Koplo alivyowabwaga IGP, RPC kortini, uamuzi wao wabatilishwaKoplo alivyowabwaga IGP, RPC kortini, uamuzi wao wabatilishwa

Kigoma. Zilikuwa siku 540 za panda, shuka ya kupigania haki yake na hatimaye Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma imempa haki kwa kuufuta uamuzi wa Desemba 4, 2024 wa kumfuta kazi, Koplo wa Polisi, Hamisi Sinzumwa.

Hii ni baada ya kushinda shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama namba 4685 ya 2026, aliyokuwa ameyafungua dhidi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na Kamanda wa Polisi (RPC) wa Mkoa wa Kigoma.

Katika shauri hilo ambalo aliwakilishwa na wakili Michael Mwangati, pia aliwaunganisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama wajibu maombi wa tatu na wa nne.

Hukumu ya kufuta maamuzi ya kumfuta kazi askari huyo, imetolewa Mei 28, 2026 na Jaji Augustine Rwizile, baada ya kukubaliana na hoja ya mlalamikaji kuwa kulikuwa na dosari za kisheria wakati wa usikilizwaji wa mashitaka ya nidhamu.

Kiini cha kufutwa kazi kwa askari huyo kilitokana na ajali ya gari la Polisi aina ya GMW Double Cabin namba PT. 5013 alilokuwa akiendesha na hivyo kufunguliwa mashitaka ya kijeshi, ambayo yalimkuta na hatia ya uzembe.

Baraza la Nidhamu ambalo lilimkuta na hatia ya kuendesha gari kwa uzembe, lilipendekeza adhabu tatu, kushushwa cheo kutoka Koplo hadi Konstebo, kupigwa marufuku kuendesha magari ya polisi kwa miaka mitatu na kugharamia matengenezo ya gari hilo.

Hata hivyo, adhabu zilizopendekezwa na mahakama hiyo ya kijeshi zilibadilishwa na mlalamikiwa wa pili ambaye ni RPC Mkoa wa Kigoma na badala yake, akampa adhabu mpya ya kufukuzwa kazi.

Uamuzi huo wa RPC ulipata baraka za IGP na kutupa rufaa iliyowasilishwa kwake na askari huyo akipinga adhabu aliyopewa, ndipo akakimbilia mahakamani na kufungua maombi ya mapitio.

Katika hati ya kiapo kinzani cha pamoja, wajibu maombi walisema uamuzi wao uliegemea ushahidi uliokuwepo katika kumbukumbu na kuzingatia masuala mengine, ikiwamo utetezi wake na na maombi ya kupunguziwa adhabu.

Hata hivyo, katika uamuzi wake, Jaji Rwizile ametupilia mbali hoja zaidi ya nne za maombi hayo, lakini akakubaliana na moja iliyoibuliwa na mleta maombi.

Mwombaji alidai uamuzi wa wajibu maombi haukuungwa mkono na ushahidi wa kutosha, si wa haki na utaratibu haukuwa wa uwazi. Pia alisema ripoti ya uchunguzi wa awali haikuwasilishwa kama kielelezo mbele ya Mahakama ya Kijeshi.

Pia, alidai kuwa mashahidi walitoa ushahidi wao bila viapo.

Wajibu maombi walipinga sababu hiyo wakisema shitaka la kinidhamu dhidi ya mwombaji lilikuwa ni matokeo ya uchunguzi wa kina walioufanya.

Uamuzi wa Jaji

Katika uamuzi wake, Jaji Rwizile amesema amechunguza kiambatisho OSG1, hasa barua kutoka kwa Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kigoma inayotokana na faili la uchunguzi namba KG/TR/AR/08/2024 kupata picha.

“Inaonyesha kuwa uchunguzi wa awali ulifanyika baada ya ajali hiyo. Kwa undani jinsi ilivyo, ripoti ilisema nini kilichotokea Juni2, 2024, matokeo ya uchunguzi na mapendekezo ya kaimu mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa.

“Kwa maoni yangu, mawasiliano yanaonyesha uchunguzi wa awali ulifanyika mara na mapendekezo ni kwamba hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya mwombaji,” aliongeza kusema Jaji.

“Baada ya kupitia vikao vya mahakama ya nidhamu, nimebaini hata hivyo uchunguzi huo wa awali haukuwasilishwa kuwa sehemu ya shauri. Ni mchoro na ripoti ya ukaguzi wa gari pekee ndizo zilizokuwa zimetolewa kama kielelezo.

“Kama ilivyoelezwa na mwombaji, PGO 106(7) (Kanuni za mwongozo wa Jeshi la Polisi) inatoa utaratibu kwa ajili ya maandalizi ya uchunguzi wa awali ili kutathmini ukweli au vinginevyo juu ya mashitaka ya kinidhamu,”alieleza Jaji na kuongeza:

“Kwa kuwa barua ya Kaimu mkuu wa upelelezi mkoa alisema uchunguzi ulifanywa kuhusu ajali hiyo, uchunguzi huo ulipaswa kutolewa wakati wa kusikilizwa kwa shauri dhidi ya mwombaji katika mahakama iliyosikiliza.

“Ilikuwa kweli kuwa sehemu ya rekodi na nadhani, ilipaswa kuwa imetolewa na kumsaidia mwombaji kuandaa utetezi wake,” amesisitiza Jaji Rwizile.

“Fursa ya kujibu (kujitetea) ni pamoja na kutoa hati muhimu za kutosha ili kuruhusu mwombaji kuandaa utetezi wake. Ninaona hiyo bila kuwepo ya uchunguzi wa awali katika shauri katika mahakama ya nidhamu kulifanya shauri hilo kuwa si la haki na bila shaka kumnyima mwombaji kesi ya haki, ambayo ni kinyume na kanuni za haki asilia,” alieleza Jaji Rwizile katika uamuzi wake.

Jaji alisema kwa msingi huo, uamuzi uliotolewa na wajibu maombi umefutwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *