Vimelea vya malaria vyaonesha usugu wa dawa mikoa mitanoVimelea vya malaria vyaonesha usugu wa dawa mikoa mitano

Dar es Salaam. Matokeo ya utafiti wa ufuatiliaji ugonjwa wa malaria kwa kutumia vinasaba, umebaini vimelea vya ugonjwa huo vimeanza kupata usugu wa dawa hasa katika mikoa mitano nchini.

Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) umeonesha mkoa ulioathirika zaidi na usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni Kagera na kusambaa katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Ruvuma na mikoa ya Njombe na Morogoro.

Akizungumza leo Jumatatu, Mei 25, 2026 kwenye hafla ya uwasilishaji wa utafiti kupitia mradi ufuatiliaji ugonjwa wa malaria kwa kutumia vinasaba, Mtafiti Mkuu Taasisi ya Ifakara Dk Deusdedith Ishengoma amesema utafiti huo umefanyika 2024.

Amesema wakati wa matibabu ya ugonjwa wa malaria, mgonjwa alipatiwa dawa na mategemeo baada ya siku tatu apone, lakini walibaini hata baada ya zaidi ya siku hizo mgonjwa bado alikuwa na vimelea mwilini.

“Tupo kwenye hatari vimelea tulivyonavyo vinaanza kupata usugu, vinakuwa sugu dhidi ya dawa tunazozitumia na maeneo yaliyoathirika sana ni Mkoa wa Kagera, ndani ya miaka mitatu hii vimelea vinasambaa kwenda Kigoma, Katavi, Ruvuma na vikismabaa kwenda mikoa ya Njombe na Morogoro,” amesema.

Dk Ishengoma amesema ni muhimu Wizara ya Afya kuongeza nguvu kufuatilia malaria, akipendekeza maeneo yaliyoathirika kuwe na mabadiliko ya dawa za kutibu ugonjwa huo ili kukabiliana na usugu.

Amesema sababu ya usugu huo ni vimelea vyenyewe kujibadilisha kukabiliana na dawa, sababu nyingine ni matumizi yasiyo sahihi ya dawa za malaria.

Washiriki mbalimbali wakifuatilia uwasilishaji wa utafiti wa malaria jijini Dar es Salaam uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Afya ya Ifakara.

Akizungumzia mradi wa kufuatilia malaria kupitia vinasaba, Dk Ishengoma amesema umejikita kuangalia aina za vimelea vya malaria vinavyopatikana nchini na kama vina usugu dhidi ya dawa za malaria.

“Pia, mradi umejikita kuangalia uwezekano wa vimelea vya malaria kama vitaonekana kupitia vitendanishi na vipimo vya papo kwa hapo na kwa mara ya kwanza tumebaini vimelea vinavyopatikana nchini.

“Kwa sasa kila mkoa tunafahamu aina ya vimelea vilivyopo nchini na aina ya vipimo vinavyohitajika ili kuwabaini, kwahiyo kwa mara ya kwanza vipimo vyetu tumeviona vina ubora mkubwa,” amesema.

Akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Profesa Said Aboud amesema mapendekezo yote yaliyowasilishwa kupitia utafiti huo Serikali imeyapokea na inathamini.

Amesema matokeo hayo ni muhimu na Serikali hutumia matokeo ya utafiti kama ushahidi pale inapofanya uamuzi wowote katika sekta ya afya.

“Tuna maendeleo makubwa kwenye utambuzi wa malaria na magonjwa mengine, mradi huu wa kutambua malaria kwa njia ya vinasaba umetekelezwa katika mikoa yote na na umesaidia kujenga uwezo kwa wataalamu wetu,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Ifakara Honorati Masanja, amesema mradi huo wa awamu ya pili umeanza kutekelezwa tangu 2024.

“Kiwango cha malaria nchini ni asilimia nane na ni maendeleo makubwa, kwani tulikuwa na asilimia 18, yapo maeneo mengine ambayo yana maambukizi zaidi ya malaria,”amesema.

Amesema ufuatiliaji wa malaria kwa njia ya vinasaba ni mbinu mpya na kupitia utekelezaji wa mradi huo wataalamu wa afya waliopo nchini wanajengewa uwezo.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) Afya Profesa Tumaini Nagu ambaye aliwakilishwa, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa afya, taasisi za utafiti na sekta ya elimu kuhakikisha tafiti zinazohusu malaria zinatumika kuboresha huduma za afya na kuimarisha mikakati ya kutokomeza ugonjwa huo nchini.

Profesa Nagu amesisitiza umuhimu wa kutumia kwa wakati matokeo ya tafiti katika kuboresha miongozo ya utekelezaji, sera na kimkakati ya kudhibiti malaria nchini.

“Tanzania bado inahitaji kuongeza juhudi ili kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030, tafiti hizi zinatupa mwanga wa kujua tulipo, zinatusaidia kuboresha afua tunazotekeleza,” amesema.

Amesema Serikali inathamini mchango wa wadau wote na itaendelea kuimarisha ushirikiano ili kutokomeza malaria nchini.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2024 zinaonesha uwepo wa kesi  za malaria milioni 282 na vifo 610,000 katika mataifa 80 duniani kwa mwaka.

WHO inaonesha kuwa mwaka huo asilimia 95(milioni 265) ya kesi za malaria ni kutoka mataifa ya Afrika na asilimia 95 (579,000) ni vifo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *