Mahakama yatupilia mbali kesi ya uchaguzi Tunduru KusiniMahakama yatupilia mbali kesi ya uchaguzi Tunduru Kusini

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songea imetupilia mbali shauri la uchaguzi lililokuwa likipinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa Jimbo la Tunduru Kusini baada ya kubaini kuwa walalamikaji walishindwa kutimiza masharti ya kisheria kuhusu ulipaji wa dhamana ya gharama za kesi.

Shauri hilo la Uchaguzi namba 29982/2025 lilifunguliwa na Mohamed Rais na Odax John dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tunduru Kusini, Fadhili Chilombe (mbunge wa Jimbo hilo) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Uamuzi huyo wa kutupilia mbali shauri hilo umetolewa jana Mei 26, 2026 na Jaji Sedekia Kisanya, na nakala ya uamuzi huo kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Katika kesi hiyo, walalamikaji walikuwa wakipinga ushindi wa Chilombe aliyekuwa ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa ubunge wa jimbo hilo na Msimamizi wa Uchaguzi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Msingi wa kesi

Mahakama ilieleza kuwa wakati walalamikaji wanafungua kesi hiyo Novemba 29, 2025, waliwasilisha hati ya kuthibitisha kuwa walikuwa wamepata msaada wa kisheria kupitia Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), wakidai hawakuwa na uwezo wa kifedha kugharamia mwenendo wa kesi hiyo.

Kwa mujibu wa hati hiyo, Wakili John Seka ndiye aliyekuwa ametajwa kuwawakilisha chini ya mpango wa msaada wa kisheria, jambo lililofanya Mahakama awali kutupilia mbali pingamizi lililokuwa limewasilishwa na upande wa walalamikiwa kuhusu kushindwa kwa walalamikaji kulipa dhamana ya gharama za kesi.

Walalamikiwa wa kwanza na wa tatu walikuwa wameiomba Mahakama kutupilia mbali shauri hilo wakidai walalamikaji walikiuka masharti ya kifungu cha 140(3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2025 pamoja na kanuni ya 11(1) ya Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge kwa kushindwa kuwasilisha dhamana ya gharama ndani ya siku 14 tangu kufungua kesi.

Katika uamuzi wa awali uliotolewa Desemba 29, 2025, Mahakama ilikubaliana na hoja ya walalamikaji kwamba hawakulazimika kulipa dhamana hiyo kwa kuwa walikuwa wanapata msaada wa kisheria.

Hata hivyo, kabla ya kesi kuanza kusikilizwa rasmi, walalamikiwa waliwasilisha maombi ya mapitio ya madai juu ya uamuzi huo wakidai walikuwa wamepata taarifa mpya kwamba TLS haikuwa na mamlaka ya kutoa msaada wa kisheria katika kesi hiyo kwa kuwa haikuwa imesajiliwa kwa madhumuni hayo chini ya Sheria ya Msaada wa Kisheria.

Katika uamuzi wa mapitio uliotolewa Mei 5, 2026, Mahakama ilikubaliana na hoja hiyo na kutengua uamuzi wake wa awali, ikisema walalamikaji hawakuwa na msaada halali wa kisheria na hivyo walipaswa kulipa dhamana ya gharama kama sheria inavyotaka.

Baada ya uamuzi huo, Wakili wa Serikali, Edwin Webiro kwa niaba ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tunduru Kusini na AG waliiomba Mahakama kufuta shauri hilo kwa hoja kuwa walalamikaji walikuwa tayari wamepitwa na muda wa kulipa dhamana ya gharama.

Webiro aliwasilisha mahakamani athari ya uamuzi wa Mei 5, 2026 na kuwa inairejesha Mahakama katika masharti ya kisheria yanayohusu ulipaji wa dhamana ya gharama na uhai wa shauri la uchaguzi.

Wakili huyo alirejea kanuni ya 11 ya Mashauri ya Uchaguzi, akisisizita kuwa dhamana ya gharama inapaswa kulipwa ndani ya siku 14 tangu kufunguliwa shauri au ndani ya muda huo kuwasilisha maombi ya uamuzi wa kiasi cha dhamana.

Aliieleza Mahakama kuwa walalamikaji hawakutekeleza wajibu huo, Mahakama inapaswa kujielekeza katika matakwa ya kifungu cha 140(7) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 (baadaye sheria ya uchaguzi), kinachotoa matokeo ya moja kwa moja kwamba endapo dhamana ya gharama haitalipwa ndani ya muda uliowekwa, shauri litafutwa.

Katika kuunga mkono hoja hiyo, alirejea uamuzi wa Mchinjita Rashid Ishaka dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Lindi Mjini na wengine, ambapo Mahakama ilifuta shauri kwa msingi wa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya gharama na masuala ya msaada wa kisheria.

Aidha, hoja hiyo iliungwa mkono na Wakili Gilbert Sawe anayemwakilisha mlalamikiwa wa pili huku wakili wa walalamikaji, John Seka akipinga vikali pendekezo la kufutwa shauri hilo na kuomba muda wa kuwasilisha majibu, ombi ambalo Mahakama iliridhia.

Mei 19, 2026 mahakama ilipopanga shauri hilo kwa ajili ya kusikiliza majibu ya walalamikiwa, wakili Seka alieleza kuwa masharti yaliyopo katika Kanuni ya 31 (1) ya Kanuniz na Masharti ya Uchaguzi yanaungwa mkono na misingi ya kikatiba hasa Ibara za 107A (2) (a) na (e), 108 na 13 (1) na (6) (a) ambazo zinaelekeza Mahakama kutofungwa na masharti ya kiufundi yanatoweza kuzingatia haki ya kikatiba na kisheria.

Ameeleza vifungu hivyo vinaelekeza kutolewa haki bila ubaguzi wa hadhi ya mtu na kuhakikisha haki ya kusikilizwa na kupata nafuu za kisheria. Kwa maoni yake, haki hiyo ya kupata nafuu za kisheria inajumuisha pia fursa ya kuomba kuongezewa muda ili kukamilisha taratibu za kisheria.

Aliongeza kuwa kanuni za kuongeza muda zinahitaji kuwepo kwa sababu za msingi (good cause), kutokuwepo kwa ucheleweshaji wa kupita kiasi,kutokuwepo kwa uzembe au kuwepo hoja za kisheria.

Wakili Seka aliijulisha Mahakama kuwa tayari walalamikaji wamewasilisha notisi ya rufaa (notice of appeal) katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa mapitio,hivyo kuomba Mahakama izingatie kuwa haitakuwa busara kulifuta shauri kabla ya hatma ya rufaa hiyo kujulikana.

Hoja hiyo ilipingwa na upande wa walalamikiwa wakieleza hoja iliyopo mbele ya Mahakama si ya kuongeza muda bali uhalali wa shauri kuendelea bila dhamana ya gharama kama inavyotakiwa kisheria.

Wakili hiyo alieleza kuhusu kuwepo notisi ya rufaa, hakuzuii mwenendo wa shauri akirejea shauri la Johari Kabourou na wengine dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Kigoma Mjini na wengine ambapo mahakama hii kwa kuzingatia hoja zilizotolewa na Wakili Seka ilikataa kusitisha usikilizwaji wa shauri la uchaguzi licha ya uwepo wa notisi ya rufaa.

Uamuzi wa Mahakama

Katika uamuzi wake, Jaji Kisanya amesema Mahakama imebaini kuna mvutano wa masuala matatu ambayo ni shauri hilo lilifunguliwa kwa msingi wa madai kuwa walalamikaji walikuwa wamepata msaada wa kisheria.

Nyingine ni pingamizi lililowekwa kupinga uhalali wa shauri hilo kwa hoja kwamba walalamikaji hawakuwa wamelipia dhamana ya gharama wala kuwasilisha maombi ya kupunguziwa au kuondolewa dhamana hiyo, lilitupiliwa mbali na Mahakama.

Suala la tatu, ni kufuatia maombi ya mapitio yaliyowasilishwa baada ya, uamuzi wa awali kuhusu pingamizi hilo ulitenguliwa na Mahakama ikaamua kuwa walalamikaji katika shauri hilo hawakuwa na msaada wa kisheria na kwamba walikuwa wameshindwa kulipa dhamana ya gharama.

Jaji amesema kutokana na hali hiyo, suala linalopaswa kuangaliwa sasa ni hatma ya shauri hilo la uchaguzi baada ya kubainika walalamikaji hawakuwa na msaada wa kisheria na walishindwa kulipa dhamana ya gharama.

“Katika kuajdili suala hilo, Mahakama inaona kuwa kimsingi athari ya uamuzi wa mapitio ilikuwa ni kukubaliana na pingamizi la kisheria lililowasilishwa na walalamikaji wa pili na tatu, na zaidi ikaamua kuwa walalamikaji wameshindwa kulipa dhamana ya gharama,”

Jaji Kisanya amesema katika mashauri ya uchaguzi, uzingatiaji wa muda ni wa umuhimu wa kipekee, hasa ikizingtakiwa kwamba kila hatua ya shauri ina muda wake maalum, ikiwemo muda wa kuanzisha na kukamilisha mwenendo wa shauri lenyewe.

Amesema Mahakama hiyo inatambua msingi wa kikatiba unaosisitiza kuwa Mahakama haipaswi kufungwa na urasimu wa kiufundi na kwamba zinapaswa Kutenda haki kwa kuzingatia masharti ya Katiba na Sheria.

Kwa kuhitimisha amesema Mahakama inaona athari ya uamuzi wa mapitio ilikuwa ni kukubaliana na pingamizi la kisheria lililohusu uhalali wa shauri hilo na kuwa ni bayana kwambas hauri limepoteza sifa za kuendelea kuwepo mbele ya Mahakama hiyo.

“Katika jumla yote, shauri hili la uchaguzi linatupiliwa mbali (struck out) kwa kukosa sifa kutokana na uamuzi wa mapitio wa Mahakama hii uliotengua uamuzi wa wali kuhusu pingamizi la kisheria. Uamuzi huu unaweza kukosa athari iwapo  rufaa iliyokusudiwa itakubaliwa na Mahakama ya Rufaa, na hivyo shauri litaendelea,”amehitimisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *