
Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imetangaza hatua za haraka za kifedha na kiufundi kusaidia kudhibiti mlipuko mpya wa Ebola unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda, huku tahadhari ikiongezeka kuhusu uwezekano wa kusambaa kwa ugonjwa huo katika nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana Mei 28, 2026, Benki ya Dunia imesema inalenga kupeleka fedha na utaalamu wa haraka kwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele, kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza uwezo wa nchi husika kufuatilia maambukizi na kudhibiti usambaaji wa virusi hivyo.
Taasisi hiyo imeeleza kuwa jamii zilizo hatarini zaidi, wahudumu wa afya na serikali zinazopambana na mlipuko huo ndizo kipaumbele chake kikuu kwa sasa.
Katika DRC, Benki ya Dunia kupitia mradi wa Health Emergency Preparedness, Response and Resilience (HEPRR), imewezesha kupelekwa kwa wataalamu wa magonjwa ya mlipuko, wataalamu wa kudhibiti maambukizi pamoja na timu za mawasiliano ya hatari katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Aidha, vifaa vya uchunguzi wa maabara na wataalamu wa vipimo wamepelekwa katika mji wa Bunia ili kuongeza uwezo wa kupima wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola.
Mbali na hilo, mradi mwingine wenye thamani ya dola milioni 555 unaendelea kuhakikisha huduma muhimu za afya ya uzazi, chanjo na huduma za watoto wachanga zinaendelea kutolewa katika zaidi ya vituo 3,500 vya afya nchini humo licha ya hali ya dharura.
Benki ya Dunia pia imekumbusha kuwa kupitia mradi wa REDISSE, ilisaidia kujenga maabara kubwa zaidi ya kiwango cha biosafety mashariki mwa DRC, ambayo sasa ndiyo kitovu kikuu cha uchunguzi wa Ebola katika eneo la mlipuko.
Wakati huo huo, taasisi mbalimbali za kimataifa zimeanza kutoa michango ya fedha kusaidia kudhibiti mlipuko huo unaoendelea kusambaa kwa kasi.
Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) limetangaza kutoa dola milioni 60 kutoka mfuko wake wa dharura wa kukabiliana na majanga ili kusaidia juhudi za kudhibiti Ebola katika DRC na nchi jirani zilizo katika hatari ya maambukizi.
Fedha hizo zinatarajiwa kuelekezwa katika shughuli za ufuatiliaji wa waliokutana na wagonjwa wa Ebola, ujenzi wa vituo vya matibabu, elimu kwa jamii, vifaa tiba pamoja na kuimarisha huduma za afya katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Kwa upande wake, Taasisi ya Gates Foundation nayo imetangaza msaada wa kifedha na kiufundi kusaidia mapambano dhidi ya Ebola, ikieleza kuwa inafanya kazi kwa karibu na serikali za DRC na Uganda pamoja na mashirika ya afya duniani ili kuhakikisha upatikanaji wa vipimo, vifaa kinga kwa wahudumu wa afya na matibabu ya haraka kwa wagonjwa.
Ingawa kiwango kamili cha fedha kilichotolewa na Gates Foundation hakijawekwa wazi hadi sasa, taasisi hiyo imesema itaendelea kuongeza msaada kulingana na mahitaji yatakayojitokeza wakati wa mapambano dhidi ya mlipuko huo.
Nchini Uganda, mamlaka zimeongeza hatua za tahadhari huku baadhi ya mipaka kati yake na DRC ikifungwa kwa muda ili kudhibiti usambaaji wa ugonjwa huo. Benki ya Dunia imesema ipo kwenye mazungumzo ya karibu na Serikali ya Uganda pamoja na washirika wa maendeleo ili kutathmini mahitaji mapya ya kifedha na vifaa tiba.
Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mlipuko huo wa aina ya Bundibugyo Ebola kuwa dharura ya afya ya kimataifa kutokana na kasi ya maambukizi na hatari ya kusambaa katika ukanda mzima.
Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), DRC tayari imerekodi zaidi ya visa 1,000 vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola pamoja na mamia ya vifo, huku Uganda ikiwa na visa vilivyothibitishwa kuongezeka.
Hata hivyo, juhudi za kukabiliana na mlipuko huo zimeanza kukumbwa na changamoto ya upungufu wa fedha baada ya baadhi ya wafadhili waliokuwa wameahidi msaada kupunguza kiwango cha fedha walizokuwa wameahidi.
Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Jean Kaseya, amesema kiwango cha fedha kilichoahidiwa kusaidia mapambano dhidi ya Ebola kimeshuka kutoka karibu dola milioni 500 hadi takribani dola milioni 290 ndani ya siku chache.
“Watu wanakufa. Haiwezekani mtu aahidi msaada leo halafu kesho aseme ilikuwa makosa,” alisema Kaseya katika mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao.
Pamoja na hayo, amepongeza Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kuruhusu baadhi ya fedha zilizokuwa kwenye miradi mingine kuelekezwa kusaidia mapambano dhidi ya Ebola.
Nchi jirani kama Sudan Kusini pia zimeanza kuimarisha ufuatiliaji mipakani kwa kushirikiana na WHO chini ya miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, ili kuzuia maambukizi kuvuka mipaka kutokana na mwingiliano mkubwa wa biashara na usafiri katika ukanda huo.
Wachambuzi wa afya wanaonya kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, mlipuko huo unaweza kuathiri zaidi mifumo dhaifu ya afya barani Afrika, hasa katika maeneo yenye changamoto za usalama, upatikanaji mdogo wa huduma za afya na imani ndogo ya wananchi kwa mamlaka za afya.
Benki ya Dunia imesema mlipuko huu ni ukumbusho wa umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya afya inayoweza kuzuia, kugundua na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kabla hayajasambaa kwa kiwango kikubwa.
