Nusu fainali AFCON U-17 utamu upo hapa kwa Serengeti BoysNusu fainali AFCON U-17 utamu upo hapa kwa Serengeti Boys

Dar es Salaam. Mechi za Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON U-17), zinaendelea kuchezwa nchini Morocco ambapo vijana wa Tanzania, Serengeti Boys wamefuzu kwa mara kucheza nusu fainali ambapo wataikabili Misri, huku wenyeji Morocco wakijiandaa kuvaana na mabingwa watetezi, Senegal katika pambano lenye mvuto mkubwa.

Nusu fainali zote mbili zitachezwa Mei 29, 2026 kwenye Uwanja wa Moulay El Hassan mjini Rabat. Serengeti Boys itaanza kwa kuivaa Misri kabla ya Morocco kukutana na Senegal katika mchezo unaobeba historia, presha na kisasi cha muda mrefu.

Serengeti Boys ilionyesha moyo wa kupambana, ujasiri na uwezo mkubwa wa kushambulia katika sare ya mabao 3-3 dhidi ya Algeria kwenye robo fainali, kabla ya kushinda kwa penalti 4-3.

Mara mbili Serengeti Boys ilitoka nyuma kusawazisha, ikionesha utulivu mkubwa, sifa ambazo watahitaji tena watakapokutana na Misri, timu iliyo katika kiwango bora.

SERE 01

Misri iliingia nusu fainali baada ya kuifunga Misri mabao 4-1 katika robo fainali. Vijana hao wa Mafarao walionekana kuwa makini, wenye nidhamu ya kiuchezaji na hatari kwenye mashambulizi ya kushtukiza, huku Khaled Mokhtar akifunga mabao mawili kabla ya mapumziko.

Licha ya Misri kuonekana kuwa miongoni mwa timu zinazowania ubingwa, uwezo wa Serengeti Boys katika kushambulia kwa ujasiri na kupambana hadi dakika ya mwisho unaonyesha kuwa wanaweza kufanya tena maajabu.

Kwa Serengeti Boys, kufika nusu fainali tayari ni mafanikio makubwa, lakini sasa timu hiyo iko hatua moja tu kutoka kufuzu fainali yao ya kwanza kabisa ya AFCON U-17. Hata hivyo, macho ya wengi yataelekezwa kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali kati ya Morocco na Senegal, pambano lililofunikwa na kumbukumbu za moja ya matukio yenye utata mkubwa katika historia ya hivi karibuni ya soka la Afrika.

Timu hizi mbili kwa wakubwa zilikutana kwenye fainali ya AFCON 2025 iliyochezwa Rabat Januari 18, 2026. Senegal walishinda mchezo huo kwa bao 1-0 baada ya Pape Gueye kutikisa nyavu muda wa nyongeza na kuwapa taji lao la pili la Afrika.

SERE 02

Lakini mchezo huo uliingia kwenye vurugu mwishoni mwa muda wa kawaida baada ya Morocco kupewa penalti iliyobeba utata mkubwa. Wachezaji wa Senegal waliondoka uwanjani kwa hasira wakipinga uamuzi huo na walikaa nje kwa takribani dakika 17 kabla ya kurejea baada ya mazungumzo na waamuzi. Morocco walikosa nafasi ya kufunga baada ya kipa wa Senegal, Edouard Mendy, kuokoa penalti hiyo na kufanya mchezo uendelee hadi muda wa nyongeza ambapo Senegal walipata bao la ushindi. Hata hivyo, sakata hilo halikuishia hapo.

Baada ya rufaa kutoka kwa Shirikisho la Soka la Morocco, Kamati ya Rufaa ya CAF iliamua kuwa Senegal walikiuka kanuni za mashindano kwa kutoka nje ya uwanja bila ruhusa ya mwamuzi. Machi 2026, CAF ilibatilisha matokeo hayo na kuipa Morocco ushindi wa mezani wa mabao 3-0, hivyo kuwataja rasmi kuwa mabingwa wa Afrika 2025. Uamuzi huo ulizua mjadala mkubwa barani Afrika, huku wengi wakigawanyika kuhusu kama sheria za mashindano zinapaswa kupewa uzito kuliko matokeo ya uwanjani. Shirikisho la Soka la Senegal lilikataa uamuzi huo na kupeleka kesi katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), ambapo bado inaendelea.

Sasa Morocco na Senegal wanakutana tena, safari hii katika timu za vijana U-17, ikiwa ni pambano ambalo si tu la kuwania nafasi ya fainali bali pia linaongeza sura mpya katika ushindani mkali unaoendelea kuvutia mashabiki wa soka Afrika nzima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *