Hiki hapa kilichotibua ushirika wa Rais Faye, SonkoHiki hapa kilichotibua ushirika wa Rais Faye, Sonko

Kwenye sayansi ya siasa ulimwenguni, kuna msemo maarufu usemao kwamba “mwanasiasa hatakiwi kuwa na rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu”.

Msemo huo umekuwa ukidhihirika mara nyingi kwenye siasa ambapo waliokuwa marafiki wakubwa wanageuka kuwa maadui na waliokuwa maadui wanakuwa marafiki wakubwa na kila mtu anashangaa.

Hapa Tanzania, kila mtu atakumbuka namna Jakaya Kikwete na Edward Lowassa walivyokuwa marafiki, walikuwa washirika wakubwa wa kisiasa hadi kufanikiwa kutwaa madaraka, lakini baadaye waligeuka kuwa mahasimu na ushirika huo kuvunjika.

Huko Kenya, Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto walikuwa maswahiba wakubwa kiasi kwamba vyombo vya habari viliupa muunganiko wao jina la “Uhuruto” likitokana na majina yao na namna walivyokuwa wameshibana.

Hata hivyo, hawakufanikiwa kumaliza uongozi wakiwa wamoja, Uhuru hakukubali kumuunga mkono Ruto kwenye mbio za uchaguzi, badala yake alimuunga mkono Raila Odinga kutoka upinzani ambaye wakati huo walianzisha mkakati wa Building Bridges Initiative (BBI).

Vilevile, Afrika Kusini, Jacob Zuma alipokuwa akiwania uais wa nchi hiyo, alimteua rafiki yake, Cyril Ramaphosa kuwa makamu wake na wawili hao walifanya kazi kwa pamoja hadi pale Zuma alipojiuzulu na nafasi yake kuchukuliwa na Ramaphosa.

Tangu Zuma ameondoka madarakani, wawili hao wamekuwa mahasimu kiasi kwamba alilazimika kujivua uanachama wa chama chake cha African National Congress (ANC) na kuanzisha chjama kipya cha uMkhontho weSizwe (MK).

Hivi karibuni, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye alitengua uteuzi wa Waziri Mkuu, Ousman Sonko ambaye walipitia misukosuko pamoja kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2024, uliowaingiza madarakani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa kupitia vyombo vya habari vya Serikali, mawaziri wote wamefutwa kazi huku Serikali iliyomaliza muda wake ikipewa jukumu la kuendelea na shughuli za kawaida za kila siku, alisema Katibu Mkuu wa Ikulu, Oumar Samba Ba.

Hatua hiyo imekuja baada ya miezi kadhaa ya mvutano uliokuwa ukiongezeka kati ya viongozi hao waliokuwa washirika wa karibu kabla ya kugeuka wapinzani wa kisiasa. Sonko, ambaye ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa kwa vijana, alimuidhinisha Faye katika uchaguzi wa mwaka 2024 baada ya kuzuiwa kugombea kutokana na hukumu ya kashfa.

Mgawanyiko huo umetokea wakati Senegal ikikabiliwa na shinikizo kubwa la kiuchumi. IMF ilisimamisha mpango wake wa mkopo wa Dola za Marekani 1.8 bilioni kwa Senegal baada ya kubainika kuwa kulikuwa na taarifa zisizo sahihi kuhusu kiwango cha deni la taifa, hali iliyosababisha deni la nchi hiyo kufikia asilimia 132 ya pato lake la taifa mwishoni mwa mwaka 2024.

Kilichoanza kama mojawapo ya miungano ya kisiasa iliyosherehekewa zaidi barani Afrika sasa kinazidi kubadilika na kuwa mgogoro kati ya Rais Faye na Sonko kuhusu mamlaka, urithi wa uongozi na udhibiti wa harakati iliyowaweka madarakani.

Hilo halikutokea ghafla, maandalizi ya mkutano mkubwa katika mji wa pwani wa Mbour nchini Senegal, ulioandaliwa na muungano unamuunga mkono Faye yalidhihirisha kuongezeka kwa mvutano kati ya Rais Faye na Sonko.

Hali hiyo inajiri huku mvutano wa nani anadhibiti chama cha Pastef, serikali na njia kuelekea uchaguzi wa urais wa mwaka 2029 ukizidi kujitokeza waziwazi.

Hatima ya Sonko kisiasa

Sonko alikuwa mmoja wa viongozi maarufu wa upinzani chini ya utawala wa Rais wa zamani wa Macky Sall, ambaye uamuzi wake wa kuahirisha uchaguzi wa mwaka 2024 ulisababisha maandamano na machafuko.

Faye na Sonko wote ni maofisa wa zamani wa kodi ambao waliwahi kufungwa gerezani kabla ya uchaguzi wa mwaka 2024. Waliachiwa huru siku 10 kabla ya uchaguzi huo uliopangwa upya, ambapo Faye aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 54 ya kura.

Baada ya ushindi huo, Faye alimteua Sonko kuwa Waziri Mkuu. Sasa baada ya Sonko kuondolewa madarakani, hatua zake zinazofuata bado hazijulikani.

Machi mwaka huu, Sonko alisema yuko tayari kukiondoa chama chake cha Pastef serikalini na kurejea upinzani iwapo Faye angeachana na ajenda za chama hicho, jambo lililochochea hisia kuwa mvutano wa madaraka kati ya wawili hao ulikuwa umefikia hatua ngumu kusuluhishwa.

Chama cha Pastef kina idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Taifa, hali inayoweza kuifanya Serikali kupata wakati mgumu kupitisha mageuzi yanayohitajika ili kupata msaada wa IMF.

Mwezi uliopita, wabunge waliidhinisha kwa wingi mabadiliko ya sheria ya uchaguzi ambayo yanaweza kufungua njia kwa Sonko kugombea urais mwaka 2029.

Miongoni mwa sera zilizomtambulisha Sonko ni ukaguzi wa mikataba ya rasilimali za Senegal, ikiwemo sekta mpya ya mafuta na gesi.

Machi mwaka huu, Sonko alitangaza kuwa mkataba wa gesi wa kampuni ya BP kwa mradi wa Greater Tortue Ahmeyim haukuwa wa haki na kufuta leseni 71 za uchimbaji madini.

Alikuwa akisisitiza kuwa kufanya mazungumzo upya ya mikataba ya mafuta na gesi kungesaidia kupunguza gharama za nishati nchini humo pamoja na kuimarisha hali ya fedha ya Senegal iliyoyumba.

Mapema mwezi huu, Rais Faye alisema kuwa Sonko angebaki madarakani kwa muda wote ambao angeendelea kuwa na imani naye. “Pindi imani hiyo itakapovunjika, kutakuwa na Waziri Mkuu mpya,” aliwaambia waandishi wa habari wa Senegal.

Sonko, ambaye amekuwa akitoa kauli zenye kuchochea chuki dhidi ya watu wa jinsia moja nchini Senegal, hivi karibuni aliongoza juhudi za kupitishwa kwa sheria mpya inayoweka vifungo vikali gerezani kwa watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Kumekuwa na mawimbi ya kukamatwa kwa watu chini ya sheria hiyo mpya, ambayo imekosolewa vikali na mataifa ya nje.

Mustakabali wa Faye

Hadi sasa, Sonko ndiyo kiongozi wa chama cha Pastef, alichokianzisha mwaka 2014, chama kilichounda serikali na chenye wabunge wengi. Unaweza kujiuliza, nini itakuwa hatma ya Faye endapo Sonko atakiondoa chama chake serikalini?

Maana yake ni kwamba Faye ambaye aliingia madarakani kama mgombea wa muungano wa upinzani, akiungwa mkono na chama cha Pastef pamoja na Sonko, aliyeenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi huo.

Faye atahitaji kutafuta uungwaji mkono wa vyama vingine ili kujiandaa na mbio za uchaguzi ujao. Hata hivyo, atakabiliana na wingi wa wabunge Pastef ya Sonko kama wataamua kuwa upande wa kiongozi wao huyo. 

Muda ni mwalimu mzuri. Marafiki wametengana. Faye atawezaje kutengeneza washirika wengine watakaomvusha kwenye uchaguzi wa 2029? Maandalizi yanatakiwa kuanza sasa na uteuzi wa Waziri Mkuu mpya utatoa picha kamili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *