Kahama yasaini mkataba mpya umaliziaji barabara, onyo latolewaKahama yasaini mkataba mpya umaliziaji barabara, onyo latolewa

Kahama. Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imesaini mkataba wa umaliziaji wa ujenzi wa barabara ya mitaro ya maji, wenye zaidi ya Sh25.5 bilioni kupitia mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (Tactic).

Mkataba huo umesainiwa leo Jumatano Mei 27, 2026, kati ya Serikali na mkandarasi ‘China Civil Engineering Constraction Corporation’ baada ya mkandarasi ‘Sichuan Road and Brigde (Group) Corporation Limited’ wa awali kuvunjiwa mkataba Januari 2026.

Mkandarasi wa awali alikuwa akitekeleza mradi huo kwa gharama ya zaidi ya Sh20.8 bilioni, mpaka mkataba unavunjwa tayari alilipwa zaidi ya Sh 5.62 bilioni, ambapo ameshatekeleza shughuli zake kwa asilimia 30.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe ameonya wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza miradi kwa wakati huku akisisitiza Serikali haitavumilia uzembe unaokwamisha maendeleo ya wananchi.

Profesa Shemdoe amewataka wakandarasi waliopewa kazi kuhakikisha wanazingatia ubora, muda na thamani ya fedha za Serikali ili wananchi waanze kuona matokeo ya miradi inayotekelezwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya waziri mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe akishuhudia shughuli ya utiaji saini mkataba mpya wa ujenzi wa barabara na mifereji ya maji ya mvua katika manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga leo Mei 27,2026, kati ya serikali na mkandarasi China Civil Engineering Constraction Corporation kwa gharama ya zaidi ya Sh25.5 bilioni. Picha na Amina Mbwambo

“Kama mnavyojua mkandarasi wa awali Sichuan Road and Bridge (Group) Corporation Ltd, alishindwa kukamilisha kazi kwa wakati tukamsitishia mkataba, nawaonya wakandarasi, tusingependa hali ile ijirudie tena kwenu,” amesema.

“Sisi kama Serikali tutaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huu ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha za umma. Viongozi wa halmashauri kasimamieni, na mtoe ushirikiano kwa mkandarasi.”

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura), ni Mratibu wa Miradi ya kimkakati inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, Mhandisi Humphrey Kanyenye amesema mradi huo umegawanyika katika awamu mbili.

Amesema awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara za mijini katika eneo la katikati ya mji kilomita 12, barabara za eneo la Zongomera kilimita 4.4 pamoja na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 4.9.

Amesema Tarura kwa kushirikiana na serikali ya mkoa na wilaya, wataendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa ubora na ndani ya muda uliopangwa.

“Kazi zinazokwenda kutekelezwa ni ujenzi wa barabara za katikati ya Mji, barabara zinazozunguka eneo la Zongomela na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua inayopita kwenye maeneo hayo,” amesema.

Naye Mbunge wa Kahama Mjini (CCM), Benjamin Ngayiwa ameishukuru serikali kwa hatua hiyo iliyokuwa kikwazo kwa wakazi wa Kahama na wageni wanaoingia wilayani humo, huku akiwatoa hofu wananchi juu ya mradi huo.

“Tulipokuwa tukizunguka huku mjini, hata uongee jambo gani bado wananchi wanakuambia barabara, barabara, barabara. Hatuna barabara tunapigwa vumbi, wakati wa mvua mafuriko, tunaishukuru serikali kwa hili,” amesema.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya China Civil Engineering Constraction Corporation tawi la Tanzania, Wu Zegang amesema wanatarajia Serikali itatoa malipo ya awali kwa wakati ili kuanza rasmi kwa mradi huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya waziri mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mkataba mpya wa ujenzi wa barabara za Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga na mifereji ya maji ya mvua leo Mei 27,2026. Picha na Amina Mbwambo

“Tunajitoa kuhakikisha tunakamilisha mradi huu ndani ya muda wa mkataba na kwa ubora mzuri. Tunatarajia kupata malipo ya awali kwa wakati ili kuwezesha kuanza utekelezaji wa mradi huu muhimu kwa wananchi.”

Baadhi ya wakazi wa Kahama akiwemo dereva bajaji Andrea John amesema:“Kama sio siasa basi hii itasaidia uhai wa vyombo vyetu maana hizi barabara ni kila siku tuko gereji, inatuchosha.”

Naye Naftal Mussa dereva pikipiki (bodaboda) Kahama amesema:“Tunashukuru kama ni kweli tumeletewa mkandarasi wa huu mradi, kama inawezekana usimamiwe na serikali kuu kabisa, serikali iweke macho ya ziada Kahama, hili ni tatizo, vumbi, barabara hazikamiliki kila siku tunapangwa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *