Wimbo maalumu waachiwa kuadhimisha Siku ya Hedhi DunianiWimbo maalumu waachiwa kuadhimisha Siku ya Hedhi Duniani

Dar es Salaam. Katika kuadhimisha Siku ya Hedhi Salama Duniani, Shirika la Rafiki wa Binti limezindua wimbo maalumu ukilenga kutoa elimu kwa wasichana kuhusu afya ya hedhi.

Siku ya hedhi duniani huadhimishwa kila mwaka Mei 28. Maadhimisho hayo yanalenga kuongeza uelewa kuhusu afya ya hedhi, kupinga unyanyapaa unaohusiana na hedhi, na kuhamasisha upatikanaji wa huduma na vifaa salama vya hedhi kwa wanawake na wasichana duniani kote.

Wimbo huo wa uhamasishaji umeandikwa na kuimbwa na msanii maarufu wa Tanzania, Ashura Kitenge, ukiwa na lengo la kutoa elimu hiyo muhimu kwa afya ya wasichana kwa njia ya sanaa ya muziki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Mei 26, 2026 na Rafiki wa Binti, wimbo huo ni sehemu ya mpango mpana wa elimu ya afya ya hedhi unaowafundisha wasichana namna ya kutumia, kufua na kuhifadhi pedi maalum za kufua  zinazoweza kutumika kwa muda mrefu.

Shirika hilo limesema matumizi ya pedi hizo maalum za kufua bado ni jambo jipya katika jamii nyingi za Tanzania, lakini yamekuwa suluhisho muhimu la kusaidia wasichana kujisitiri wakati wa hedhi na kupunguza unyanyapaa unaohusishwa na suala hilo.

Kupitia mpango wake wa “Binti Packs”, Rafiki wa Binti tayari imetoa zaidi ya jozi 24,000 za pedi hizo maalumu kwa wanafunzi wa kike katika maeneo ya Mafinga, Kilwa Masoko, Mkoa wa Kagera na Zanzibar.

Imeelezwa pedi hizo zinaweza kutumika kwa zaidi ya miaka miwili, hatua inayolenga kupunguza gharama kwa familia na kuongeza upatikanaji wa vifaa salama vya hedhi kwa wasichana wa shule.

Kila kifurushi cha “Binti Pack” kina jozi sita za chupi zinazotumika tena, elimu ya afya ya hedhi pamoja na mifuko ya kuhifadhia chupi kavu na zenye unyevunyevu.

Aidha, shirika hilo limetangaza kuwa linatarajia kugawa jozi nyingine 24,000 katika miezi ijayo kadri linavyoendelea kupanua huduma zake katika maeneo mbalimbali nchini.

Mmoja wa viongozi wa mpango huo, Nancy Bondo, amesema afya ya hedhi ni suala la elimu na fursa kwa wasichana.

“Maoni kutoka serikalini, kwa walimu na wanafunzi kuhusu mradi wa Binti yamekuwa mazuri sana. Mradi huu unawasaidia wasichana kuendelea kuhudhuria masomo wakati wa hedhi kwa heshima na kujiamini,” amesema Bondo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rafiki wa Binti ni mpango unaolenga kusaidia wasichana wa Tanzania kupitia elimu ya afya ya hedhi pamoja na ugawaji wa chupi zinazoweza kutumika tena ili kuwasaidia kubaki shuleni, kujiamini na kujengewa uwezo.

Mpango huo unasimamiwa na taasisi ya Rafiki Australia Tanzania, ambayo inaendeshwa kwa mfumo wa kujitolea nchini Australia na Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *