
Arusha. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali za Afrika katika kuandaa na kutekeleza mipango ya maendeleo ya vijana kwa lengo la kukabiliana na changamoto zinazowakabili, pamoja na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya uchumi.
Nanauka amesema changamoto zinazowakabili vijana hazipo Tanzania pekee bali zinagusa mataifa mengi ya Afrika, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa pamoja katika kutafuta suluhisho la kudumu.
Waziri huyo ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 25, 2026 wakati akizungumza katika jukwaa la tisa wa vijana (You Lead 2026) linalowakutanisha viongozi vijana, watunga sera, wabunifu, watendaji wa asasi za kiraia pamoja na wadau wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Waziri huyo amesema wadau hao wamepata nafasi ya kusikiliza na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu vijana.
Amesema kongamano hilo limejikita katika kujadili namna ya kufikia maendeleo endelevu kwa kujenga msingi wa amani, haki pamoja na ustahimilivu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
“Serikali tumeeleza dhamira yetu na namna tunavyotambua kuwa changamoto za vijana zipo katika mataifa mengi ya Afrika, hivyo tutaendelea kushirikiana na nchi jirani pamoja na mataifa mengine kupanga na kutekeleza mipango inayowahusu vijana,” amesema.
Nanauka amesema Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maendeleo ya Vijana iliyoundwa mahususi kwa ajili ya vijana imeendelea kuhakikisha kundi hilo linashiriki kikamilifu katika maendeleo badala ya kuwa watazamaji.
Amesema wizara hiyo imeanzisha jukwaa maalumu lijulikanalo kama ‘Vijana Platform’ linalowahusisha vijana katika kutoa maoni, kushiriki mijadala ya maendeleo na kupata taarifa kuhusu fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.
Amesema Serikali imeendelea kutengeneza fursa kupitia miradi ya kimkakati pamoja na programu mbalimbali zinazolenga kuongeza ajira, utoaji wa mitaji na kuongeza ujuzi wa vijana kwa kushirikiana na sekta binafsi.
“Tuna mipango ya miaka mitano inayolenga kukuza uchumi jumuishi na kuongeza ajira zaidi kwa vijana. Pia tunawaelekeza vijana kushiriki kwenye sekta zinazokuwa kwa kasi nchini ili wawe sehemu ya ukuaji wa uchumi wetu,” amesema.
Kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, amesema imeweka mkazo mkubwa katika matumizi ya teknolojia na uchumi wa kidijitali ambapo lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka huo asilimia 80 ya huduma za Serikali zinatolewa kwa njia ya mtandao.
Amesema hali hiyo ni fursa kubwa kwa vijana kwani itahitaji uwepo wa miundombinu ya kidijitali pamoja na wataalamu wenye ujuzi wa kisasa katika maeneo ya akili mnemba (Artificial Intelligence), biashara mtandao (e-commerce) na teknolojia nyingine bunifu.
“Ndiyo maana Serikali inaendelea kubadili sera mbalimbali ambazo zinaweza kuwa vikwazo kwa vijana kushiriki katika uchumi wa kidijitali huku tukiongeza uwekezaji katika kuwajengea ujuzi wa kisasa,” amesema.
Akizungumzia suala la amani na haki, Nanauka amesema amani siyo tu kutokuwepo kwa vurugu bali ni pamoja na uwepo wa mifumo inayowajumuisha watu wote bila ubaguzi na kuhakikisha sauti zao zinasikilizwa.
“Amani inahusisha watu kupata haki wanapohitaji na kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi kila siku. Tunataka utulivu tulioupata utusaidie kujenga mifumo bora inayogusa maisha ya wananchi wote ili kila mmoja ajione ni sehemu ya mustakabali wa Taifa letu,” amesema.
Aliwataka vijana kuwa sehemu ya kujenga Taifa badala ya kubomoa, akieleza kuwa mustakabali wa taifa unawahusu zaidi vijana kwa kuwa ndio watakaoishi kwa muda mrefu zaidi katika mazingira yanayojengwa sasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC), Dk Anna Haule amesema kongamano hilo ni kuhakikisha kila kijana katika Afrika Mashariki anakuwa na sauti na muhimu kuhakikisha vijana wanapata sehemu salama ya kuzungumza kuhusu ujasiriamali, biashara na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema tangu kuanzishwa kwa jukwaa la YouLead mwaka 2017 jijini Arusha, limeendelea kukua na kuwa jukwaa linalowaunganisha viongozi vijana kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kujenga ushirikiano na kuimarisha uwezo wao wa uongozi.
