UCHAMBUZI WA MJEMA: Tunatamani maridhiano, kauli na matendo yetu vinatusalitiUCHAMBUZI WA MJEMA: Tunatamani maridhiano, kauli na matendo yetu vinatusaliti

Siyo jambo la siri; Watanzania wanajua na dunia inajua nchi yetu iko katika mkwamo wa kisiasa na kijamii kutokana na matukio ya kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, na tiba pekee ya kutibu majeraha ni maridhiano.

Lakini kuna kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wetu wa kisiasa, wakiwamo wa Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), zinazodhihirisha kuwa hakuna utashi wa kisiasa wa kufikia maridhiano, jambo ambalo ni la hatari sana.

Kwa takwimu za ripoti ya Tume ya Kuchunguza Ghasia za Oktoba 29 iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, imetueleza kuwa Watanzania 518 walipoteza maisha, na hiyo siyo takwimu ya mwisho au “inconclusive data”.

Kati ya watu 518 waliofariki dunia, 373 walifikishwa hospitalini wakiwa wamefariki, na majeruhi 121 walifariki wakati wakipatiwa matibabu. Lakini hadi leo kuna ndugu wanaodai miili ya ndugu zao; hawajui waweke msiba au waanue tanga.

Wengine walienda mbali na kuamua kuzika nguo za wapendwa wao. Jambo hili linaumiza mioyo ya wengi, hasa ikizingatiwa kuwa kwa mila na tamaduni zetu, simanzi za msiba hudumu hadi siku ya mazishi ndipo watu hurudi katika hali ya kawaida.

Lakini katika mazingira ya kutopata fursa ya kuwazika wapendwa wao, jambo hilo haliwezi kufutika kamwe katika mioyo na kumbukumbu zao, na litadumu milele. Tupende tusipende, ni ukweli tu ndio utakaotuweka huru.

Tathmini ya Tume inaonyesha kuwa hadi tarehe 31 Machi 2026, majeruhi waliokuwa wamehudumiwa katika vituo vya umma na binafsi vya kutolea huduma za afya kutokana na ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu walikuwa 2,390.

Nimejaribu kuonyesha takwimu hizo, japo kama nilivyotangulia kusema, siyo “conclusive” (siyo za mwisho), kwa sababu wako waathirika waliogoma kuipa Tume ushirikiano wakidai siyo huru, ili kuonyesha majaribu ambayo Tanzania imepitia.

Lakini kwa nini tulifika hapo? Tume ya Jaji Chande iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ilianisha kiini, chimbuko au mzizi wa tatizo lililotufikisha katika vurugu na ghasia za Oktoba 29 zilizogharimu maisha ya wapendwa wetu.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Tume hiyo iliyokabidhi ripoti kwa Rais Aprili 23, 2026, ghasia za wakati na baada ya uchaguzi zilitokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwepo katika jamii kwa muda mrefu bila kutatuliwa.

Miongoni mwa changamoto hizo ni madai ya Katiba Mpya, demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, malalamiko ndani ya vyama vya siasa, madai ya maboresho ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, na mfumo mzima wa uchaguzi.

Zingine ni masuala ya kiuchumi yanayojumuisha ugumu wa maisha, kukosekana kwa usawa katika fursa za ajira na za kiuchumi, mazingira ya biashara na uwekezaji yasiyo rafiki, utitiri wa kodi na tozo, na mfumo usio rafiki wa kodi.

Tume ikataja changamoto nyingine kuwa ni masuala ya kijamii yanayojumuisha mmomonyoko wa maadili na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, na madai ya utekaji, mauaji, na kupotea au kupotezwa kwa watu hapa Tanzania.

Sasa badala ya kushughulika na kiini cha tatizo, baadhi ya viongozi wa kisiasa wanatoa kauli ambazo ni kama wanafanya mzaha kwa changamoto hizo, hasa suala la wimbi la utekaji lililoshika kasi, na kudai ni “michezo tu” ya kuichafua Serikali.

Ni muhimu sana viongozi wetu wakapima kauli zao kabla ya kuzitoa, na ikibidi wajizuie kufanya propaganda katika mambo mazito kama utekaji, ukiukwaji wa haki za binadamu, na ghasia za Oktoba 29 zilizoacha majeraha makubwa.

Taifa hivi sasa linahitaji kauli za kufariji na kuponya majeraha, na siyo kutonesha vidonda wakati tukiwa katika hatua za mwanzo za kusaka maridhiano. Hili taifa ni letu sote; likiparaganyika, wengine hatuna pa kukimbilia.

Halafu viongozi wetu wasiongee na Watanzania kama wanaongea na watoto wadogo wasio na uelewa wa mambo. Watanzania wa leo wameelimika; wanajua mchele ni upi na chuya ni zipi, na wanajua propaganda za kisiasa zinafananaje.

Sasa leo unapomsikia kiongozi anasema tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, ambaye sasa ni mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Septemba 7, 2017, ulikuwa ni “mchezo” ili kuichafua Serikali, napata kizunguzungu.

Ama akisema msaidizi yule wa Lissu aliyetekwa na kundi la watu wenye silaha na kupatikana siku iliyofuata akiwa na majeraha huku amefungwa pingu, kwamba alitekwa na wenzake katika siasa, unashindwa kuelewa dhamira yake ni nini.

Ukiacha hilo, vyombo vyetu kutoa sababu za watu kutekwa kuwa ni mapenzi, visasi, na madeni, unashindwa kuelewa kwa nini wanaendelea kumwagia petroli katika moto unaowaka au kuzima moto wa petroli kwa kutumia maji.

Jaji Chande ametoa kiini au chimbuko la ghasia zile za Oktoba 29, na ni pamoja na Watanzania kuchoshwa na wimbi la utekaji. Lakini leo kuambiwa watu wanajiteka tena, kwa sehemu kubwa ni wa upande mmoja, ni jambo linalofedhehesha.

Ndiyo maana nimetangulia kusema tunahubiri maridhiano, lakini kwa kauli na matendo ya viongozi wetu ni kama vinasaliti dhamira yao hiyo, kwa sababu hiki ni kipindi ambacho Watanzania wanatamani kusikia kauli za kufariji na kuponya majeraha.

Kauli za kushupaza shingo na propaganda hazitatuacha salama. Tunazidi kuchochea kuni kwenye moto unaowaka; madhara yake tutayaona siku si nyingi kama tutaendelea na mwendo huu.

Niwasihi Watanzania wenzangu, puuzeni kauli zozote zenye lengo la kudhoofisha dhamira njema ya Rais Samia ya kutafuta maridhiano, kwa sababu nyinyi mnaufahamu ukweli wa nini kilitokea Oktoba 29 na siku zilizofuata.

Kudhihaki matukio ya utekaji ni kusaka maridhiano tukiwa tumeficha mapanga nyuma. Nawaambia, hatutatoboa; tuonyeshe dhamira ya kweli ya maridhiano. Ukweli usemwe ili utuweke huru, tusahau yaliyopita na tugange yajayo.

Kama Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, alivyowahi kusema, tusitatue matatizo yetu kwa kujifanya hayapo. Basi tusifanye mzaha au kutumia changamoto za utekaji kufanya propaganda za kisiasa; huko tuendako kutakuwa na giza nene.

Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *