
Simanjiro. Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ruvu Remit wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Godbless Mollel amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la ubadhirifu na wizi wa fedha za kijiji.
Hukumu hiyo imetolewa Mei 28, 2026 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Wilaya ya Simanjiro, Onesmo Nicodemos katika shauri la uhujumu uchumi namba 22415/2025.
Mahakama hiyo imemtia hatiani Mollel katika kesi iliyokuwa ikiendeshwa na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Faustin Mushi.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Nicodemos amesema Mollel amepatikana na hatia katika makosa mawili ya ufujaji na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329.
Ameeleza kuwa Juni 30, 2022, Mollel akiwa Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, alitoa Sh4.3 milioni kutoka katika akaunti ya kijiji.
Imeelezwa kuwa kati ya fedha hizo, Sh3.3 milioni zilifanyiwa ubadhirifu na kuibwa na kuonyesha kuwa zilitumika kwa shughuli mbalimbali za kijiji.
Hakimu amesema mshtakiwa amehukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kosa la kwanza la ufujaji na ubadhirifu.
Katika kosa la pili la wizi akiwa mtumishi wa umma, mahakama imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela.
Hata hivyo, mahakama imeeleza kuwa adhabu hizo zitatumikia kwa pamoja, hivyo mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 20 gerezani.
Mbali na kifungo hicho, Mollel pia ameamriwa kurejesha fedha Sh3.3 milioni alizoziiba na kuzifanyia ubadhirifu.
