Wananchi Masasi kupata huduma za kibingwa bure kumuenzi MkapaWananchi Masasi kupata huduma za kibingwa bure kumuenzi Mkapa

Dodoma. Madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) wameanza safari kuelekea Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu bure kwa wananchi katika kambi maalumu ya afya.

Kambi hiyo imeandaliwa kuadhimisha miaka sita tangu kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, hayati Benjamin William Mkapa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 29, 2026, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, amesema huduma hizo zitatolewa kwa ushirikiano kati ya hospitali hiyo na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation.

Amesema kambi hiyo itafanyika kuanzia Juni 1 hadi 5, 2026 wilayani Masasi, ikiwa na lengo la kumuenzi kiongozi huyo ambaye hospitali hiyo imepewa jina lake.

Hayati Mkapa alifariki dunia Julai 24, 2020 na kuzikwa Julai 29 mwaka huo katika kijiji cha Lupaso wilayani Masasi, Mkoa wa Mtwara.

“Tunapeleka huduma karibu zaidi na wananchi ikiwa ni sehemu ya kutoa shukrani kwa wananchi wa Mtwara, hasa wa Masasi alikozaliwa Hayati Mkapa. Madaktari wetu wana ari kubwa na wako tayari kutoa huduma,” amesema Profesa Makubi.

Ametaja baadhi ya huduma zitakazotolewa kuwa ni matibabu ya shinikizo la damu, kisukari, saratani, magonjwa ya figo pamoja na huduma za upasuaji kwa wagonjwa watakaobainika kuwa na uhitaji.

Profesa Makubi amesema utoaji wa huduma kwa wananchi wenye uhitaji ulikuwa miongoni mwa maono ya hayati Mkapa.

Amesema katika utekelezaji wa huduma hizo watatumia magari matatu maalumu ya kitabibu yenye vifaa vya kisasa, ambayo tayari yamewahi kutumika katika Wilaya ya Kondoa na nchini Burundi.

“Magari haya ni msaada mkubwa kwetu. Tumefanya kazi hii kwa ushirikiano na wenzetu wa SOTAC na tumeona manufaa yake. Natamani Taifa liwe na magari mengi zaidi ya aina hii,” amesema.

Kuhusu gharama za matibabu, amesema baadhi ya huduma zitahitaji uchangiaji mdogo kutoka kwa wagonjwa huku zaidi ya asilimia 80 ya gharama zikigharamiwa na Benjamin Mkapa Foundation pamoja na Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Operesheni wa Shirika la Sotac, Robert Roal Van den Boss, amesema wanatarajia kutoa huduma bora kwa wananchi wa Masasi kupitia ushirikiano huo.

Amesema katika maeneo mengine waliyowahi kufika ikiwemo Burundi, mwitikio wa wananchi ulikuwa mkubwa kutokana na ubora wa huduma zinazotolewa kupitia magari hayo ya kisasa yenye uwezo wa kufanya kazi kama hospitali kamili.

“Hakuna atakayepata usumbufu kwa sababu magari haya yana vifaa vyote muhimu vya matibabu,” amesema Robert.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *