Mahakama yatupilia mbali madai ya Kibo Poultry ya fidia ya Sh528 milioniMahakama yatupilia mbali madai ya Kibo Poultry ya fidia ya Sh528 milioni

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Kanda ya Arusha imeitupilia mbali kesi ya Kampuni ya Kibo Poultry Unit Limited iliyokuwa ikiidai Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) zaidi ya Sh528.7 milioni kama fidia ya ardhi iliyopo Kijiji cha Samaria wilayani Arumeru, mkoani Arusha.

Kesi hiyo ya ardhi ilifunguliwa na kampuni hiyo ikidai kuwa ililipwa fidia isiyo ya haki baada ya ardhi yake yenye ukubwa wa ekari 48 kuchukuliwa kwa ajili ya matumizi ya eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), eneo ambalo kwa sasa lina thamani ya zaidi ya Sh582.7 milioni.

Hukumu hiyo ilitolewa Mei 25, 2026 na Jaji Dafina Ndumbaro, huku nakala yake ikiwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Jaji Ndumbaro amesema Mahakama ilikubaliana na hoja za TAA kwamba kampuni hiyo haikuwa mmiliki halali wa ardhi hiyo bali ililipwa fedha za ‘kifuta jasho’ kutokana na maboresho yaliyokuwa yamefanywa kwenye eneo hilo.

Msingi wa kesi

Katika madai yake, kampuni hiyo ilidai kuwa ilikuwa na hati miliki ya kimila namba 045 iliyotolewa Novemba 11, 2016 na kwamba ardhi hiyo ilikuwa na thamani ya zaidi ya Sh582 milioni kwa mujibu wa bei za sasa za soko.

Kibo Poultry ilidai kuwa Mei 29, 2025 ililipwa Sh2.57 milioni pekee kama fidia, kiwango walichodai hakikulingana na thamani halisi ya ardhi pamoja na maendeleo yaliyokuwapo, ikiwamo kisima cha kisasa na miti iliyopandwa katika eneo hilo.

Kupitia kesi hiyo, kampuni iliomba Mahakama iamuru kufanyika kwa tathmini mpya ya ardhi na TAA ilipe fidia ya Sh528.7 milioni pamoja na gharama za kesi.

Hata hivyo, upande wa TAA ulipinga madai hayo ukieleza kuwa ardhi hiyo imekuwa chini ya umiliki wa Serikali tangu mwaka 1969 kupitia eneo la maendeleo ya uwanja wa ndege wa KIA.

TAA ilieleza kuwa eneo hilo ni sehemu ya ekari 11,085 zilizokuwa chini ya Kurugenzi ya Viwanja vya Ndege kabla ya baadaye kuhamishiwa Kampuni ya Maendeleo ya Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KADCO) na sasa TAA.

Shahidi wa kwanza wa mlalamikaji, Viola Chuwa, aliiambia Mahakama kuwa eneo hilo lilinunuliwa kutoka kwa familia ya Melkizedeck Palangyo Novemba 11, 2016 kwa Sh168 milioni na kwamba waliomba idhini ya Baraza la Kijiji na kupewa hati ya kimila namba 045.

Alieleza kuwa walifanya uchunguzi wa kina kabla ya kununua eneo hilo ambapo kupitia ofisi ya kijiji walibaini kuwa eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na Palangyo.

Shahidi wa pili, Melkizedeck Palangyo, alieleza kununua eneo hilo kutoka kwa Mbise, lakini wakati anahojiwa alidai kurithi eneo hilo kutoka kwa baba yake na hakukuwa na makubaliano ya mauzo kati yake na Mbise ili kuthibitisha uuzaji wa awali.

Mashahidi wa TAA waliieleza Mahakama kuwa ardhi inayogombaniwa ni sehemu ya eneo la uwanja wa ndege wa KIA lililokuwa chini ya Serikali tangu mwaka 1969.

Shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi, Hamis Tembele, amesema eneo hilo awali lilikuwa chini ya pori la akiba la Sanya Lelatema kabla ya kukabidhiwa kwa shughuli za uwanja wa ndege na baadaye kumilikishwa rasmi kupitia hati ya umiliki namba 22270 iliyotolewa mwaka 2006.

Alidai kuwa eneo hilo lenye zaidi ya hekta 11,000 limekuwa likivamiwa na wananchi kwa miaka mingi kwa shughuli za kilimo na makazi, huku Kibo Poultry ikiwa miongoni mwa wavamizi 1,712 waliobainika kupitia doria za mara kwa mara za mamlaka hiyo.

Alisisitiza kuwa watu hao hawakuwa wamiliki halali wa ardhi na hivyo hawakustahili kulipwa fidia kama wamiliki wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, Serikali kupitia usimamizi wa KADCO na baadaye TAA ilikubali kutoa malipo ya ‘kifuta jasho’ kwa watu waliokuwa wamefanya maboresho kwenye ardhi hiyo baada ya viongozi wa vijiji kuomba wananchi hao wasiondolewe bila chochote.

Amesema Kibo Poultry ililipwa Sh2.57 milioni kwa ajili ya maboresho yaliyokuwapo kwenye eneo hilo na si kama fidia ya umiliki wa ardhi.

Shahidi wa tatu, Leonard Mpanju, aliieleza Mahakama kuwa hati miliki ya kimila iliyokuwa inashikiliwa na Kibo Poultry ilitolewa kimakosa kutokana na taarifa zisizo sahihi zilizowasilishwa kwa mamlaka za kijiji.

Amesema katika mazingira ya umiliki wa aina mbili, hati iliyotolewa kwanza ndiyo inayotambuliwa kisheria, akisisitiza kuwa hati ya TAA ya mwaka 2006 ilikuwa na nguvu zaidi kuliko hati ya mlalamikaji iliyotolewa mwaka 2016.

Ameeleza kuwa mamlaka za kijiji zilipotoshwa wakati wa kutoa hati ya kimila kwa mlalamikaji bila kujua kuwa eneo hilo tayari lilikuwa chini ya umiliki wa Serikali.

Amesema kwa msingi huo, mlalamikaji hakuwa mmiliki halali wa ardhi bali alikuwa miongoni mwa waliovamia eneo la KIA na hivyo hakuwa na haki ya kudai fidia hiyo.

Katika ziara ya Mahakama kwenye eneo la mgogoro Aprili 30, 2026, shahidi wa pili, Clement Mgungo, alisema tathmini iliyofanywa na Serikali ilibaini kuwapo kwa kisima kisichokamilika chenye thamani ya Sh1 milioni na kwamba hakukuwa na miti iliyopandwa kama ilivyodaiwa na mlalamikaji.

Badala yake, alisema eneo hilo lilikuwa na miti ya asili aina ya minyaa iliyopandwa pembezoni mwa mipaka ya ardhi hiyo.

Uamuzi wa Mahakama

Jaji Ndumbaro amesema Kibo Poultry Unit Limited ilishindwa kuthibitisha umiliki halali wa ardhi hiyo ili kustahili kulipwa fidia waliyoidai.

Mahakama ilieleza kuwa pamoja na kampuni hiyo kuwa na hati miliki ya kimila iliyotolewa mwaka 2016, haikuweza kuonyesha mlolongo wa namna ardhi hiyo ilivyopatikana kutoka kwa wamiliki wa awali hadi kufika kwake.

Mahakama ilikubaliana na ushahidi wa TAA kuwa eneo hilo lilikuwa chini ya umiliki wa Serikali tangu mwaka 1969 na lilikuwa na hati rasmi ya mwaka 2006.

Jaji Ndumbaro amesema Sh2.57 milioni zilizolipwa kwa mlalamikaji zilikuwa ni malipo ya maboresho yaliyofanywa kwenye eneo hilo na si fidia ya umiliki wa ardhi.

Aidha, Mahakama ilibaini kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai ya kuwapo kwa miti na kisima chenye thamani ya Sh20 milioni kama ilivyodaiwa na mlalamikaji.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama ilitupilia mbali madai ya fidia ya zaidi ya Sh528 milioni na kuiamuru kampuni hiyo kulipa gharama za kesi.

“Mlalamikaji alishindwa kuthibitisha umiliki wa ardhi hiyo ili kustahili fidia anayodai. Malipo aliyopokea yalikuwa kwa ajili ya maboresho yaliyofanyika kwenye eneo hilo,” ilieleza sehemu ya hukumu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *