Kauli za wabunge dhidi ya Bunge Marekani zawaibua wadauKauli za wabunge dhidi ya Bunge Marekani zawaibua wadau

Dar es Salaam. Mbinu ya Tanzania ya kusawazisha diplomasia yake na Marekani imeanza kuangaliwa kwa karibu zaidi kufuatia mijadala mikali bungeni kuhusu muswada wa Seneti ya Marekani, unaopendekeza kuiwekea nchi vikwazo kutokana na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu, unaohusishwa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Wachambuzi wa siasa wanasema ingawa utetezi mkali wa wabunge kuhusu uhuru wa Tanzania unaonyesha hisia za uzalendo, namna mjadala huo ulivyoendeshwa pia umeweka wazi changamoto nyeti inayoikabili diplomasia ya nchi katika kulinda hadhi yake kimataifa bila kuonekana kupuuza hoja zinazotolewa na washirika wa maendeleo.

Mjadala huo uliibuka bungeni Jumanne Mei 26, 2026 wakati wabunge wakijadili bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Sh359.3 bilionikwa mwaka wa fedha 2026/27.

Kiini cha mjadala huo kilikuwa ni muswada unaoitwa Reassessing the United States–Tanzania Bilateral Relationship Act, uliowasilishwa Mei 20 na Jeanne Shaheen na Ted Cruz.

Muswada huo unapendekeza kufanyika kwa tathmini upya ya uhusiano wa pande mbili kati ya Washington na Dar es Salaam pamoja na uwezekano wa kuiwekea Tanzania vikwazo kutokana na madai ya ukandamizaji wa kisiasa na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Miongoni mwa hatua zinazopendekezwa ni pamoja na vizuizi vya viza kwa viongozi na wanasiasa, tathmini upya ya ushirikiano wa kiusalama na mapitio ya ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema Tanzania itashughulikia suala hilo kupitia njia za kidiplomasia na imewaalika waasisi wa muswada huo kuitembelea nchi ili kujionea hali halisi.

Wabunge Nape Nnauye (Mtama), Ester Bulaya (Bunda Mjini), Elibariki Kingu (Singida Magharibi) na Mariam Mungula (Viti Maalumu) walitetea uhuru wa Tanzania na kushauri kuwepo kwa ushirikiano wa kidiplomasia wenye utulivu.

Mbunge wa ACT-Wazalendo, Addo shaibu alionya sera ya kutofungamana na upande wowote isitumike kufumbia macho hoja za haki, uwajibikaji na kupinga ukandamizaji duniani.

Shaibu amesema Sera ya Taifa ya kutofungamana na upande wowote isifanye jamii kukaa kimya kwenye ukandamizaji wa haki.

Ameitaka Serikali kusimama katika kusimamia haki na uwajibikaji ikipinga dhuluma na uonevu wa mataifa makubwa, akisisitiza juu ya sera ya kutofungamana.

Kufuatia m,jadala huo, Mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Salbinus David amesema ingekuwa msaada mkubwa kama wabunge wangeelekeza nguvu zaidi katika kueleza hatua zilizochukuliwa na Serikali baada ya vurugu za uchaguzi.

Amesema badala ya kushindana kutoa majibu makali dhidi ya ukosoaji kutoka nje, walipaswa kuonyesha mageuzi ya taasisi na michakato ya uwajibikaji iliyoanzishwa baada ya mgogoro huo.

“Ingeliimarisha nafasi ya kidiplomasia ya Tanzania kama wabunge wangeeleza kile ambacho nchi imefanya baada ya vurugu za uchaguzi wa Oktoba 29,” amesema.

David ametaja kuundwa kwa Tume ya Jaji Chande kuchunguza yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi wa 2025 pamoja na pendekezo lake la kuundwa kwa tume ya haki jinai ili kuwawajibisha waliohusika.

“Hilo lingeonyesha jumuiya ya kimataifa kuwa Tanzania inatambua yaliyotokea na inachukua hatua za dhati kurekebisha hali hiyo,” amesema.

“Diplomasia siyo kuhusu nani anazungumza kwa sauti kubwa zaidi. Ni kuhusu kuwashawishi wengine kuwa nchi yako inatambua changamoto zilizopo na inafanya kazi kuzitatua kwa uwajibikaji,” ameongeza.

Amesema hatari ya kutumia lugha za kimakabiliano ni kwamba inaweza kuimarisha mitazamo hasi nje ya nchi na kufanya mazungumzo na washirika wa kimkakati kuwa magumu wakati Tanzania bado inategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa kimataifa katika biashara, uwekezaji, usalama na ufadhili wa maendeleo.

Mwanasiasa na mchambuzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Loisulie amesema mijadala ya bungeni imeonyesha mvutano mpana zaidi kati ya uhuru wa Taifa na uwajibikaji wa kimataifa, ambao mataifa mengi ya Afrika yanazidi kukabiliana nao.

Anasema ingawa Tanzania ina msingi wa kutetea uhuru wake na kukataa kuingiliwa na mataifa ya nje, pia inapaswa kutambua kuwa diplomasia ya kimataifa ya sasa inaathiriwa sana na masuala ya utawala bora, haki za binadamu na uhalali wa kidemokrasia.

“Katika mfumo wa kisasa wa kimataifa, siasa za ndani na sera za nje zimeunganishwa kwa karibu sana. Matukio yanayohusiana na uchaguzi yanapovuta usikivu wa dunia, nchi haziwezi kutegemea hoja za uhuru wa taifa pekee. Lazima pia zionyeshe uwazi, uwajibikaji na utayari wa kushirikiana,” amesema.

Hata hivyo, Dk Loisulie amesema uamuzi wa Serikali kuwaalika wabunge wa Marekani kuitembelea Tanzania ulikuwa wa busara kidiplomasia kwa sababu umeonyesha utayari wa mazungumzo badala ya makabiliano.

Lakini ameonya kuwa mvutano wa muda mrefu na Washington unaweza kuwa na athari pana zaidi ya kisiasa.

“Marekani bado ni mshirika muhimu wa maendeleo na kimkakati kwa Tanzania. Kuzorota kwa uhusiano kunaweza kuathiri ushirikiano wa misaada, imani ya wawekezaji na hata ushirikiano wa kiusalama,” amesema.

Amesema sera ya Tanzania ya kutofungamana na upande wowote haipaswi kutafsiriwa kama kujitenga, akibainisha kihistoria nchi imeweza kudumisha uhusiano na mataifa yenye ushindani wa kimataifa kupitia diplomasia ya wastani na ya kimkakati.

Hata hivyo, Profesa Ali Makame Ussi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, amesema mjadala huo umeonyesha kuongezeka kwa hisia za kisiasa za ndani wakati juhudi za maridhiano ya kitaifa baada ya uchaguzi wenye utata, zikiendelea.

Amesema mara nyingi wanasiasa hutumia lugha kali za kizalendo wanapokabiliwa na ukosoaji wa kimataifa kwa sababu huvutia hadhira ya ndani na kuonyesha taswira ya kutetea heshima ya taifa.

“Lakini diplomasia inahitaji kuwepo kwa tofauti kati ya uhamasishaji wa kisiasa wa ndani na ushirikiano wa kimataifa,” amesema.

Profesa Ussi amesema ingawa ujumbe mkali wa kisiasa unaweza kuleta uungwaji mkono wa ndani, diplomasia yenye mafanikio mara nyingi hutegemea kujizuia, mawasiliano ya makini na hatua za kujenga imani.

“Changamoto ya Tanzania kwa sasa ni kuepuka kujenga taswira ya kujihami kupita kiasi huku ikiendelea kulinda uhuru wake,” amesema.

Ameongeza mtazamo wa kimataifa una umuhimu mkubwa katika dunia ya sasa iliyounganishwa, hasa kwa nchi zinazotafuta uwekezaji wa kigeni na ushirikiano mkubwa wa kijiografia na kisiasa.

“Majibu ya Tanzania yatapimwa si kwa kile viongozi wanasema bungeni pekee, bali pia kwa namna nchi inavyoonyesha kwa ushawishi mkubwa dhamira ya kufanya mageuzi, kutoa haki na kuendeleza maridhiano ya kisiasa,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *