KONA YA MALOTO: Kilichompeleka Msigwa CCM ndicho kimemrudisha ChademaKONA YA MALOTO: Kilichompeleka Msigwa CCM ndicho kimemrudisha Chadema

Mtego mkuu wa mwanasiasa ni upatikanaji, kuonekana na ushawishi. Mambo hayo matatu, kama hayapati, atahama. Anaweza kuhama eneo, chama au hata nchi. Zingatia kuwa mwanasiasa hawezi kuondoka mahali ambapo masilahi yake yapo na uelekeo wake ni mwema.

Mwanasiasa anapotaka kuondoka sehemu moja kwenda nyingine, kwa asilimia zaidi ya 80, atachagua maneno ambayo yatampa thamani kwa jamii. Yale hasa yaliyompa shinikizo, hatayasema. Endapo atayasema, basi atachukua yale ambayo yatampa mtaji wa umma. Kinywa cha mwanasiasa hakitamki neno, ispokuwa lenye masilahi kwake. Vinginevyo awe amelewa, au amekamatwa na mazingira.

Aghalabu (mara nyingi), mwanasiasa anapopanda ngazi na kufika juu kabisa, hushindwa kumudu kushuka chini na kuishi bila ushawishi wowote. Rais wa zamani wa Botswana, Ian Khama aliondoka nchini mwake mwaka 2021, akaweka makazi Afrika Kusini na Eswatini. Aliporejea Botswana, Ian alijiunga na chama cha upinzani, BPF, aliachana na kilichompa urais kwa mihula miwili, BDF.

Yupo Jose Eduardo dos Santos, Rais aliyeiongoza Angola kwa miaka 38 (Septemba 21, 1979 mpaka Septemba 26, 2017). Baada ya kuachia madaraka na kumkabidhi Joao Lourenco, Santos hakukaa Angola, aliweka makazi yake Barcelona, Hispania. Mauti yalimkuta akiwa ughaibuni. Ikuongezee alama kwenye hoja kuhusu wanasiasa, kuonekana, kupatikana na ushawishi.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu Tanzania 2010, wanasiasa wengi wa vyama vingine vya upinzani Tanzania Bara, walijiunga na Chadema. Vijana wapya waliotoka vyuoni, walichagua Chadema kuwa jukwaa lao la kisiasa. Sababu ni moja tu; Chadema kilikuwa chama kinachotoa ahadi ya jukwaa mbadala lenye nguvu. Kila mwanasiasa aliona dhahiri kwamba akiwa Chadema angeonekana, angesikika, na ingekuwa rahisi kujenga ushawishi.

Kueleka Uchaguzi Mkuu 2015, Chadema kwa mara nyingine walitoa ahadi ya jukwaa lenye nguvu. Jumlisha mapokezi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kisha kumfanya kuwa mgombea urais, wanasiasa wengi walitimkia Chadema. Siku zote, wanasiasa hufuata jukwaa rahisi kwao kuonekana, kupatikana, kusikika, kufikika na kupata fursa ya kujenga ushawishi.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, ilikuwa dhahiri kwamba Chadema wasingeshiriki. Na kweli hawakushiriki. Kutokana na mazingira hayo, Chadema hawakuwa wakitoa ahadi ya kuwa jukwaa la kisiasa, ambalo lingewezesha wanasiasa kuonekana, kusikika na kujenga ushawishi wa kuchaguliwa. Ni kwa sababu hiyo, wanasiasa hawakuhamia Chadema, zaidi chama hicho kilikimbiwa.

Vyama vya ACT-Wazalendo na Chaumma, vilikuwa jukwaa mbadala. Wana-Chadema walioona chama hicho hakikuwa na mlango wa kufanikisha masilahi ya ndoto zao za kisiasa, wengi walikimbilia Chaumma, wengine walikwenda ACT-Wazalendo. Aliyekuwa mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, baada ya kuona dirisha lake la upumuaji wa kisiasa limezibwa CCM, alihamia ACT-Wazalendo.

Mei 29, 2024, Peter Msigwa, mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, kwa tiketi ya Chadema, alishindwa uchaguzi wa uenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyasa. Alishindwa na mbunge wa zamani wa za Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi “Sugu”. Kabla ya uchaguzi huo, Msigwa alikuwa ndiye Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa. Matokeo hayo Msigwa hakuyapokea.

