Utekaji, maridhiano vyawaibua wanawake wa vyama 12 vya siasaUtekaji, maridhiano vyawaibua wanawake wa vyama 12 vya siasa

Dar es Salaam. Matukio ya utekaji, ajenda ya maridhiano na amani ni miongoni mwa mambo matano yaliyowaibua wanawake wa vyama 12 rafiki vya siasa wakitaka suluhu na hatua stahiki kuchukuliwa.

Umoja huo wa wanawake umeeleza sintofahamu ya kuwepo kwa matukio ya utekaji na mauaji ni jambo linalopaswa kutazamwa kwa upana na kudhibitiwa kisheria ili kuondoa hofu kwa wananchi.

Vilevile wamegusia ajenda ya maridhiano kwa ajili ya kurejesha utulivu wa kisiasa wakiamini zinapotokea vurugu zozote ikiwamo za kisiasa waathirika wakubwa huwa ni wanawake na watoto.

Viongozi hao wametoa kauli hiyo leo Mei 26, 2026 walipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan katika suala la utekaji na mauaji kuunda Tume maalumu ya uchunguzi  ili wote watakaobainika kuhusika  wachukuliwe hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa Taifa wa wanawake wa NRA, Rachel Balama amesema matukio ya utekaji yameendelea kuibua hofu kubwa kwa jamii na kuhatarisha amani ya nchi.

Ameshauri kuimarishwa ulinzi na kuongeza intelejensia ili kuwatambua wahusika wa matukio hayo na kuchukuliwa hatua za kisheria, wakiomba Rais kuunda tume maalumu ya kuchunguza matukio hayo.

Baadhi ya wanawake viongozi wa Umoja wa wanawake wa vyama rafiki 12 vya siasa nchini.

Mbali na suala la utekaji, viongozi hao pia waligusia mjadala wa maridhiano ya kisiasa, ambayo kwa sasa ni moja ya ajenda za kitaifa na kuvishauri vyama vya siasa kuweka mbele maslahi ya taifa kwa kushiriki mazungumzo yatakayosaidia kuimarisha amani na mshikamano nchini.

Mwenyekiti wa wanawake wa AAFP, Shania Ali Kitumbua amesema baadhi ya vyama vinavyokataa maridhiano vinapaswa kutafakari upya msimamo wao kwa kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.

“Kuhusu suala la maridhiano, vyama vyetu vingi tuko tayari, wanaokataa maridhiano sijui wanawaza nini, tunaomba vyama vyote vikubali maridhiano ili nchi yetu iendelee kuwa na amani,” amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Taifa wa UMD, Mwajuma Mirambo amegusia suala la amani akibainisha Tanzania imeendelea kuwa na mazingira mazuri ya kisiasa chini ya uongozi wa Rais Samia kwani hivi sasa vyama vya siasa vinafanya mikutano yao kwa uhuru tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita.

Amesema ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha amani inaendelea kudumishwa kwa kuwa machafuko yanapoibuka wanawake na watoto huwa wa kwanza kuathirika.

“Tumeshuhudia sasa vyama vya siasa vikifanya mikutano kwa uhuru, ikiwemo kampeni za chaguzi ndogo, hivyo basi tusisahau kudumisha amani katika kipindi chote,” amesema Mwajuma.

Viongozi hao walionya kuwa kupotea kwa amani kunaweza kusababisha madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo kukosekana kwa ajira, kuongezeka kwa umasikini pamoja na njaa.

Katika mkutano huo, wanawake hao pia walimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto pamoja na kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri inawafikia walengwa wote bila upendeleo.

Wameshauri pia wasaidizi wa Rais kuhakikisha kile ambacho Rais alikiahidi kinatekelezeka ikiwamo huduma za afya bure kwa wajawazito, wazee na watoto, pamoja na utaratibu wa kuzuia maiti mochwari kwa sababu ya deni.

Wameshauri wasaidizi wa Rais kusimamia majukumu yao kwa uadilifu ili kuepusha vitendo vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wa majukumu ya serikali.

Umoja huo wa wanawake wa vyama rafiki vya siasa unaundwa na vyama 12 ambavyo ni SAU, NRA, DP, AAFP, UMD, NLD, UPDP, UDP, CCK, ADA-TADEA, MAKINI na TLP.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *