
Dodoma. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania imesema bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo amezitaja baadhi ya changamoto ni kwa nchi wanachama katika jumuiya za kikanda kutoheshimu baadhi ya Mikataba na Makubaliano ikiwemo kutolipa michango yao ya kibajeti kwa wakati.
“Hatua hii inaathiri uratibu na ushiriki wetu katika utekelezaji wa Programu za Mtangamano wa Kikanda,”amesema Balozi Kombo.
Amebainisha hayo leo Jumanne, Mei 26, 2026 wakati akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2026/27 Sh359.3 bilioni. Kati ya fedha hizo, Sh312.9 bilioni zitatumika kwenye matumizi ya kawaida huku Sh46.3 bilioni zikipelekwa kwenye miradi ya maendeleo.
Waziri amesema baadhi ya wadau ikiwemo sekta binafsi hawachangamkii ipasavyo fursa zitokanazo na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kupitia ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa.
Ametaja baadhi ya wafanyabiashara hawana uwezo wa kusambaza bidhaa kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa wakati wote huku baadhi ya bidhaa zikikosa ubora unaotakiwa na zinazokidhi viwango vya masoko ya kimataifa.
“Kingine ni kuzorota kwa hali ya amani na usalama katika baadhi ya nchi ndani na nje ya ukanda wa Afrika na hivyo kuathiri utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024,” amesema Kombo.
Ametaja changamoto nyingine ni mabadiliko ya mwelekeo wa hali ya kisera na mvutano katika siasa za kidunia.
Amesema hali hii imesababisha kutotabirika kwa mwelekeo wa sera katika uhusiano wa kimataifa na kasi ndogo ya kuridhia na kutekeleza Makubaliano ya uwili, kikanda na kimataifa hivyo kusababisha kuchelewa kufanikisha malengo ya makubaliano.
