo ulioandaliwa na Kituo cha Afrika cha uchunguzi wa magonjwa, Africa CDC, Dkt. Tedros amesema mlipuko wa mlipuko wa sasa ulioanzia DRC na kuripotiwa pia Uganda unaenea kwa kasi zaidi kuliko wahudumu wa afya wanavyoweza kuudhibiti.

Katika DRC, kitovu cha mlipuko huo, WHO imepandisha tathmini yake ya hatari ya kitaifa kutoka kiwango cha juu hadi cha juu sana, na nchi jirani – ikiwemo Uganda, ambapo wagonjwa watano wameripoti wa kifo kimoja vimethibitishwa – ziko katika hatari kubwa zaidi.

Maeneo yapi yenye Ebola DRC

Hadi Jumapili ya Mei 24, Ebola imeripotiwa katika jimbo la Ituri, hasa kwenye kanda za afya za Bunia, Mongbwalu, Nyakunde, Nizi na Rwampara.

Halikadhalika katika jimbo la Kivu Kaskazini kwenye kanda ya afya ya Butembo, Katwa na Goma, na pia katika jimbo la Kivu Kusini kwenye kanda ya afya ya Miti-Murhesa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *