
Hayo yameelezwa katika ripoti mpya iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
Ripoti hiyo inajumuisha tathmini za tabiri zilizotolewa na taasisi 13 tofauti za kisayansi.
Ripoti hiyo imechambua takwimu za hali ya hewa za miaka mitano iliyopita na kutoa makadirio ya joto na mvua kwa maeneo mbalimbali duniani kwa miaka mitano ijayo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wastani wa joto la uso wa dunia kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030 unatarajiwa kuwa nyuzi joto 1.3 hadi 1.9 za celsiasi juu ya wastani wa kipindi cha kabla ya mapinduzi ya viwanda cha mwaka 1850 hadi 1900.
Rekodi mpya za joto
Kuna uwezekano wa asilimia 86 kwamba mwaka mmoja kati ya 2026 na 2030 utakuwa na joto kubwa zaidi kuliko mwaka 2024 ambao ndio mwaka wenye joto la juu zaidi kuwahi kurekodiwa duniani.
Wakati huo huo, wastani wa joto la uso wa dunia unatarajiwa kuzidi kwa muda kiwango cha nyuzi joto 1.5 za celsiasi juu ya wastani wa miaka ya 1850 hadi 1900 kwa angalau mwaka mmoja kati ya 2026 na 2030, jambo ambalo lina uwezekano wa asilimia 91 kutokea.
Pia kuna uwezekano mkubwa kwamba wastani wa joto kwa kipindi kizima cha miaka mitano ya 2026 hadi 2030 utakuwa zaidi ya nyuzi joto 1.5 za celsiasi juu ya kiwango cha kabla ya mapinduzi ya viwanda.
Hata hivyo, kuna uwezekano mdogo kwamba joto litazidi nyuzi joto 2 za celsiasi juu ya kiwango hicho cha miaka ya 1850 hadi 1900.
Wataalamu pia wanatarajia hali ya El Niño kujitokeza, hasa katika miaka ya 2027 na 2028.
“Hali ya El Niño inatarajiwa kujitokeza mwishoni mwa mwaka 2026, jambo ambalo linaongeza uwezekano kwamba mwaka 2027 utakuwa mwaka mwingine wa rekodi ya joto,” amesema Leon Hermanson, mwandishi mkuu wa ripoti hiyo.
Ripoti imefafanua kuwa kiwango cha nyuzi joto 1.5 na 2 za celsiasi kilichowekwa katika Mkataba wa Paris kinarejelea ongezeko la joto la muda mrefu, kwa kawaida katika kipindi cha miaka 20.
Hivyo, ukweli kwamba katika baadhi ya miaka joto duniani linaweza kuvuka viwango hivyo kwa muda mfupi haumaanishi kwamba malengo ya muda mrefu yaliyowekwa katika Mkataba wa Paris hayawezi kufikiwa tena.
Makadirio ya kikanda
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, joto katika eneo la Aktiki katika misimu mitano ijayo ya baridi ya Kaskazini mwa Dunia kati ya Novemba na Machi linatarajiwa kuwa nyuzi joto 2.8 za celsiasi juu ya wastani wa miaka ya 1991 hadi 2020, kiwango ambacho ni zaidi ya mara tatu na nusu ya wastani wa ongezeko la joto duniani kwa kipindi hicho.
Makadirio ya hali ya barafu ya bahari katika Aktiki kwa mwezi Machi kati ya mwaka 2026 hadi 2035 yanaonesha kuendelea kupungua kwa kiwango cha barafu katika bahari za Barents, Bering na Okhotsk.
Makadirio ya mvua yanaonesha kuwa Kaskazini mwa dunia kutakuwa na hali ya mvua nyingi kuliko kawaida katika misimu mitano ijayo ya baridi.
Katika maeneo ya Sahel, Kaskazini mwa Ulaya, Alaska na Siberia, hali ya mvua nyingi inatarajiwa zaidi katika kipindi cha kiangazi.
