Waziri Mkuu aliyetenguliwa achaguliwa kuwa SpikaWaziri Mkuu aliyetenguliwa achaguliwa kuwa Spika

Bunge la Taifa la Senegal limemchagua waziri mkuu aliyeondolewa madarakani, Ousmane Sonko, kuwa spika wake.

Kuchaguliwa Sonko kuwa spika kumefanyika ndani tya siku nne baada ya Rais Bassirou Diomaye Faye kumfuta kazi, huku wabunge walio wachache bungeni wakidai kurejeshwa mwanasiasa huyo katika Bunge la Taifa kuwa kinyume cha sheria.

Sonko ni kiongozi wa Chama cha Pastef, ambacho kinashikilia viti 130 kati ya 165 katika chombo hicho cha kutunga sheria nchini Senegal.

Amepata kura 132 na alikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo, hivyo anachukua nafasi ya El Malick Ndiaye, mshirika wake aliyejiuzulu Jumapili, hatua iliyofungua njia kwa aliyekuwa waziri mkuu kupanda madarakani.

Kikao cha Bunge kilianza muda mfupi baada ya saa 3:00 asubuhi leo Jumanne Mei 26, 2026 na kuhudhuriwa na Sonko.

Kiongozi wa upinzani wenye wabunge wachache, Aissata Tall Sall amelaani hatua hiyo kumrejesha Sonko serikalini kwa kile alichokiita ni mapinduzi ya kitaasisi na kudai kwamba yaliandaliwa chini ya shinikizo.

Sall amesema anaamini kuwa Sonko, ili aweze tena kuwa mbunge, alipaswa kwanza kujiuzulu kama waziri mkuu ili akae hata kwa muda mfupi bungeni kabla ya kurejea serikalini.

Faye alimchagua Sonko kuwa waziri mkuu mwezi Aprili 2024 baada ya kushinda uchaguzi wa urais mwezi uliotangulia.

Awali Sonko, amewahi kuwa mshauri wa Faye katika masuala ya kisiasa.

Faye anakabiliwa na jukumu la kuongoza na kutekeleza mageuzi katika nchi inayokumbwa na changamoto kubwa za kiuchumi.

Jana Jumatatu, alimchagua mwanauchumi mwandamizi Ahmadou Al Aminou Mohamed Lo kuwa waziri mkuu, akisema mteule huyo mpya ana utaalamu wa kuiwezesha Senegal kujinasua kutoka changamoto za kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *