
Dar es Salaam. Wakili wa utetezi katika kesi ya wizi wa dawa na vifaa tiba inayowakabili watumishi sita wa Bohari ya Dawa (MSD), Seif Rashid ameutaka upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi kwa wakati ili iweze kuandelea na hatua nyingine.
Pia, ameiomba Mahakama itoe hati ya wito wa kuwapeleka washtakiwa mahakamani kutoka rumande, kwa sababu kesi hiyo imeahirishwa mara tatu bila washtakiwa hao kupelekwa mahakamani.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 7833 ni Mhasibu Mwandamizi, Suddi Abas (34), mkazi wa Kibamba Shule.
Wengine ambao wote ni wafamasia ni Petro Mdegela (42), mkazi wa Manga Veta; Rashid Hassan (34) na mkazi wa Isyesye.
Pia yupo, Edward Tengulaga(40) mkazi wa Manga Veta; Mfamasia wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Jackson Mahagi(39) na Wema Mohamed(39) ambaye ni mfamasia wa wilaya ya Singida na mkazi wa Mandewa.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 37 yakiwamo ya wizi wa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh5.537 bilioni na kuisababishia MSD hasara ya Sh14.6 bilioni.
Rashid ametoa ombi hilo leo Jumatatu Mei 25, 2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa kutajwa.
Wakili huyo ameieleza Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya anasikiliza kesi hiyo.
“Tuomba wenzetu upande wa Jamhuri wajitahidi kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hii iweze kuendelea na hatua nyingine za kisheria,” amedai na kuongeza.
“Mheshimiwa hakimu, hii ni mara ya tatu kama sijakosea tangu washtakiwa waliposomewa mashtaka yao na kupelekwa rumande, hawajawahi kuleta hapa mahakamani kwako kwa ajili ya kujua mwenendo wa kesi yao, hiyo tunaomba tarehe ijayo, waletwe mahakamani,” amedai wakili Rashid ambaye maombi yake wawili yaliungwa mkono na mawakili wenzake.
Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Monica Ndekidemi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Akijibu hoja ya kukamilisha upelelezi kwa wakati, wakili Ndekidemi amedai kuwa ombi hilo wamelichukia na wanalifanyika kazi na upelelezi utakapokamilika watatoa taarifa mahakamani hapo.
Kuhusu washtakiwa kupelekwa mahakamani wakitoka rumande, wakili Ndekidemi amedai kuwa jambo hilo lipo chini na Mahakama na sio upande wa mashtaka.
Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 8, 2026 kwa kutajwa na ametoa hati ya wito kwa washtakiwa hao kupelekwa Mahakamani wakitoka rumande.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Aprili 13, 2026 na kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Kati ya mashtaka 37 yanayowakabili washtakiwa hao, mashtaka 31 ni ya kutakatisha fedha; matatu ni ya wizi wakiwa watumishi; mawili ni kuisababishia mamlaka hasara na moja ni kuongoza genge ma uhalifu.
Miongoni mwa mashtaka hayo, ni kuongoza genge, linalowakabili washtakiwa wote ambapo wanadaiwa kati ya Julai mosi, 2021 na Juni 30, 2025 katika maeneo tofauti ya a Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Dodoma, Singida na maeneo mengi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu kwa kutenda kosa la wizi wakiwa watumishi.
Shtaka la pili ni wizi wakiwa watumishi, linalomkabili Abas, Mdegela, Hassan na Tengulaga, ambapo wanadaiwa kati ya Julai mosi, 2021 na Juni 30, 2025 katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam na Mbeya, wakiwa watumushi kwa vyeo vyao, wanadaiwa kuiba dawa na vifaa tiba vya Sh2.695bilioni, mali ya MSD, iliyofika mikononi mwao wakiwa waajiriwa.
Shtaka la tatu ni wizi linalowakabili Mshtakiwa Abasi, Mdegela, Hassan na Mahagi, siku na maeneo hayo, washtakiwa wanadaiwa kuiba Sh2.592bilioni, mali ya MSD iliyofika mikononi mwao wakiwa waajiriwa.
Shtaka la nne ni wizi wakiwa watumishi wa MSD linalomkabili Abas na Mohamed, ambapo wanadaiwa kati ya Januari 1, 2023 na Juni 30, 2025 katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam, Dodoma na Singida, kwa pamoja wanadaiwa kuiba Sh250milioni, mali ya MSD.
Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo, kuwa shtaka la tano ni kuisababishia mamlaka hasara, shtaka linalomkabili Abas pekee yake, anadaiwa kati ya Julai mosi, 2021 na Juni 30, 2025 katika ofisi za MSD zilizopo Keko, Wilaya ya Temeke, mshtakiwa kwa makusudi aliisababishia MSD hasara ya Sh9.1bilioni.
Shtaka la sita ni kuisababishia mamlaka hiyo hasara linalowakabili washtakiwa wote, katika kipindi hicho na katika mikoa hiyo, washtakiwa waliisababishia MSD hasara ya Sh5.537bilioni.
Shtaka la saba ni kutakatisha fedha, linalowakabili washtakiwa wote, katika kipindi hicho, wanadaiwa kutakatisha Sh5,537 bilioni huku wakijua kuwa shtaka hilo ni kosa tangulizi la wizi akiwa mwajiriwa.