Kila lawama ya Msigwa aliielekeza kwa Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Freeman Mbowe, kwamba aliingiza ushawishi wake Kanda ya Nyasa, uliombeba Sugu na kumning’iniza yeye. Juni 30, 2024, Msigwa, alitimkia CCM na kupokelewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan. Mapokezi yenye hadhi, bila shaka!

Mwanasiasa kuhama chama na kupokewa na mkuu wa chama alichohamia, hakuna heshima kubwa kuliko hiyo. Baada ya kutua CCM, Msigwa alizungumza mpaka alijimaliza. Alikosoa mfumo wa demokrasia Chadema, kisha Msigwa alifika mbali zaidi akatamka kwamba hakuna mwanasiasa wa upinzani Tanzania ambaye hatamani kuwa CCM.

Mei 23, 2026, ukiwa umepita mwaka mmoja, miezi 10 na siku 22, Msigwa alitangaza kurejea Chadema. Kisha, Mei 24, 2026, Msigwa alipokewa Chadema, kupitia Tawi la Mkimbizi, jimbo la Iringa Mjini. Sababu ambayo Msigwa ameitoa kurejea kwake Chadema ni kuwa alipokuwa CCM aliishi kwa maumivu makali tangu yatokee matukio ya Oktoba 29, 2025, ambayo yalisababisha vifo, majeruhi, wizi, na uharibifu mkubwa wa mali binafsi na za umma.

Msigwa katika maneno yake ya kuhama CCM na kurejea Chadema, aliyaita matukio ya Oktoba 29, 2025 kuwa yalikuwa ya ukiukwaji wa haki, utu na dhuluma dhidi ya uhai wa binadamu. Akasema kwamba baada ya tafakuri ya kina, aliona asingeweza kuendelea kuishi katika huzuni na ukimya tena. Kwa maana hiyo, amerejea Chadema ili aseme. CCM alishindwa kusema.

Kwa nini Chadema leo? Wapo watu watasema ni kwa sababu ndiyo nyumbani kwao kisiasa. Yupo mtu anakumbusha kuwa Msigwa alishakuwa NCCR-Mageuzi na TLP, kabla ya Chadema. Mbona si Chaumma au ACT-Wazalendo. Mtu mwenye jicho la uchambuzi atakumbusha kuwa Chadema ndicho chama ambacho upepo wake wa kisiasa unavuma vizuri kabisa.

Mikutano ya Oparesheni Katiba Mpya, iliyoanza Katoro, Geita, Kahama, Shinyanga, Arusha na Dodoma, imevuta watu wengi. Chadema kupitia mikutano hiyo kimethibitisha uhai na uungwaji mkubwa wa kisiasa kutoka kwa wananchi. Kila mwanasiasa angependa kuwa sehemu ya jukwaa linalokubalika kisiasa.

Msigwa anarejea Chadema kipindi upepo ukivuma hasa kwenye chama hicho. Unaweza kujiuliza; kama chama hicho kingekuwa bado kimefungiwa kufanya shughuli za kisiasa, Msigwa angeomba kurejea Chadema? Amesema hataki kuendelea kukaa kimya kuhusu yaliyotokea Oktoba 29, 2025. Je, angesema kwenye chama ambacho kimefungiwa?

Inakaribia miezi saba tangu Oktoba 29, 2025. Kipindi chote hicho Msigwa hakufanya uamuzi wowote. Je, Msigwa anaumizwa zaidi sasa na matukio ya Oktoba 29, 2025, kuliko kipindi ambacho hali ilikuwa ya moto zaidi? Zingatia, nilishatangulia kusema kuwa mwanasiasa anapofanya uamuzi wake, hutafuta ujumbe ambao utamfanya apate thamani kwenye uso wa jamii.

Ukweli ni huu; Msigwa alihama Chadema na kutimkia CCM kwa sababu aliona mtungi wa oksijeni yake ya kisiasa umefungwa. CCM alikuwa na matarajio. CCM walimtumia sana kipindi cha uchaguzi, ingawa hawakumpa tiketi ya kugombea ubunge Iringa Mjini. Baada ya uchaguzi, CCM hawamtumii tena. Haonekani, hasikiki, hapatikani, na hana jukwaa la kujenga ushawishi. Jiulize, Msigwa angepata ubunge CCM, angehamia Chadema?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *