Geita. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Geita, Neema Chozaire anatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho Jumanne, Julai 14, 2026, baada ya kushindwa kufikishwa leo kama ilivyotarajiwa, huku sababu za kuahirishwa kwa hatua hiyo zikiwa hazijawekwa wazi.

Chozaire anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita tangu Juni 29, 2026, alipokamatwa akiwa njiani kuelekea sokoni kununua mahitaji ya nyumbani kwake.

Mpaka leo Jumatatu, Julai 13, 2026 ni siku 15.

Baada ya kukamatwa, baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema walidai kuwa alikuwa ametekwa, wakieleza kuwa simu zake hazikupatikana na juhudi za kumtafuta katika vituo vya polisi hazikufanikiwa, hali iliyozua taharuki miongoni mwa wanachama wa chama hicho.

Hata hivyo, baadaye Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita kupitia taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, Safia Jongo lilithibitisha kumshikilia Chozaire, likisema anachunguzwa kwa tuhuma za makosa ya jinai.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Julai 13, 2026, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obad amesema baada ya shauri hilo kushindwa kutajwa mahakamani leo, sasa limepangwa kusikilizwa kesho asubuhi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Geita.

“Walisema watamfikisha mahakamani leo, lakini hilo halijafanyika. Kwa kuwa muda wa kazi za mahakama ulikuwa umeisha, tumejulishwa kuwa ataletwa kesho kuanzia saa 2:00 asubuhi. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa ametueleza kuwa wamejiandaa kumfikisha mahakamani,” amesema Obad.

Julai 8, 2026, Chadema kwa kushirikiana na Wakili, Beatus Emmanuel wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), walifungua shauri namba 15077 la mwaka 2026 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Geita, wakiwasilisha maombi ya hati ya Habeas Corpus.

Kupitia shauri hilo, wadai wanaitaka Mahakama iamuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita (RPC) pamoja na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO), kufika mahakamani Julai 14, 2026 kueleza sababu za kuendelea kumshikilia Chozaire bila kufikishwa mahakamani au kupewa dhamana.

Obad pia amesema baada ya kufungua shauri hilo, viongozi wa Chadema wameruhusiwa kumuona Chozaire Julai 10, 2026 katika Kituo Kikuu cha Polisi Geita, ambapo walimpelekea mahitaji muhimu ya kibinadamu.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi, taarifa ya awali iliyotolewa na RPC Safia ilieleza kuwa uchunguzi dhidi ya Chozaire kuhusiana na tuhuma za makosa ya jinai ulikuwa unaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *