
Angalau KMC itaenda katika mapumziko ya siku 16 ikiwa haijashuka daraja baada ya leo, Jumanne, Mei 26, 2016, Singida Black Stars kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Airtel, Singida.
Kama Mbeya City ingepata ushindi katika mechi ya leo, ingefikisha pointi 25 ambazo zingefanya KMC ishuke rasmi daraja kwa vile isingeweza kuzifikia.
Ikiwa imebakiza michezo mitano ya ligi, KMC inayoshika mkia na pointi zake tisa, inaweza kufikisha pointi 24 tu kama itapata ushindi katika mechi hizo zote zilizobakia.
Mabao manne ya Singida Black Stars ambayo yameichelewesha KMC kushuka daraja, katika mchezo wa leo yamefungwa na Ande Koffi, Horso Muaku, Khalid Aucho na Mossi Ndumumwe.
Bao pekee la kufutia machozi la Mbeya City katika mechi hiyo ni la kujifunga la kiungo wa Singida Black Stars, Morice Chukwu.
Matokeo ya leo yameifanya Singida Black Stars kupanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 41.
Mbeya City imebaki katika nafasi ya 14 ikiwa na pointi zake 22.
Kwingineko katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Maafande wa Tanzania Prisons wamefufua matumaini yao ya kubaki Ligi Kuu baada ya kupata ushindi wa mabao 3-2, dhidi ya wenyeji wao Pamba Jiji FC.
Ushindi huo licha ya kuifanya Tanzania Prisons kufikisha pointi 20, haujaisaidia kuiondoa katika nafasi ya 15 ilipokuwepo kabla ya mchezo huo.
Pamba Jiji imebaki katika nafasi ya saba na pointi 33.
Mabao ya Tanzania Prisons leo yamefungwa na Haruna Chanongo, George Mpole na Oscar Mwajanga huku ya Pamba Jiji yakipachikwa na Mathew Tegis.
