
Dar es Salaam. Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’, itacheza na Senegal katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) itakayochezwa Jumanne, Juni 2, 2026 jijini Rabat, Morocco.
Serengeti Boys imeingia fainali hiyo baada ya kuichapa Misri kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika nusu fainali ya kwanza iliyochezwa Alhamisi, Mei 28, 2026 katika Uwanja wa Prince Moulay Hassan, Rabat.
Mechi hiyo imeamriwa na mikwaju ya penalti baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bila kufungana.
Katika nusu fainali ya pili, Senegal imewatupa nje wenyeji Morocco baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 7-6.
Katika muda wa kawaida, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Serengeti Boys kabla ya kuitoa Misri, iliitupa nje Algeria katika hatua ya robo fainali na ilimaliza ikiwa kinara wa kundi C.
Kwa upande wa Senegal, katika robo fainali ilipita mbele ya Mali na iliongoza msimamo wa kundi D.
Timu zote hizo tayari zimeshajihakikishia kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Qatar mwishoni mwa Novemba na mwanzoni mwa Desemba mwaka huu.
Mbali na Tanzania na Senegal, nyingine za Afrika zitakazoshiriki Kombe la Dunia ni Misri, Morocco, Mali, Ivory Coast, Algeria, Cameroon, Uganda na Msumbiji.
